ad

ad

Miss Utalii Arusha atwaa tuzo ya SJMC

FAINALI za Utalii Tanzania zimeendelea kushika kasi kwa warembo kushindania tuzo mbalimbali, ambapo juzi amepatikana mshindi wa Tuzo ya Habari (Media Awards).

Katika shindano hilo lililofanyika viunga vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), ambao ni wadhamini wakuu wa tuzo hiyo, mshindi wa kwanza aliibuka Miss Utalii Tanzania 2012/13 kutoka mkoa wa Arusha, Rose Godwin.

Nafasi ya pili ilikwenda kwa Miss Utalii kutoka mkoa wa Rukwa, Neema Kafanunzi, na mshindi wa tatu alikuwa Miss Utalii kutoka Mtwara, Baby Juma.
Katika shindano hilo, zaidi ya warembo 30 walipanda jukwaani kwa kuelezea mada ya vivutio vya mikoa wanayowakilisha na kisha majaji kutoka SJMC, walitangaza warembo walioingia sita bora.

Baadaye waliulizwa maswali kila mmoja na lake na pia swali la pili lilikuwa ni la jumla ambapo wote waliulizwa.
Mshindi wa SMJC Miss Tourism Tanzania 2012/13 Media Award, Rose Godwin, alipata zawadi ya udhamini wa kusomeshwa katika shule hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoa tuzo, Rais wa Miss Utalii Tanzania, aliwashukuru wadhamini wakuu wa tuzo hiyo, SJMC, kwa kutoa heshima kubwa ya kumsomesha mshindi huyo na kuongeza kuwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha.
Powered by Blogger.