Wazungu wasituletee ukoloni – Na Paul Nabiswa
Paul Nabiswa
Mojawapo wa sifa kuu za lugha yoyote ile
ulimwenguni ni kuwa ‘lugha hukua’. Katika misingi hiyo ni sawa kusema
kuwa lugha hujisimamia ikiwa ina msamiati mpana tena wa kutosha.
Ni sawa kusema kuwa lugha
inaponawiri wasemaji na wazawa wake hujimudu kuitumia kwa wepesi bila
mahangaiko ya kutafuta msamiati ama kutumia msamiati mdogo tu.
Nimeanzia mbali kidogo kwa sababu nimetambua
kuwa waswahili wananyanyaswa na wazungu katika kutumia lugha yao ya
Kiswahili. Nasema wazungu wametukalia kwa sababu wamewatumia waswahili
wenyewe kudunisha lugha yao.
Katika taaluma ya uanahabari watangazaji wa Kiswahili wanabanwa zaidi ili watumie maneno fulani mahsusi.
Hii inafanya lugha ya Kiswahili kuonekana kuwa
ina umasikini mkubwa mno wa maneno. Wazungu wanahabari wenyewe wanatumia
visawe vya maneno na hakuna anayewakashifu.
Japokuwa tunajua kuwa umuhimu wa habari ni
kuwasiliana, lakini palepale ni vyema kutambua kuwa kubadilisha maneno
katika taarifa ni hatua muhimu.
Mwanzo inaonysha kuwa kuna demokrasia katika lugha ya Kiswahili, na pili inaleta picha kuwa Kiswahili kina msamiati mpana.
Katika kutoa mifano utapata wazungu wakisema
figures, digits, numbers na statiscs kwa maana ya idadi. Hata hivyo
Mswahili hujikita katika majina mawili tu. Takwimu na tarakimu. Kenya
wanatumia sana Takwimu.
Je makosa yako wapi mimi nikisema mahaba,
mwenzangu aseme huba, mwengine aseme mapenzi na hata mwingine aite hawa?
Waswahili tumefinywa eti tuseme tu mapenzi na hao wanaosema hivyo ni
watu wenye uwezo wa kusema Kiswahili lakini wanajifanya kuwa wamo katika
mbawa salama za Kiingereza.
Kuna haja ya dharura kwa Kiswahili kupata
wakombozi wao ili meli yao isizamishwe na mawimbi ya Kiingereza. Ni
muhimu kutaja kuwa Kiswahili kina zaidi ya lahaja ishirini na ikiwa jina
haliko kwa lahaja ya Kimtang’ata kwa mfano si dhambi jina lenye mizizi
ya lahaja ya Kivumba kutumiwa.
Vivyo hivyo wapemba hawatakiwi kusutwa
wanapotumia maneno yasiyopatikana katika lahaja ya Kiswahili sanifu.
Yaani lahaja inayotumika katika mazingira rasmi.
Hivyo basi nikisema kidole na jirani yangu asema
chanda ni neno moja. Nikiona ni bora kuita mshipi na mama yangu aone
neno mkanda linafaa hamna dhambi. Kwa hoja hiyo hiyo, ikiwa kwetu
tumezoea kumwita mama ya mzazi nyanya na mwingine aseme bibi pia ni
sawa. Kadhalika ukimwita mama kuwa ni nyina hutakiwi kusulubiwa.
Ikiwa wasemaji wa Kiswahili wataanza kufikiria mambo kwa mawanda hayo, ni sawa kusema kuwa Kiswahili kitakuwa kimepata watetezi.
Hata hivyo ni muhimu kupima mahali
unapozungumzia maneno hayo. Ikiwa ni mazingira ya mazungumzo ya kawaida
ni sawa zaidi lakini darasani kidogo kuna utata. Kwa hivyo wazungu
wakiachwa watumie maneno yao, waswahili wasifinywe wakifanya hivyo.
Paul Nabiswa ni mwanahabari wa BBC na hayo ni maoni yake.

Post a Comment