NEC YAJIBU HOJA 6 ZA CHADEMA
Jana
16/02/2018 baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe, walifika
ofisi za Tume ya Taifa kuwasilisha malalamiko yao kadhaa ambayo walikuwa
wanahitaji ufafanuzi kutoka NEC kuhusu uchaguzi mdogo wa jimbo la
Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya kupitia hoja za Chadema, inapenda kutoa ufafanuzi wa hoja hizo:
Hoja
ya kwanza, kwamba, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Uchaguzi la
Kinondoni amekaa kuwaapisha mawakala wa ziada wa upigaji kura kutoka
CHADEMA ambao ni asilimi kumi na tano (%15) ya Mwakala wote
wanaohitajika kwenye vituo 613, na kuwa utaratibu huu umekuwa unatumiwa
katika Chaguzi zilizopita.
Ufafanuzi,
kwa mujibu wa kifungu cha 57(1)(2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi,
Sura ya 343, kila Chama cha Siasa kilichopata ridhaa ya kuweka wagombea,
kinaweza kuteua wakala mmoja wa upigaji kura kwa kila kituo ndani ya
jimbo.
Aidha,
Kanuni ya 48(2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za
mwaka 2015 inakitaka kila Chama cha Siasa kinachoshiriki katika Uchaguzi
siyo zaidi ya siku saba (7) kabla ya siku ya Kupiga Kura kiwe
kimewasilisha kwa maandishi kwa Msimamizi wa Uchaguzi majina ya
Mawakala, anwani zao na vituo walivyowapangia.
Vilevile,
kifungu cha 57(3) cha Sheria tajwa, kimeweka utaratibu na mazingira
ambayo wa Chama kilichosimamisha Mgombea kuweka wakala mbadala wa
upigaji kura.
Tunashauri CHADEMA kuzingatia matakwa ya kifungu cha 57(3) cha Sheria husika pale patakapohitajika uwepo wa mawakala mbadala.
Hoja
ya pili, kwamba, Msimamizi wa Uchaguzi amekataa kuwaruhusu na Viongozi
wa CHADEMA kuwa Mawakala wa upigaji kura, kwa maana hiyo atakichagulia
chama mawakala wa upigaji kura, na kwamba, orodha ya viongozi hao
watambuliwe na kuapishwa kuwa Mawakala wa upigaji kura.
Ufafanuzi,
kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343
kikisomwa pamoja na Kanuni ya 48(2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais,
Wabunge na Madiwani za mwaka 2015 vimeweka utaratibu wa muda wa
kuwasilisha orodha ya mawakala na muda wa kuwaapisha kuelekea siku ya
Uchaguzi.
Kwa
maana hiyo, siku ya kuwasilisha na kuapishwa mawakala ilikuwa tarehe 10
Februari, 2018. Hivyo, kupokea na kuwaapisha mawakala wengine itakuwa
ni kinyume cha masharti yaliyowekwa chini ya kifungu na kanuni
niliyoitaja.
Hoja ya tatu, kwamba, Mawakala wa upigaji kura wa CHADEMA hawajapewa nakala za hati zao za kiapo cha kutunza siri.
Ufafanuzi,
kwa mujibu wa Kanuni ya 48(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani za mwaka 2015 kila Wakala wa Upigaji kura anapaswa kuapa kiapo
cha kutunza siri katika Fomu Na. 6 kabla ya kutekeleza wajibu wake
katika kituo cha kupigia kura.
Kwa
takwimu zilizopo jumla ya vituo vya kupigia kura ni 613 na jumla ya
Vyama vya Siasa 12 vinashiriki katika uchaguzi huo. Kwa kuwa kila Wakala
mmoja alijaza nakala mbili ya Kiapo cha kutunza siri, hapo unazungumzia
uwepo na viapo 14,712.
Kanuni
ya 48(3) ya Kanuni tajwa, Wakala wa Upigaji Kura atapaswa kupewa barua
na Msimamizi wa Uchaguzi ya kumtambulisha kwa Msimamizi wa Kituo cha
kupigia kura. Hapa unazungumzia nakala 22,068 kwa sababu, nakala moja
atapewa wakala, nakala itabaki kwenye jalada kwa kumbukumbu na nakala
itapelekwa kwa Msimamizi wa Kituo kwa urahisi wa rejea.
Hata
hivyo, taarifa tulizonazo ni kuwa, Msimamizi wa Uchaguzi ameanza kutoa
nakala hizo za Viapo kwa Wawakilishi wa Vyama vyote vinavyoshiriki
Uchaguzi mdogo ili wawapatie Mawakala wa Vyama husika. Utaratibu huu
nidyo uliokubaliwa kwenye vikao vya Msimamizi wa Uchaguzi na Wawakilishi
wa Vyama.
Hoja
ya Nne, kwamba, Msimamzi wa Uchaguzi ametoa maelekezo kuwa Mawakala
wawe na utambulisho wa kumtambulisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi mbali ya
barua kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi. Utambulisho huo ni Vitambulisho
vya Mpiga Kura, Leseni ya Udereva, Hati ya Kusafiria na Kitambulisho cha
Kitaifa.
Ufafanuzi,
kwa kuzingatia matakwa ya vifungu vya 13(2) na 61(3)(a) vya Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume imeruhusu wapiga kura
walioandikishwa kwenye Daftari ya Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2015 na
ambao wamepoteza kadi za kupigia kura au zimechakaa au zimeharibika,
watumie Kitambulisho cha Taifa, Hati ya Kusafiri na Leseni ya Udereva
kupiga kura.
Kwa
kuwa Wakala wa upigaji kura aliyeandikishwa ndani ya Jimbo la Kinondoni
anayohaki ya kupiga kura, na kwa kuwa inawezekana wakawa wamepoteza
kadi za kupigia kura au zimeharibika au kuchakaa. Hivyo, mahitaji ya
vitambulisho hivyo ni kuwezesha utekelezaji wa matakwa ya vifungu
vilivyonukuliwa.
Hata
hivyo, uzoefu unaonesha kuwa, siku ya upigaji kura, baadhi ya mawakala
wanao kwenda vituoni siyo Mawakala waliokura kiapo cha kutunza Siri
katika Fomu Na. 6 na siyo waliotambulishwa na Msimamizi wa Uchaguzi kwa
Msimamizi wa Kituo.
Hivyo,
tunapenda ieleweke kuwa, endapo itatokea wakala wa upigaji kura aliyepo
katika kituo cha kupigia kura siyo aliyeapa kiapo cha kutunza siri na
siye aliyetambulishwa na Msimamizi wa Uchaguzi, utakuwa ni ukiukwaji wa
Sheria, na atachukuliwa hatua za kisheria mara moja.
Hoja ya Tano, kwamba, Msimamizi wa Uchaguzi hajatoa na kuweka wazi kuhusu kituo kikuu cha majumuisho.
Ufafanuzi,
Tume imejiridhisha kuwa Msimamzi wa Uchaguzi kupitia barua yenye Kumb.
Na.KMC/U.21/06/119 ya tarehe 14 Februari, 2018 alivijulisha Vyama vyote
vya Siasa vinavyoshiriki Uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Kinondoni
eneo na muda wa kuanza kujumlisha hesabu za kura. Kwa mujibu wa barua
hiyi ambayo CHADEMA walipatiwa, Kituo cha majumuisho ya hesabu za kura
ni Biafra na zoezi la majumuisho ya hesabu za kura litaanza majira ya
saa kumi na mbili jioni (12:00) siku ya Uchaguzi.
Aidha,
kupitia barua hiyo, Msimamizi wa Uchaguzi alivitaka Vyama vya Siasa
vyenye wagombea kuwasilisha majina ya Mawakala wa Kujumlisha Kura.
Hoja
ya Sita, kwamba, Uteuzi wa Wasimamizi wa Vituo ambao ni Makada wa Chama
cha Mapinduzi kutoka Temeke, Ilala na Kinondoni na majina yao kutowekwa
hadharani.
Ufafanuzi,
Kifungu cha 7(4)(5) 2015 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343,
ikisomwa pamoja na Kanuni ya 14 na 15 ya Kanuni cha Uchaguzi wa Rais,
Wabunge na Madiwani za mwaka 2015 na kipengele cha 10.1.(ii) cha
Maelekezo kwa Vyama vya Siasa na Wagombea ya mwaka 2015 kwa pamoja
umewekwa utaratibu wa namna ya kuwapata Wasimamizi wa Vituo na
Wasimamizi Wasaidizi wa Vituo na namna Vyama vinavyoshiriki uchaguzi
vinavyoweza kuhusishwa katika utaratibu wa kuwapata Watendaji hao.
Kwa
mujibu wa taarifa ambazo Tume inazo, taratibu zote za kuwapata
watendaji hao zilizingatiwa ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi za kazi,
waliohitaji kuomba, kuchujwa waliokuwa na sifa zinazohitajika,
kufanyika usaili na majina ya walioteuliwa kuwa Wasimamizi wa Vituo na
Wasimamizi wa Vituo Wasaidizi kubandikwa kwenye mbao za matangazo katika
Ofisi za Kata zote kumi katika Jimbo la Kinondoni.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa barua yenye Kumb. Na. KMC/U21/06/12 ya tarehe 11
Februari, 2018 Msimamzi wa Uchaguzi aliwasilisha orodha ya Watendaji hao
kwenye Vyama vinavyoshiriki katika Uchaguzi.
Kuhusu,
kuwepo kwa wapiga kura 3065 watakaopiga kura na ambao hawakuadikishwa
katika Jimbo la Kinondoni. Tunapenda kuwakumbusha kuwa, kifungu cha
63(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kimeweka utaratibu wa
nani anayeruhisiwa kupiga kura. Hivyo, hakuna atakayeruhusiwa kupiga
kura iwapo hajaandikishwa na jina lake halipo katika orodha ya wapiga
kura waliopo katika daftari.
Nashukuru kwa ushirikiano wako.
Kailima, R.K
MKURUGENZI WA UCHAGUZI
Post a Comment