ad

ad

Michirizi Ya Damu - 12


Uturuki kwenda nchini Marekani. Kwa usafiri wa meli hiyo, wangetumia mwezi mmoja njiani mpaka kufika huko.
“Mwezi mmoja?” aliuliza Fareed.
“Ndiyo!” alijibu Mustapha.
“Ni kipindi kirefu mno, kweli hatuwezi kutumia hata wiki moja au chini ya hapo?” aliuliza Fareed.
“Ila ni mbali sana.”
“Ndiyo! Ila mwezi mzima nao ni mwingi mno,” alisema Fareed.
Hawakuwa na jinsi, hakukuwa na uwezekano wa kuwahi huko, ilikuwa ni lazima watumie mwezi mzima mpaka kufika nchini humo. Hawakuwa na hofu, walichojua ni kwamba walikuwa katika mikono salama na kusingekuwa na tatizo lolote lile.
Hawakutaka kujiuliza sana kuhusu mabegi madogo ambayo waliambiwa kwamba ni lazima waingie nayo nchini Marekani na kukutana na mtu ambaye aliwaambia kwamba wangekutana naye. Walimwamini Mustapha, kila mtu ambaye walikutanishwa naye, walimwamini kwa asilimia mia moja.
Safari ikaanza, ilikuwa ni ndefu na yenye kuchosha mno lakini hawakujali. Wiki ya kwanza ikakatika wakiwa majini, ya pili, ya tatu mpaka ya nne bado walikuwa njiani kuelekea nchini Marekani kwa kupitia katika Bahari ya Atlantiki.
Baada ya kupita siku ishirini na nane, wakaingia katika Visiwa vya Puerto Rico ambapo walipokelewa kinyemela na Waarabu wengine na kupelekwa katika nyumba moja kubwa na kutulia huko.
Bado waliendelea kuwaona Waarabu kuwa watu wema, hawakujua mpango mzito waliokuwa nao watu hao, hawakujua kama walikuwa wakienda kutolewa mhanga pasipo wao kujua.
Hapo Puerto Rico walikaa kwa siku mbili kisha kuondoka na kuelekea nchin Cuba ambapo hapo wakakutana na Waarabu wengine waliowaunganisha kwa baadhi ya wanajeshi na kuambiwa lengo la watu hao kufika hapo.
Kutokana na uadui mkubwa baina ya Marekani na Cuba, mipango ikaanza kusukwa upya, ilikuwa ni lazima Marekani ilipuliwe kwa mara nyingine tena na watu hao ndiyo waliowafanyia mpango Fareed na wenzake kuingia nchini Marekani kinyemela kabisa, njia walizokuwa wakitumia Wacuba hasa wauza unga na kutulia jijini New York.
“Kesho mtaelekea katika Kituo cha Pennslyvania, hapo kuna treni itakuja, kuna mtu atawaletea tiketi na nyie kuondoka, popote mtakapokwenda mtajua kivyenuvyenu, cha msingi tumekwishawaleta Marekani, sasa kutafuta maisha ni juu yenu,” alisema Mustapha huku akiwaangalia.
“Tunashukuru sana!” waliitikia huku wakiwa na furaha.
“Kesho ndiyo mtakwenda. Jiandaeni!”
“Sawa.”
****
Mustapha aliwapanga vijana wake ambao walitakiwa kuwapokea wakina Fareed ambao ndiyo wangekwenda katika kituo cha treni cha Pennslyvania kwa ajili ya kulipua kituo hicho.
Siku ambayo ndiyo ingekuwa siku ya tukio, vijana wa Mustapha ambao ndiyo wangeyaseti mabomu hayo tayari walifika katika kituo hicho kwa ajili ya kuwasubiri vijana waliokuwa na mabomu kwa ajili ya kuyalipua pasipo wao wenyewe kugundua kitu chochote kile.
Wakati hayo yote yakiendelea, Fareed alikuwa katika chumba kimoja na vijana wenzake, walikuwa wamejiandaa kwa ajili ya kwenda kulipua kituo hicho cha treni pasipo kujua kama ndani ya mabegi hayo kuliwa na mabomu.
Baada ya kupewa kiasi fulani kama kuwalaghai kwamba sasa wangekwenda huko na kuanza maisha yao, wakaelekea nje ambapo wakapanda gari na Mustapha na kwenda katika kituo hicho. Hakukuwa mbali sana, hawakutumia muda mrefu wakafika ambapo moja kwa moja wakaingia ndani.
Hakukuwa na mtu aliyejua kitu chochote kile, kila aliyekuwa akiwaangalia, alijua kwamba watu hao walikuwa abiria kama wengine. Walijichanganya na watu wengine na wao kusubiri treni ambayo ingefika mahali hapo muda si mrefu.
Bango kubwa lililokuwa mahali hapo lilikuwa likionyesha dakika zilizokuwa zimebaki kabla ya treni hiyo kufika katika kituo hicho. Watu walijikusanya, bango hilo lilionyesha kwamba ziliokuwa zimebaki dakika tano tu kabla ya treni hiyo kuchukua abiria kwenye kituo hicho na kuondoka.
Kila mmoja macho yake yalikuwa yakiangalia saa yake, kwa Fareed, alikosa amani, wenzake walikuwa wakifurahi kwamba hatimaye maisha yao yangeanza nchini Marekani lakini kwake, kila dakika zilipokuwa zikienda mbele ndivyo alivyokuwa na hofu zaidi.
“Humu ndani ya mabegi kuna nini? Kwa nini hawakuturuhusu tufungue ili tuangalie? Kama kuna kitu kizuri, hivi kweli wasingependa tujue?” alijiuliza Fareed huku akijaribu kujiuliza juu ya kile kilichokuwa ndani ya begi.
Muda huo Mustapha alikuwa pembeni yao, macho yake yalikuwa katika saa aliyokuwa ameivaa. Huku zikiwa zimebaki dakika tatu hata kabla ya treni kufika, Mwarabu mmoja akafika mahali hapo na kusimama pembeni ya Mustapha na kuanza kuzungumza naye.
Fareed alisikika lakini hakufahamu watu hao walikuwa wakizungumzia mambo gani. Mwanaume huyo aliyekuwa akizungumza na Fareed alikuwa na kifaa kama rimoti mkononi mwake, hakujua kazi ya hicho ila kwa jinsi kilivyoonekana, alijua kwamba hakikuwa kitu kizuri.
“Guys! I think this is our last time to meet each other! Have the good journey,” (jamani! Nafikiri huu ndiyo mara ya mwisho kuonana sisi nanyi! Muwe na safari njema) alisema Mustapha huku akiwaangalia wanaume hao.
“Thank you sir,” (ahsante bwana mkubwa)
Mustapha na yule mwanaume hawakutaka kusubiri mahali hapo, wakaondoka mahali hapo na kuelekea nje ya kituo hicho. Fareed na wenzake wakabaki kituoni hapo wakiwa na mabegi yale yaliyokuwa na mabomu.
Bado kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, alikuwa na maswali mfululizo juu ya kile kilichokuwa ndani ya mabegi yale. Hakutaka kuridhika, akawaaga wenzake kwamba anakwenda chooni kujisaidia na angarudi muda si mrefu.
Akaondoka harakaharaka, alipofika chooni, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuliweka chini lile begi, zipu zilifungwa kwa kufuli ndogo alichokifanya ni kulichana, ndani, akakutana na mfuko mweusi na alipoufungua, macho yake yakatua katika bomu moja kubwa lililokuwa likiwaka kitaa chekundu.
“Mungu wangu!” alisema kwa mshtuko, ghafla akasikia huko nje treni ikiwa inaingia, muda ambao bomu hilo lilitakiwa kulipuliwa.
****
Mustapha na mwenzake wakatoka nje, wakaelekea kwenye gari lao huku akiwa na furaha tele. Moyo wake aliona kwamba alifanikiwa katika kile walichokuwa wamekipanga kwamba mabomu yalifika salama nchini Marekani na muda huo yalikuwa kituoni.
Wakalifuata gari lao na kutulia humo. Mudda wote macho yao yalikuwa katika saa zao huku masikio yao yakisikiliza kwa makini kile kilichokuwa kikiendelea katika kituo kile. Kama treni ingekuwa inaingia kituoni hapo, kusingekuwa na ugumu wa kujua hilo, wangesikia mlio wake na hivyo kukaa kwa sekunde chache, litakaposimama tu waweze kulipua bomu hilo.
“Muda unakwenda tu! Subiri tusubiri,” alisema Mustapha.
Walisubiri kwa dakika tatu tu wakasikia treni likiwa linaingia, hawakutaka kuwa na presha kubwa, walisubiri mpaka waliposikia limesimama na abiria kuanza kuteremka. Mwanaume aliyekuwa na Mustapha akachukua kirimoti kile kwa lengo la kulipua mabomu yale.
“في سبيل الله,” (kwa ajili ya Mungu) alisema mwanaume yule kisha kubonyeza kitufe kile.
“Puuuuuuuu…..” ilisikika milio ya mabomu makubwa matatu yaliyopuka ndani ya kituo hicho.
****
Bilionea Belleck alikuwa na kila kitu, kila siku alikuwa akikusanya fedha nyingi kutokana na biashara mbalimbali alizokuwa akizifanya. Aliingiza kiasi kikubwa cha fedha na kila siku katika maisha yake aliendelea kuogelea kwenye dimbi kubwa la utajiri.
Alipendwa kutokana na sura nzuri aliyokuwa nayo, alipendwa kutokana na utajiri mkubwa aliokuwa nao. Kila siku kazi yake ilikuwa ni kubadilisha wanawake, alikuwa akienda kununua wanawake barabarani na kwenda kufanya nao mapenzi.
Aliyazoea maisha hayo, hakutaka kutulia nyumbani, alikuwa mtu wa safari, kusafiri kuelekea Ufaransa, Uholanzi, Italia, kila alipokuwa ilikuwa ni lazima kulala na wanawake kitu ambacho alipenda kufanya katika maisha yake.
Hakumfikiria mtu aliyeitwa Fareed, kwake, alijua kabisa mtu huyo hakuwepo katika uso wa dunia, alikumbuka jinsi alivyowatuma watu na kwenda kumtupa baharini, tena hakutupwa huku wakiwa watu hao, alitupwa huku akishuhudia kitu kilichompa uhakika kwamba mtu huyo alikuwa chakula cha samaki mpaka muda huo.
Baada ya kupata sana pesa, hatimaye yeye kama bilionea alitakiwa kukutana na mabiliona wenzake nchini Ufaransa kwa ajili ya kujadili biashara zao, huo ulikuwa mkutano mkubwa ambao kwa bilionea kama yeye ilikuwa ni lazima kushiriki na kuangalia ni kwa namna gani wangeweza kufanikiwa zaidi katika biashara zao na kuweka ubia na mabilionea wa Kiarabu kwa ajili ya kupanua soko lao.
Kikao kikafanyika nchini humo, kilikuwa kizito, kikubwa ambacho kilitangazwa na vyombo mbalimbali vya habari. Kikao hicho kilitakiwa kuchukua wiki moja kwani kulikuwa na mada nyingi, na kwenye kila mada ilikuwa ni kuwapendelea wao na si watu masikini ambao waliwafanya kuwa hapo.
Kwa sababu machangudoa walijua kwamba mabilionea walikuwa wateja wao wakubwa, wakawa wanakusanyika nje ya Hoteli ya King Napoleon II kwa ajili ya kuwanunua na kwenda kulala nao.
Kama ilivyokuwa kwa mabilionea wengi, kila siku ilikuwa ni lazima kwa Bilionea Belleck kuchukua changudoa na kuondoka naye kulala naye usiku mzima. Alikuwa na pesa, alikuwa na kila kitu alichokuwa akikihitaji katika maisha yake, hakuona kama kulikuwa na ugumu wa kulala na mwanamke yeyote aliyekuwa akimuhitaji katika kipindi hicho.
“Unaitwa nani?” aliuliza mara baada ya kumfuata msichana mmoja kisri.
“Natalie!”
“Ooh! Gharama zako zipo vipi?”
“Euro elfu moja!”
“Sawa!”
Hakuwa na mazungumzo marefu, alijiamini, hakuona kama kulikuwa na changudoa ambaye angemtajia gharama ya pesa ambazo hakuwa nazo. Akamchukua msichana huyo na kuondoka zake.
Hakutaka kuwa na wapambe, alitaka kufanya kila kitu peke yake, aliamini kwamba kama angekuwa na wapambe mambo yangevuja na hatimaye kujulikana kama alikuwa akinunua machangudoa kitu ambacho hakutaka kabisa kijulikane kwa kuogopa kumuumiza mkewe.
Machangudoa wengi walipenda kununuliwa na mzee huyo kwa sababu alikuwa na uhuru wa kukwambia wewe mwenyewe upange bei. Walipokuwa wakiliona gari lake, walilikimbilia na kujipanga mstari na hivyo kuchagua ni yupi alitakiwa kulala naye usiku wa siku hiyo.
Baada ya wiki moja kumalizika na mkutano huo kuisha, hakutaka kuondoka nchini Ufaransa, alitaka kuendelea kubaki mahali hapo kwani kulimteka, wanawake wazuri waliokuwa katika Jiji la Paris walimdatisha kichwa chake na hivyo kutamani kuendelea kukaa zaidi.
****
Kila kitu alichokuwa akikifanya ndani ya choo kile, Fareed alikifanya harakaharaka, hakutaka kuchelewa kwani kwa jinsi bomu lile lilivyoonekana, halikuwa limebakiza dakika nyingi kulipuka.
Akaliacha begi palepale chini na kisha kukimbia kutoka chooni hapo, hakutaka kubaki ndani ya kituo hicho kwani aliamini kwamba endapo angebaki basi naye pia angeweza kufa.
Kila mtu alibaki akimshangaa, wengine walihisi kwamba alikuwa mwizi, kwamba aliiba na hivyo kukimbia. Sehemu ambayo ilikuwa ikijifungua kwa kichuma kwenda juu baada ya kuweka tiketi, hakutaka hata ijifungue, akaruka kwa juu na kuelekea nje.
Wakati anafika nje ya kituo hicho kwa kupitia mlango mwingine, mabomu yakasikika yakilipuka na nguvu yake ilikuwa kubwa kiasi kwamba mpaka wao waliokuwa nje ya kituo kile wakarushwa akiwepo yeye mwenyewe.
Akaangukia katika gari moja lililokuwa limepaki pembeni, watu wengine waliokuwa hapo walikuwa hoi, wengine walikuwa wakiteketa kwa moto, pale alipoangukia ambapo kulikuwa ni kama hatua kumi kutoka pale alipokuwa amefikia, Fareed alikuwa hoi, kichwa chake kilikuwa kikitoka damu, alisikia maumivu makubwa mwilini mwake.
Akajitahidi kusimama, akashindwa, akabaki hapohapo akiwa amelala huku macho yake yakiwa mazito kabisa. Akajitahidi kuuinua mkono wake, akashindwa, kila kitu alichotaka kukifanya mahali hapo alishindwa kabisa.
Kwa kutumia uangaliaji wake wa kwa mbali, akawaona watu wakikimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada, baada ya sekunde ishirini tu akiwa hapo, giza kubwa likayafumba macho yake na baada ya sekunde hizo, akapoteza fahamu na hakujua kitu gani kiliendelea.
****
Lilikuwa tukio kubwa lililoishtua dunia, hakukuwa na mtu aliyeamini kama kweli Marekani ingeweza kulipuliwa kama ilivyotokea. Kila mtu alishangaa kwani kwa jinsi nchi hiyo ilivyokuwa imejiwekea ulinzi tangu kulipuliwa kwa maghorofa ya biashara ya WTC, hakukuwa na aliyeamini kwamba kweli magaidi wangeweza kuilipua nchi hiyo kwa mara nyingine.
Watu zaidi ya elfu moja mia tano wakasadikiwa kufa katika tuki hilo huku maelfu wakijeruhiwa vibaya. Ndani ya dakika chache tangu tukio hilo litokee, magari ya zimamoto yakafika mahali hapo yakiongozana na magari kadhaa ya wagonjwa.
Polisi wakaweka kamba ya nyano iliyoandikwa ‘Do not cross’ yaani Usivuke huku ni polisi tu na watu wa afya ndiyo walioruhusiwa kwenda ndani ya kituo kile kulipotapakaa miili mingi ya watu.
Mambo yote hayo yalikuwa yakiendelea huku Fareed akiwa chini, hakujitambua, pale alipokuwa, kwa jinsi alivyokuwa amerushwa, ilikuwa vigumu kuamini kama mtu huyo alikuwa mzima.
Yeye na majeruhi wengine wakachukuliwa na kukimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu huku nyuma waandishi wa habri wakiendelea kukusanyika katika eneo hilo la tukio kwa ajili ya kuripoti kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Gari halikuchukua muda mrefu likafika katika Hospitali ya St. Joseph Medical Centre iliyokuwa hapohapo Pennsylvania ambapo mara baada ya magari kuingizwa ndani, machela zikaletwa, majeruhi wakapandishwa kwenye machela hizo kisha kupelekwa ndani.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kwa Fareed kukaa ndani ya hospitali hiyo. Matibabu yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Baada ya saa kumi na mbili, akarudiwa na fahamu, akayafumbua macho yake na kuanza kuangalia huku na kule.
Mahali pale palikuwa ni hospitali, hakujua alikuwa amefikaje, aliangalia huku na kule, kwa juu, dripu ilikuwa ikining’inia huku mwili wake ukiwa na maumivu makali kiasi kwamba alishindwa hata kugeuka.
Mbali na yeye, ndani ya wodi ile kulikuwa na wagonjwa wengine ambao hawakuonekana kuwa na nafuu kama alivyokuwa. Huo haukuwa mwisho wa safari yake, ilikuwa ni lazima aondoke mahali hapo, alitaka kwenda sehemu kwa ajili ya kukaa kisha kumtafuta Bilionea Belleck ambaye aliamini kwamba bado alikuwa hapohapo Marekani.
“Ni lazima niondoke hapa,” alisema Fareed.
Kuondoka mahali hapo haikuwa kazi nyepesi, mara kwa mara madaktari na manesi walikuwa wakifika kwa ajili ya kuangalia maendeleo yao. Hakutaka kabisa kuendelea kubaki kwani bado maisha yake aliyaona kuwa na hatari kubwa.
Kwa kuwa kulikuwa na ugumu wa kufanya hivyo, kitu chepesi alichokifanya ni kusubiri mpaka usiku ambapo akaomba nafasi ya kwenda chooni kwa lengo la kufika huko na kukimbia zake.
Akasimama na kutembea kwa mwendo wa taratibu, mwendo ulioonyesha kwamba hakuwa mzima kiafya, alipofika chooni, akajisaidia haja ndogo na kuangalia ni kwa namna gani angeweza kutoroka hospitali hapo pasipo kuonekana.
**
Bado watu waliendelea kushangaa juu ya tukio la kigaidi lililokuwa limetokea nchini Marekani. Shirika la kipelelezi la FBI lilikuwa kwenye wakati mgumu, hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kuwapata wahusika wakuu wa tukio hilo ingawa Al Qaida walijitokeza hadharani na kusema kwamba wao walihusika kwa kila kitu.
Walichokuwa wakikihitaji FBI ni picha zilizokuwa zimepigwa dakika kadhaa kabla ya tukio kutokea. Ilikuwa ni lazima waangalie kwenye kamera za CCTV kuona kila kitu kilichokuwa kimetokea humo.
Wakaelekea katika chumba kilichokuwa na kompyuta nyingi, zilikuwa zimeunguzwa vibaya lakini walichoshukuru Mungu ni kwamba memory cards zote ambazo zilikuwa zimechukua picha kutoka ndani ya kituo hicho kabla ya tukio la kmlipuko kutokea, zilikuwa salama kabisa.
Wakazichukua na kuelekea katika kompyuta zao na kuangalia kuona kama wangeweza kuwaona wahusika wa mlipuko ule. Walifanikiwa kumuona Fareed na wenzake, waliwahisi kwamba hawakuwa na nia nzuri kutokana na mabegi ya kufanana waliyokuwa nayo. Baada ya dakika kadhaa, wakamuona Fareed akiondoka.
“Let’s roll with him,” (twende naye huyo) alisema Frankline, mmoja wa FBI waliokuwa wakifuatilia tukio hilo.
Kwa kutumia kamera mbalimbali waliweza kumfuatilia Fareed aliyekuwa akikimbia, alipofika chooni, akaingia na kisha kutoka na kuendelea kukimbia. Wakahisi kwamba huyo ndiye aliyekuwa amehusika na mlipuko ule, wakaendelea kumfuatilia mpaka nje, kituo kikalipuka, na yeye mwenyewe akarushwa na kujipigiza katika gari moja.
“Take his picture,” (chukua picha yake) alisema Frankline na mwenzake kufanya hivyo, walivyoikuza, wakamgundua, picha ikaprintiwa na mpaka gari la wagonjwa lilipomchukua na kuondoka naye, walikuwa wakifuatilia kila kitu.
“Which hospital?” (hospitali gani?)
“St. Joseph!”
“Let’s go…let’s go,” (twendeni…twendeni) alisema Franckiline, maofisa wanne wa FBI waliokuwa na bunduki wakaanza kwenda kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kumkamata Fareed ambaye walikuwa na uhakika kwamba alihusika kwa asilimia mia moja katika mlipuko huo.
Wakawapa wenzao taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea, hawakuishia kuwataarifu bali wakawatumia na picha za mwanaume huyo na kwamba walikuwa njiani kwenda kumkamata.
Kwa kuwa mahali hapo hakukuwa mbali na hospitali, ndani ya dakika kumi wakafika na moja kwa moja kuingia ndani. Kulikuwa na idadi kubwa ya watu, wengi waliokuwa mahali hapo walifika kwa ajili ya kuwaona ndegu zao waliokuwa hoi.
Wakazungumza na madaktari na kumuonyeshea picha ya Fareed, kwa kuwa daktari huyo alikuwa akiwakumbuka watu aliokuwa amewapokea, hakukuwa na ugumu kugundua kwamba picha ya mtu aliyekuwa ameonyeshewa alikufikishwa ndani ya hospitali hiyo saa moja iliyopita.
“Where is him?” (yupo wapi?)
ITAENDELEA KESHO

No comments

Powered by Blogger.