Michirizi Ya Damu - 15
Akaanza kuelekea mpaka kule alipokuwa rubani, akamuuliza juu ya hali iliyokuwa ikiendelea, akamwambia kwamba walikuwa usawa wa bahari, mita mia moja na ilikuwa ngumu kurudi kwani yeye mwenyewe alishindwa kabisa kuiweka sawa ndege hiyo.
“Kwa hiyo?”
“Hatujui tufanye nini! Tusalini sala zetu za mwisho!” alisema rubani, hakuona kama wangeweza kupona kutokana na hali iliyokuwa ikiendelea mahali hapo.
Hakukuwa na mtu aliyejiona kuwa salama, kila mmoja aliona kuwa huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Wakachukua maparachuti yaliyokuwa katika viti vyao kwa ajili ya kurukia baharini ambapo kulionekana kuwa salama kwa maisha yao.
Nje, hakukuwa na mwanga wa kutosha, mawingi mazito yalitanda na upepo mkali uliendelea kuvuma kama kawaida. Chini, hawakuona kitu kwani mawingu yale yalianza kushuka chini kutokana na upepo huo uliokuwa ukiendelea kuvuma kama kawaida.
“Let’s jump,” (turuke) alisema De Leux huku akimwangalia mwenzake, tayari maparachuti yalikuwa migongoni mwao.
“What about me?” (na mimi je?) aliuliza Fareed.
Hawakumjibu kitu chochote zaidi ya kumwangalia. Wakaufungua mlango wa ndege na kutokana na upepo mkali uliokuwa ukiendelea kuvuma, hali ikawa mbaya zaidi, ndege ikayumbishwa kupita kawaida, De Leux na mwenzake wakaruka na maparachuti yale kuelekea chini huku wakimwacha Fareed akiwa na rubani wa ndege ile.
Alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alitamani kuruka lakini alishindwa kufanya hivyo. Haraka sana akamfuata rubani na kuanza kuzungumza naye, alimwambia kwamba lengo lake lilikuwa ni kuruka kwani vinginevyo ndege ile ingepata ajali na kufa humo.
Akamtaka kushusha ndege, kutoka kwenye umbali wa mita mia moja mpaka hamsini ili aweze kujirusha baharini. Kwanza rubani akaogopa, aliijua bahari hiyo, ilikuwa hatari kuliko bahari nyingine kwani baridi lililokuwa likipiga humo, lilikuwa kubwa na ndiyo bahari ileile iliyoua watu katika meli ya Titanic miaka hiyo ya nyuma.
“It’s impossible! You can’t jump,” (haiwezekani! Huwezi kuruka) alisema rubani yule huku akimwangalia Fareed.
Fareed hakutaka kuelewa, alichokitaka kilikuwa ni kuyaokoa maisha yake kutoka katika ndege ile. Alimwangalia rubani, aliangalia mbele ya ndege ile, ni kweli kulikuwa na upepo mkali na mawingu mazito yalitanda kiasi kwamba ilikuwa vigumu sana kuona mbele.
Aliendelea kumwambia rubani yule ashushe ndege kwa kiasi fulani ili aweze kuruka. Baada ya kubembelezwa sana hatimaye rubani huyo akaishusha ndege hiyo kwa umbali wa mita hamsini kisha kumruhusu Fraeed kuruka.
“Una parachuti?” aliuliza rubani.
“Hapana!”
“Boya!”
“Hapana!”
“Hebu subiri!” alisema rubani huyo.
Akaangalia chini ya kiti chake, akaona boya la kuvaa na kumwambia Fareed alivae kwani hapo alipokuwa akirukia palionekana kuwa sehemu ya hatri sana. Hilo halikuwa tatizo, akalichukua boya hiyo, akalivaa, akaufungua mlango na kisha kuruka baharini.
Alikuwa kwenye hali mbaya, wakati mwingine alishindwa kuhema vizuri kutokana na upepo mkali uliokuwa ukiendelea kuvuma. Baada ya sekunde chache akatumbukia ndani ya maji.
Bahari ilichafuka, kulikuwa na mawimbi makubwa yaliyopiga huku na kule. Fareed alipelekwa huku na kule, hakutulia baharini pale, kitu kilichokuwa kikimsaidia kilikuwa ni lile boya tu alilokuwa amelivaa.
Ilikuwa ni mchana lakini kitu cha ajabu, kulionekana kama jioni, hakuweza kuona hata mita kumi na tano kutoka pale alipokuwa. Alikiona kifo, mawimbi makubwa yaliendelea kumpiga na kumpeleka huku na kule mpaka kuona kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
“Mungu nisaidie,” alisema Fareed huku mawimbi yakiendelea kumpeleka huku na kule.
****
Bilionea Belleck alikuwa kwenye kiti chake ofisini kwake, masikio yake yalikuwa kwenye simu yake iliyokuwa mezani. Alikuwa na presha kubwa, alitaka kuona simu kutoka kwa De Leux ikiingia na kumpa taarifa kwamba tayari walifanya mauaji ya Fareed ili moyo wake uridhike.
Muda ulizidi kusonga mbele, dakika ziliendelea kukatika lakini hakukuwa na taarifa yoyote ile. Moyoni mwake akawa na hofu, akahisi kabisa kwamba watu hao walishindwa kumuua au kulikuwa na tatizo jingine ambalo lilitokea.
Aliwaambia kwamba walitakiwa kufanya mauaji hayo haraka sana baada ya ndege kupaa lakini kitu cha ajabu kabisa hakukuwa na simu iliyoingia kumpa taarifa hiyo ambayo aliamini kwamba ingeufanya moyo wake kumtukuza Mungu kwa hicho kilichotokea.
Baada ya kupita saa mbili, akaamua kumpigia mwanaume huyo ili kujua ni kitu gani kiliendelea. Simu haikuwa ikipatikana, ilionekana kuzimwa kitu kilichomuudhi sana Belleck kwa kuona kwamba amedharauliwa.
Alichokifanya ni kumtumia ujumbe wa sauti (voice mail) ili atakapoiwasha simu yake aweze kuipata sauti hiyo na kumwambia kitu kilichokuwa kimeendelea.
“Kitu gani kinaendelea? Kwa nini umekuwa kimya sana? Mmekamisha au bado hamjakamilisha? Hebu ukifungua simu nitafute nijue manake nilishatuma pesa, kama amekufa niambie nizitoe pesa kabla hajathibitisha kuzipata,” alisema Belleck huku simu ikiwa sikioni mwake.
Moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, bado aliendelea kuwa na hofu kwamba inawezekana kulikuwa na jambo lililokuwa limetokea huko. Hakutulia, moyo wake ulikuwa na shaka tele kwa kuona kwamba kama Fareed hakuuawa basi kile kiasi alichokuwa amemtumia, kingeweza kuondoka mikononi mwake jumla kama tu mwanaume huyo angethibitisha kukipokea ndani ya siku saba.
Alitaka afe haraka iwezekanavyo! Alifanya kazi aliyoitaka, mtu aliyetakiwa kuuawa aliuawa hivyo alichokuwa akikiangalia kwa sasa ni kupewa taarifa kwamba kazi ile ilifanyika.
Siku ya kwanza ikapita, ukimya ukatawala, siku ya pili nayo ikapita, ukimya ukatawala, siku ya tatu na nne nazo zikaingia lakini hakukuwa na taarifa yotoye ile kama Fareed aliuawa au la, mbaya zaidi hata alipokuwa akimpigia simu rubani, naye hakuwa akipatikana.
****
Fareed alikuwa akielea juu ya maji, alipelekwa kila kona na kitu kilichokuwa kikimsaidia asizame ni lile boya alilokuwa amelivaa. Aliendelea kuelea mpaka bahari ilipotulia, akaangalia huku na kule na kwa mbali sana akafanikiwa kukiona kisiwa kimoja, hakikuwa kikubwa sana, kilikuwa kidogo hivyo kuanza kupiga mbizi kuelekea kule.
Alichoka, maji yalimchosha, yalimpeleka huku na kule, mikono yote alihisi ikiuma kupita kawaida. Japokuwa kisiwa kile kilionekana kuwa kama umbali wa nusu kilometa lakini alitumia dakika arobaini na tano mpaka kukifikia.
Kilikuwa kisiwa kilichokuwa na miti mingi, hakujua kilikuwa nchi gani lakini kwa jinsi kilivyoonekana, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiishi humo. Akazunguka huku na kule, aliogopa, moyoni mwake alihisi kama angekutana na watu wabaya, au wala wala watu waliokuwa wakipatikana katika nchi nyingine lakini kwa bahati nzuri kwake hakuweza kukutana na mtu yeyote yule.
Alitafuta sehemu chini ya mti na kutulia, macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule kutafuta msaada, pale alipokuwa ilikuwa ni sawa na mtu aliyetengwa, kila kona alipoangalia, hakuona kitu au mtu yeyote yule zaidi ya kisiwa kile kuzungukwa na bahari kila upande.
Alihisi baridi, hicho kilikuwa kisiwa kilichokuwa katika Bahari ya Atlantiki, moja ya bahari zilizokuwa na baridi kali. Alibaki akitetemeka pale alipokuwa kiasi kwamba mpaka akahisi kuwa muda wowote ule angeweza kufa.
Alitulia kwa saa moja, hakuona msaada wowote ule zaidi ya maji yale yaliyokuwa yamezunguka kisiwa kile. Alikaa mpaka usiku, giza likaingia, hakuwa na sehemu salama ya kulala zaidi ya mtini, tena huku akiangalia huku na kule.
Usiku mzima alikesha macho, moyo wake ulimwambia kwamba kungekuwa na msaada kutoka mahali fulani lakini kitu cha kushangaza mpaka inafika asubuhi hakukuwa na msaada wowote ule alioweza kuupata kitu kilichomfanya kukosa tumaini la kuondoka kisiwani hapo.
“Inamaana ndiyo nitakufa hapa?” alijiuliza huku akiangalia huku na kule.
“Labda! Lakini haiwezekani hata kidogo! Siwezi kufa kirahisi namna hii,” alijisemea huku akiteremka kutoka mtini.
Siku hiyo alishinda katika kisiwa hicho, alipokuwa akisikia njaa, aliingia katika pori lililokuwa kisiwani hapo, akachuma makomamanga na kuanza kula. Hayo ndiyo yakawa maisha yake, alipata tabu mno kisiwani humo, alitamani kuondoka lakini ilishindikana kwa kuwa tu hakukuwa na msaada wowote uliotokea.
Alidhamiria kurudi nchini Marekani, ilikuwa ni lazima kwenda kukamilisha kazi aliyokuwa ameiacha. Aliwaua watu wawili ambao walidiriki kumuondoa duniani lakini kutokana na ujanja wake, akanusurika kufa.
Hakutaka kuwaacha watu hao, akawaua na hivyo kubaki mtu mmoja ambaye alikuwa Padri Luke. Naye ilikuwa ni lazima amuue kwa kile alichomfanyia. Moyo wake haukujisikia hukumu wala huzuni, alichokuwa akikihitaji ni kuhakikisha mwanaume huyo anakufa kama walivyokufa wenzake.
Muda ulizidi kwenda mbele, alishindia makomamanga, hakuweza kupata chakula kingine zaidi ya hicho. Aliendelea kuishi kwa mateso makubwa, kila siku akawa anapigwa na baridi kali, alihuzunika mno, aliumia moyoni mwake na wakati mwingine alihisi kwamba huko ndipo ambapo kungekuwa nyumbani kwake milele, hakuona kama angeweza kuondoka mahali hapo salama.
Kila wakati ilikuwa ni lazima kuangalia huku na kule, alitaka kuona kama angebahatika kuona meli yoyote ile ili aweze kuomba msaada lakini hilo halikuwezekana, kila kona alipoangalia aliona kuwa peupe.
“Mungu wangu! Ni nini hiki?” Fareed alishtuka, ghafla tu akaanza kusikia maumivu makali ya tumbo, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea tumboni mwake, akalishikilia tumbo lake vilivyo, alisikia maumivu mahali ambayo hakuwahi kuyasikia kabla.
Akaanza kusikia kichefuchefu na kuanza kukohoa, madonge ya damu yakaanza kumtoka mdomoni, alishindwa kuvumilia, akalala chini na kuanza kulia. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea,
Hakupata msaada wowote ule ule. Baada ya dakika kadhaa, akaanza kutapika, madonge makubwa ya damu yakaanza kutoka. Akahisi kwamba yale matunda ndiyo yaliyokuwa yakimsababishia hali hiyo na kuanza kujitahidi kuyatema.
“Mungu nisaidie,” alisema Fareed huku akiwa kwenye hali mbaya, kwa jinsi tumbo lile lilivyoanza kuuma ghafla, akahisi kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
****
Mauaji ya Bwana Belleck yaliyokuwa yametokea nchini Ufaransa yalimshtua kila mtu, watu hawakuamini kile kilichokuwa kimetokea, ni ndani ya siku tatu mabilionea wawili walikuwa wameuawa na kwa jinsi alama za mauaji zilivyokuwa zikionyesha, kila mtu akagundua kwamba muuaji alikuwa mmoja.
ITAENDELEA KESHO
Post a Comment