Tanzania Kinara Utawala Bora Afrika Mashariki....Pia imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Orodha
ya Hali ya Demokrasia Duniani (2017 Democracy Index) iliyozinduliwa
Februari 2, mwaka huu na kuchapishwa na jarida kongwe na mashuhuri
duniani la The Economist imeitaja Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika
maswala ya Utawala Bora kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Mkurugenzi wa Idara ya
Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi alisema
kuwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwenye masuala ya Utawala bora
imeweza kusaidia ukuaji wa Uchumi wake.
“Utawala
Bora ni kigezo muhimu cha ukuaji wa uchumi na hata ustawi wa jamii,
kama ambavyo Orodha ya Hali ya Demokrasia Duniani iliyotolewa na jarida
kongwe na mashuhuri duniani la The Economist imeitaja Tanzania ni ya
kwanza katika ukanda wa EAC, ikifuatiwa na nchi za Kenya, Uganda,
Rwanda, Burundi na DRC.
Pia,
ripoti ya Foresight Afrika na taarifa ya Uchumi ya Benki ya Dunia
vyote vimeitaja Tanzania kuwa katika nchi tano Bora za Afrika ambazo
uchumi wake unakua kwa kasi katika mwaka 2018, nchi hizo ni Ghana,
Ethiopia, Kodivaa , Senegali na Tanzania”.
Aidha,
Dkt. Abbasi alisema kuwa ukuaji huo wa uchumi ni dhamira isiyoyumba ya
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, ikiwa ni
pamoja na kuhakikisha uchumi mkuu unaendelea kujiakisi katika maisha ya
watanzania kupitia utoaji wa huduma kwa wananchi na kuboresha sekta
mbalimbali.
Katika
sekta ya Afya, Dkt. Abbasi alisema kuwa pamoja na ujenzi wa vituo vya
afya unaoendelea nchi nzima na uboreshaji wa hospitali, Serikali
imetenga bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka Bilioni 31 mwaka 2015 hadi
Bilioni 269. Aidha, bajeti ya sasa imewezesha Serikali kuboresha
usambazaji wa dawa hadi kufikia asilimia 86 ya uhakika wa kupatikana
dawa muhimu.
Bajeti
hiyo imewezesha ukarabati wa wodi 5 za ICU na kuongezwa vitanda
kutoka 21 mpaka 75, kununua mashine mpya za CT-Scan yenye uwezo mkubwa
imenunuliwa katika hospitali ya Muhimbili na Taasisi ya Mifupa na
Mishipa ya fahamu (MOI) zenye uwezo mkubwa ambapo wastani wa wagonjwa
wanaopimwa imepanda kutoka 20 hadi 50 kwa siku.
Vifaa
vingine vilivyonunuliwa ni pamoja na mashine 14 za upasuaji (diathermy
machines) na mashine za kuchuja damu kwa ajili ya wagonjwa wa figo
zipatazo 25 na kuongeza uwezo wa kuhudumia wagonjwa kutoka 68 kwa siku
hadi 126.
Uboreshaji
huo wa sekta ya afya umeifanya Muhimbili kuwa hospitali ya kwanza ya
umma katika ukanda wa Afrika Mashariki kutoa huduma za juu za kibingwa
hasa oparesheni ya kuweka vifaa vya kusaidia kusikia ambapo watoto 5
waliokuwa awali hawasikii kabisa walifanyiwa oparesheni mwaka jana na
kusikia kwa mara ya kwanza katika maisha yao. Wengine 6 wamefanyiwa
wiki iliyopita.
Katika
sekta ya Sekta, Msemaji huyo wa Serikali alisema kuwa lengo la
Serikali ni kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 85 vijijini ifikapo
mwaka 2020 kutoka asilimia 67.7 mwaka 2015, makao makuu ya mikoa
asilimia 95, Dar es Salaam asilimia 95 na miji mikuu ya wilaya asilimia
90 ifikapo 2020.
Ambapo
hadi sasa kwa ujumla kuna takribani miradi 1,423 imekamilika na kuna
vituo vya maji 117,190 vyenye uwezo wa kuhudumia watu milioni 29 sawa na
asilimia 79. Katika miaka hii miwili pekee zaidi ya miradi 388
ilikamilishwa.
Dkt.
Abbasi, anafafanua kuwa katika usambazaji wa umeme mijini na vijijini
kazi imeendelea kwa kasi kubwa. Katika kutekeleza Mradi wa REA III,
kiasi cha shilingi bilioni 985.9 zitatumika kuwafikishia wananchi umeme
katika programu maalum iliyoanza kutekelezwa.
Alisititiza
kuwa, “Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli, imedhamiria kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili
wananchi si tu kwa maneno bali kwa vitendo, mfano namna ambavyo
Serikali imeongeza wigo wa barabara vijijini na mijini, pamoja na
kuundwa kwa wakala maalum (TARURA) ambao utajikita zaidi katika
kuharakisha ujenzi wa barabara za vijijini”
Aliongeza
kuwa mwaka huu Serikali inakusudia kutekeleza upanuzi wa njia za
mwendokasi jijini Dar es Salaam kwenda njia za barabara ya Kilwa kwenda
Mbagala yenye urefu wa kilomita 19 na barabara ya Uhuru kwenda
Gongolamboto yenye urefu wa kilomita 23.9.
Aidha,
Dkt Abbasi amewakumbusha watanzania kuwa wazalendo, kuunga mkono
jitihada za Serikali kufanya kazi kwa bidii, kama ambavyo Serikali ya
Awamu ya Tano inasisitiza wananchi kufanyakazi ili kuijenga Tanzania
uitakayo.
Post a Comment