Usalama waimarishwa Libya
Majeshi ya usalama yamewekwa katika hali ya juu ya tahadhari nchini
libya leo Jumapili(17.02.2013)wakati taifa hilo linaadhimisha miaka
miwili tangu kuanza kwa uasi ambao ulimwondoa madarakani dikteta Moammer
Gaddafi.
Mipaka imefungwa na baadhi ya safari za ndege za kimataifa zimefutwa kwa muda huku kukiwa na hofu ya kuzuka kwa ghasia mpya.
Maadhimisho hayo ya vuguvugu la mapinduzi ambalo lilimalizika kwa
kuuwawa kwa Gaddafi hapo Oktoba 2011 yanakuja wakati viongozi wapya wa
Libya wanakabiliana na wakosoaji ambao wanatoa wito wa kile
kilichoelezwa kuwa ni "mapinduzi mapya", na wanawashutumu viongozi hao
kwa kushindwa kuleta mageuzi ambayo yanahitajika sana.
Sherehe za bila kupangwa zinatarajiwa nchini Libya
Siku ya Ijumaa , maelfu ya watu walikusanyika katika miji mkuu ya
Tripoli na Benghazi kusherehekea mwanzo wa maandamano hayo Februari 15,
2011, ambayo yalizusha uasi siku mbili baadaye.
Hakuna sherehe rasmi
Hakuna mpango maalum rasmi ulioandaliwa na serikali kwa ajili ya
maadhimisho haya leo Jumapili(17.02.2013), lakini maafisa wamechukua
hatua zenye lengo la kuzuwia ghasia zozote katika siku hii ambayo
sherehe za bila kupangwa zinatarajiwa.
Mipaka ya Libya na Misri na Tunisia imefungwa kuanzia Alhamis kwa muda
wa siku nne, na safari zote za ndege za kimataifa zimefutwa kwa muda,
isipokuwa katika uwanja wa ndege wa Tripoli, na mji wa pili kwa ukubwa
nchini humo wa Benghazi, ambao ulikuwa ni shina la uasi wa hapo Februari
17.
Waziri mkuu Ali Zeidan amesema kuwa hatua hizo zilichukuliwa ili kuepuka
, "juhudi zozote za kuchafua usalama wa Libya na kuharibu sherehe za
maadhimisho hayo ya mapinduzi.
Vizuwizi vya barabarani pia vimewekwa katika mji mkuu Tripoli na Benghazi.
Wito wa kukaidi sheria
Makundi ya upinzani yanadai kuwa maafisa wa zamani wa utawala wa Gaddafi
wanazuiwa kushika nyadhifa za umma, na vijikaratasi vilivyosambazwa
mjini Tripoli vinatoa wito wa " kufanyika uasi wa umma", na umma
kutofuata sheria ili kuiangusha serikali ya hivi sasa.
Haijafahamika wazi ni nani anahusika na vijikaratasi hivyo na wito huo
wa kufanya upinzani, lakini maafisa wa Libya pamoja na mashirika kadha ,
ikiwa ni pamoja na makundi ya Kiislamu, wanashutumu mabaki ya utawala
wa zamani kwa kuchochea ghasia , ili "kupandikiza hali ya kutokuwa na
amani na vurugu".
Maafisa wamesema kuwa vibali maalum vitahitajika kwa ajili ya kufanyika
"maandamano ya amani", na wametishia kutumia nguvu dhidi ya mtu yeyote
atakayejaribu kuchafua maadhimisho hayo.
Benghazi waanzisha vikundi vya kujilinda
Wakaazi wa mji wa benghazi , ambao wameathirika na ghasia zinazohusishwa
na makundi ya Waislamu wenye itikadi kali ambao wanaelekeza ghasia zao
dhidi ya mashirika ya kimataifa pamoja na balozi mbali mbali , wameweka
vikundi vya ulinzi katika maeneo yao.
Mji huo ulikumbwa na ghasia tarehe 11 mwezi Septemba mwaka jana kutokana
na shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani ambapo balozi wa
Marekani Chris Stevens aliuwawa pamoja na watu wengine watatu raia wa
Marekani.
"Suala la usalama ni moja kati ya changamoto kubwa zinazoikabili nchi
hiyo, hususan kuenea kwa silaha na maelfu ya wafungwa kukimbia kutoka
jela , wakati wa mapinduzi, mchambuzi wa masuala ya kisiasa Suleyman
Azqim ameliambia shirika la habari la AFP.

Post a Comment