ad

ad

Michirizi Ya Damu - 08

Huo ndiyo ulikuwa uamuzi wake, hakutaka siku hiyo ipite pasipo kuwasiliana naye, alichokifanya usiku huo ni kuamka usiku wa manane, akatoka kitandani huku akinyata na kuelekea chooni kwa lengo la kuzungumza na mwanaume huyo kwani pasipo kufanya hivyo asingefanikiwa kutokana na Kaith kumng’ang’ania kama ruba.
“Naomba upokee simu,” alisema wakati simu ikianza kuita, baada ya sekundee kadhaa tu, simu ikapokelewa.
“Bila shaka ni mrembo wa mgahawani,” alisema mwanaume huyo baada ya kupokea simu, alionekana kabisa kuwa macho japokuwa usiku ulikuwa umekwenda sana.
“Ndiyo! U mzima bebi,” alisema Maria, hakutaka kujivunga, alikuwa tayari mwanaume huyo ajue kwamba alikuwa akimpenda.
“Nipo poa.”
“Upo wapi nije tuzungumze kama ulivyotaka?” aliuliza Maria.
“Nipo hotelini! Ila nipo na mke wangu!”
“Jamani! Kumbe umeoa?”
“Yeah! Lakini nahisi hili haliwezi kuninyima kuwa na wewe,” alisema mwanaume huyo.
“Kweli kabisa. Umetokea kunichanganya sana mpenzi. Naomba nionane na wewe hata kesho!” alisema Maria.
“Haina shida. Wewe tu! Bye!”
“Bye! Nakupenda.”
“Nakupenda pia!”
****
Fareed aliumia moyoni mwake, hakujua sababu iliyomfanya Mungu kumpitisha katika maisha aliyokuwa akipitia kipindi hicho. Alidhamiria kubadilisha maisha yake, alidhamiria kumuabudu Mungu katika roho na kweli lakini pale alipokubaliana na moyo wake kwamba alitakiwa kubadilika, tayari tatizo likawa limetokea.
Alilia, alihuzunika, moyo wake ulichoma mno. Alimwamini Padri Luke kwa kuona kwamba angemuombea msamaha kwa Mungu ili maisha yake mapya yaanze rasmi lakini kitu cha ajabu kabisa, mwanaume huyo akaamua kumbaka.
Hakutaka kuendelea kubaki pale alipotupwa, akaondoka na kurudi hotelini, huko akakaa na kulia sana, akahuzunika mno na mwisho wa siku kupanga kurudi nchini Tanzania, alitaka kuanza upya kabisa, kama mtu aliyezaliwa kwa mara ya pili.
Alirudi nchini kimya kimya, hakutaka kumtaarifu Asteria kama alikuwa amerudi, alifanya hivyo kwa sababu alitaka kuyabadilisha maisha yake, aiondoe tamaa iliyokuwa mwilini mwake, asimtamani tena mwanaume ashinde vishawishi vyote na kuwa mtu mpya.
Akamtafuta daktari aliyekuwa akiwahudumia sana wanaume tata, huyo aliitwa Emmanuel Kihampa, daktari maarufu aliyekuwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Alipofika huko, akamfuata katika ofisi yake na kuanza kuzungumza naye.
Hakutakiwa kumficha kitu chochote kile, alitakiwa kumwambia kila kitu kilichokuwa kikiendelea mwilini mwake, alimwambia tabia yake hiyo ambayo ilianza tangu utotoni, alimwambia juu ya tamaa kali aliyokuwa nayo.
Daktari huyo akampa vidonge vya kumeza lakini pia alitakiwa kuchomwa sindano nyumba kwa ajili ya kuua vijidudu ambavyo vilikuwa vikimuingiza katika matamanio makubwa. Hilo halikuwa tatizo, alidhamiria kubadilika, alidhamiria kuyabadilisha maisha yake, hivyo akachomwa sindano hiyo.
Haikutosha, akaambiwa kwamba ilikuwa ni lazima auweke mwili wake kimazoezi, alitakiwa kufanya mazoezi ya kila aina kuhakikisha anakuwa sawa. Akaanza kukimbia mitaani, akawa anajiunga na vijana wengine kufanya mazoezi huku ikifika usiku, alitumia muda wake mwingi kusoma vitabu, yote hiyo ilikuwa ni harakati za kuachana na tabia chafu alizokuwa nazo kwamba asingeweza kufikiria ngono kama kipindi cha nyuma.
Ilikuwa kazi kubwa, alipambana nayo, ilimtesa, ilimnyima raha kwani wakati mwingine alikuwa akishtuka kutoka usingizini, mwili ulikuwa ukimsumbua na kutandani, alikuwa na matamanio makubwa ya kuwa na mwanaume kipindi hicho, alivyokuwa akiiona hali hiyo, haraka sana alichukua mazoezi humohumo, kuruka kamba na kupiga pushapu kisa kulala.
Hayo yalikuwa ni maisha yake, hakuacha kwenda hospitalini, kila alipokwenda, alichomwa sindano nyumba kwa ajili ya kuua vijidudu vilivyokuwa vikimpa hamu ya kufanya mapenzi na mwanaume, ilimsaidia japokuwa ilionekana kuwa vigumu kumalizana na matatizo aliyokuwa nayo.
Kila siku alikuwa akienda katika sehemu ya mazoezi, gym kwa ajili ya kuchukua mazoezi mbalimbali hata kunyanyua vyuma. Alikuwa na muonekano wa kike, alikuwa na sauti iliyofanana na mwanamke lakini baada ya kuanza kufanya mazoezi, kunyanyua sana vyuma hatimaye mwili wake ukaanza kubadilika.
Akaanza kujazia, kifua chake kikaanza kuwa kipana, muonekano wa kike ukapotea, akaanza kuwa na six packs tumboni, mabadiliko hayo yote yalitokea ndani ya miezi sita, akaonekana kuwa mwanaume kamili, aliyeendelea kupata tiba kila siku na kufanya mazoezi ya nguvu.
Hakuwasahau watu waliomtenda, aliwachukia mno na hakutaka kabisa kuona watu hao wakiendelea kuishi. Alimkumbuka Keith, mwanaume mwenye roho mbaya ambaye alidhamiria kumuua baharini lakini kwa bahati nzuri sana akanusurika baada ya kuokolewa na mvuvi mmoja.
Hakuishia hapo, alimkumbuka bilionea Belleck ambaye alijifanya kumpenda, alimtumia alivyotaka na mwisho wa siku kutaka kumuua kwa kumtoa madawa ya kulevya yaliyokuwa tumboni, tena pasipo kujali kama alimsaidia kusafirisha madawa hayo au la.
Na mtu wa mwisho kabisa aliyemkumbuka alikuwa Padri Luke Mathew ambaye alimfuata kwa ajili ya kutubu dhambi zake lakini mwisho wa siku mwanaume huyo akambaka. Alikumbuka kila kitu, hakutaka kuona watu hao wakiendelea kuishi kwa raha na wakati walishirikiana kumuumiza moyoni mwake, walishirikiana hata kuuumiza moyo wake.
Mtu wa kwanza kabisa aliyetaka kumuua alikuwa Bilionea Keith. Hakutaka kumuona mwanaume huyo akiendelea kuvuta pumzi ya dunia hii na wakati alimtenda vibaya. Mara ya mwisho kumsikia mwanaume huyo ni kwamba alikuwa na msichana mrembo mwenye asili ya Kinaigeria aliyeitwa Maria.
Alitaka kujua mahali alipokuwa, hakuendelea kuishi nchini Tanzania, akasafiri mpaka nchini Marekani, kwa kuwa bilionea huyo alikuwa akifahamika sana, hakupata kazi kuzipata data zake tena kutoka kwa watu walioonekana kuwa wa karibu sana.
Akaambiwa kwamba mwanaume huyo alikuwa akijiandaa na safari ya kuelekea nchini Italia kwa ajili ya kula bata na mpenzi wake na kuliona jengo kubwa la Collosseum. HAkutaka kubaki nchini Marekani, ilikuwa ni lazima kwenda huko.
Alijiamini kwamba alikuwa na sura nzuri, mwili uliojengeka, alijua fika kwamba mara baada ya Maria kumuona ilikuwa ni lazima kumtamani na kutaka kulala naye. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa, alivyoonana na msichana huyo hotelini, akampenda na kuchukua namba yake ya simu.
Wakaanza kuwasiliana, alimdanganya kwamba alikuwa na mkewe hotelini, hakutaka kuona msichana huyo akipata muda wa kuwa naye kwa kujiachia, alitaka kumuingizia hofu ajue kwamba kweli mwanaume huyo alikuwa na mkewe hapo hotelini.
Mazungumzo yao yalikuwa ya kwenye simu, walitumiana meseji za mapenzi, kwa kipindi kifupi tu tayari Maria alionekana kufa na kuoza, hakutaka kuona mwanaume Fareed akiendelea kuwa na mkewe, alijipanga na alijipiza kwamba ni lazima alale naye kwa gharama yoyote ile.
“Siwezi kumuacha mwanaume mwenye mwili mzuri kama yule, nitamuachaje mwanaume mwenye sura nzuri kama yule?” alijiuliza.
Hakutaka kuona hilo likitokea, alijipiza kwamba ni lazima amfuate kitandani, alale naye na kufanya naye mapenzi. Ni kama Keith alijua, ukaribu kwa Maria ukaongezeka zaidi au kwa Kiswahili chepesi cha mtaani ni kwamba alikuwa akikaba mpaka penalti.
“Bebi naomba nionane na wewe,” aliandika ujumbe mfupi.
“Leo!”
“Ndiyo! Kesho tunaondoka!”
“Kwenda wapi?”
“Misri!”
“Kuna nini?”
Tunakwenda kuangalia mapiramidi ya Giza!”
“Ooh! Nitakuweepo huko, nitakuja peke yangu kuonana nawe,” aliandika Fareed.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Niahidi kama tutakuwa wote!”
“Nakuahidi!”
Moyo wa Maria ukaridhika, hakuamini kama hatimaye mwanaume huyo alikubaliana naye kwamba wangeonana na kufanya mambo yao. Moyo wake ukawa na furaha tele, akajitupa kitandani huku akiiona dunia yote kuwa yake kwani kile alichotaka kukisikia ndicho alichoambiwa na mwanaume huyo.
“Nitalala naye na kumuonyeshea kwa nini yule babu amepagawa kwa penzi langu,” alisema Maria na kujilaza kitandani huku akiisubiri kesho ifike, waondoke kuelekea Misri ambapo huko angeonana na mwanaume huyo.
****
Keith hakutaka kukaa sana na mpenzi wake nchini Italia, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea katika Mji wa Giza, nchini Misri kwa ajili ya kuyatazama mapiramidi yaliyokuwa nchini humo.
Njiani, bado walionyesheana mapenzi ya dhati, walikuwa wakibusiana sana lakini mawazo ya Maria hayakuwa hapo, alimfanyia mwanaume huyo kila kitu lakini moyo wake, kichwa chake, vyote vilikuwa vikimfikiria Fareed, mwanaume ambaye hakujua kama alikuwa akitoka kimapenzi na mpenzi wake.
Ndege haikuchukua muda mrefu ikafika nchini Misri ndani ya Jiji la Cairo ambapo hapo wakachukua basi lililowapeleka mpaka katika Mji wa El Giza. Macho ya Maria yalishangaa, hakuamini kile alichokuwa kikiona, aliyaona mapiramidi makubwa ambayo alikuwa akiyasoma kwenye vitabu na wakati mwingine kuyaangalia kwenye televisheni.
Alishangaa mno, wakati mwingine alitamani kulia kwani furaha aliyokuwa nayo kipindi hicho ilikuwa kubwa sana. Akamkumbatia mpenzi wake, Keith na kumshukuru sana kwa kumsafisha macho kwa kumpeleka nchini Misri.
“Tutakwenda kule kesho, leo tulale hotelini,” alisema Keith, wakati huo waliyaona mapiramidi yale yakiwa mbali kabisa.
Walipoingia hotelini, kama kawaida wakaanza kucheza michezo ya kimahaba kitandani, kila mmoja alimtamani mwenzake, kila mmoja alihitaji sana kuwa na mwenzake wakati huo.
Japokuwa Maria alijitoa sana kama ilivyo kawaida yake lakini kichwa chake hakikuacha kumfikiria Fareed, kwake, mwanaume huyo alikuwa kila kitu, alikichanganya kichwa chake, muda mwingi alikuwa na mawazo tele juu yake.
Walipomaliza kucheza, wakatoka kitandani na kuelekea bafuni kuoga na walipomaliza, wakaenda kula chakula. Muda mwingi Maria alikuwa akiangalia huku na kule, macho yake hayakutulia, alikuwa akimtafuta mwanaume wake, alitaka kujua kama alifika mahali hapo au la.
Hakuacha kuangalia na simu yake pia, aliingia WhatsApp kwa kuhisi labda mwanaume huyo angekuwa amemtumia ujumbe mfupi lakini napo hakuona kitu jambo lililomshangaza mno.
“Amekuja kweli au alinidanganya kuniridhisha?” alijiuliza huku akionekana kushtuka. Wakati akiwa bize na simu yake huku akijiuliza maswali mengi, Keith akagundua kwamba mpenzi wake huyo hakuwa sawa.
“Kuna nini?” aliuliza Keith swali lililomfanya Maria kushtuka.
“Eeh!”
“Kuna nini?”
“Nina mawazo sana, nimekuwa nikiwafikiria sana wazazi wangu!” alijibu Maria, alikuwa akimdanganya.
“Pole sana! Ila tutakwenda. Nakuahidi kwamba tukitoka hapa, tunaelekea Nigeria,” alisema Keith.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
Kidogo Maria akajifanya kuwa na furaha lakini ukweli ni kwamba bado moyo wake ulikuwa na mawazo tele kwani mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa penzi la dhati kutoka moyoni mwake hakuwa amewasiliana naye kwenye simu japokuwa alimuahidi kufanya hivyo.
Akainuka na kurudi chumbani. Huko, hakutulia, alijilaza kitandani lakini kichwa chake kilikuwa mbali kabisa. Keith alipoingia na kumuona msichana huyo kajilaza, akajua kwamba alikuwa na uchovu wa safari hivyo kumuacha na kuondoka kwenda baa kunywa pombe.
Kule ndani, Maria akachukua simu yake na kuanza kumtafuta mwanaume huyo kwa kumtumia meseji mbalimbali kwenye Mtandao wa WhatsApp, japokuwa hakuwa hewani lakini aliamini kwamba mara atakapofungua akaunti yake basi angekutana na ujumbe aliokuwa amemtumia.
Wala hazikupita hata dakika thelathini, akapokea ujumbe kutoka kwa Fareed ambaye alimwambia kwamba na yeye mwenyewe alifika na kuchukua chumba ndani ya hoteli hiyo.
“Unasemaje?”
“Nipo chumba namba ishirini!”
“NAkuja!”
“Eeh! Nipo na mke wangu mpenzi! Subiri, leo usiku nitakushtua. Mnakwenda muda gani kwenye piramidi?” aliuliza Fareed.
“Kesho asubuhi!”
“Basi na mimi nitakuwepo huko mpenzi!” alisema Fareed.
Moyo wa Maria ukafarijika, akajisikia furaha moyoni mwake, hakuamini kama mwisho wa siku mwanaume huyo angemtumia ujumbe na kumwambia kwamba tayari alifika nchini Misri. Akasimama na kuanza kuzungukazunguka ndani ya chumba kile, kwa jinsi alivyojisikia moyoni mwake, alikuwa radhi kufanya jambo lolote lile mahali hapo.
Siku hiyo alilala kwa amani kabisa tena akiwa amekumbatiana na mpenzi wake, Keith. Ilipofika asubuhi, wakaamka na kuelekea bafuni ambapo baada ya kumaliza, wakaondoka na kuchukua gari ndogo na kwenda kulipokuwa na mapiramidi yake.
“Huku utafurahia kwa roho yako! Ni pazuri na kunasisimua sana,” alisema Keith.
“Leo nitajione mwenyewe mpenzi!” alisema Maria.
Wakati wao wakielekea huko, huku nyuma Fareed alikuwa akitoka chumbani kwake. Siku hiyo alidhamiria kufanya mauaji, alikumbuka vema Keith alichokuwa amemfanyia, moyo wake ulikuwa na hasira naye na hakutaka kumwacha hata kidogo.
Alikuwa radhi kumuua kwa sababu tu aliyaumiza maisha yake, alikuwa tayari kumuua kwani hapo kabla mwanaume huyo alitaka kumuua, pasipo kuokolewa na mvuvi, angekuwa tayari marehemu.
Akaingia ndani ya gari na kuanza kwenda kwenye mapiramidi yale. Hawakuchukua muda mrefu wakafika ambapo akateremka na kuanza kuelekea kule kulipokuwa na piramidi kubwa.
Kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wamefika mahali hapo. Wengi walisafiri kutoka nchini mwao na kufika Misri kwa ajili ya kuangalia jinsi mapiramidi hayo makubwa yalivyokuwa yametengenezwa.
Fareed alisimama mbali kabisa, aliwaona wakiwa wamesimama karibu na geti huku wakisubiri kufunguliwa kwa geti na kuingia ndani. Ilipofika saa mbili kamili, muda wa kufungua mageti, likafunguliwa na watu kujiandikisha na kuanza kuingia ambapo kwa hatua za haraka sana, naye Fareed akaanza kwenda kule, alipofika, akalipia na yeye kuingia.
“Huu ndiyo mwisho wake,” alijisemea.
Alivalia kofia kubwa, ilikuwa vigumu sana kumgundua, ndani ya piramidi lile, walikuwa wakitembea huku na kule, hakukuwa na mtu aliyekuwa akimfuatilia mwenzake, kila mmoja alionekana kuwa bize na mambo yake.
“Today is the day!” (leo ndiyo siku yenyewe) alisema Fareed huku akigusa kisu chake kuona kama kilikuwepo kiunoni.
****
Ndani ya piramidi kulikuwa na mwanga hafifu, watu waliokuwa ndani ya piramidi hilo walikuwa wakiongozwa na watu maalum waliokuwa na kazi ya kuwatembeza watu huku na kule.
Macho ya Maria hayakutulia, muda wote alikuwa akiangalia huku na kule, alitaka kumuona mwanaume aliyeuteka moyo wake, alimwambia kwamba angekuwa mahali hapo pamoja naye lakini mpaka muda huo hakumuona na hakugundua kwamba alikuwa katika kundi la watu waliokuwa wameingia na kundi hilo.
Fareed hakutaka kuonekana, macho yake yalikuwa chini, hakutaka kukutanisha macho yake na msichana Maria. Waliendelea kusonga mbele, hakuwa akimsikiliza muongozaji aliyekuwa akiwaambia kuhusu kila kitu kilichokuwa mule ndani.
Alichokifanya Fareed ni kuchukua simu yake na kumtumia ujumbe mfupi Maria kwamba watakapofika sehemu kubwa, basi aachane na Keith na kumfuata yeye.
“Sawa. Utaniambia utakapokuwa,” alisema Maria, kidogo moyo wake ukapoa, alikuwa na hofu kubwa na alipowaangalia vizri watu wale waliokuwa katika kundi lile, akamuona mwanaume huyo japokuwa kulikuwa na mwanga hafifu.
Walikwenda mpaka walipofika sehemu kubwa, ilionekana kuwa kama uwanja fulani, sehemu ambayo Wamisri kwa zamani walitumia kama sehemu za wafalme kufanya vikao na viongozi wengine, kwa pembeni, kulikuwa na vyumba vingi ambavyo vingine vilitumika kama vyumba vya kulalia lakini vingine vilitumika kama makaburi.
“You can go to other rooms to have a look,” (mnaweza kwenda kwenye vyumba vingine kuangalia) alisema msimamizi.
Keith hakutaka kumuachia Maria, alimshikilia msichana huyo na kuanza kwenda kwenye chumba kimoja. Kwenye chumba walichokuwa wakienda, walikuwa wawili tu.
“Baby! Just wait,” (mpenzi! Subiri kwanza!) alisema Maria.
“What’s wrong?” (kuna tatizo gani?)
“I have seen my aunt?” (nimemuona shangazi yangu)
“Where is she?” (yupo wapi?)
“In that room,” (ndani ya chumba kile) alisema Maria huku akijifanya kuwa na hofu.
Alimdanganya mwanaume huyo, aliyemuona hakuwa shangazi yake bali mwanaume ambaye alitamani sana kulala naye. Akataka kuondoka hapo kumfuata Fareed, Keith alipong’ang’ania akamwambia kwamba huo si muda mzuri wa kumuona shangazi yake kwani hakuwa akijulikana nyumbani na haikuwa mila za kiafrika.
Keith hakuwa na jinsi, kwa kuwa alimpenda sana msichana huyo, akamuacha aendele kwa huyo shangazi yake na yeye angemsubiri ndani ya chumba hicho.
Wakati hayo yote yakiendelea, Fareed alikuwa akiangalia kupitia mlangoni huku akiwa ametokeza jicho tu. Alipomuona Maria akianza kuja kule alipokuwa, kwa haraka sana akapitia mlango mwingine, wakati msichana yule akiingia ndani ya chumba kile, na yeye alikuwa akitoka kutoka katika mlango mwingine.
Alitakiwa kuwa na haraka sana, hakutakiwa kupoteza muda hata mara moja. Akatembea kwa mwendo wa haraka mpaka katika chumba alichokuwemo Keith, akaingia ndani.
“Who are you?” (wewe nani?) aliuliza Keith kwani kwa jinsi Fareed alivyoingia ndani ya chumba kile, alionekana kama mtu mwenye haraka nyingi.
“Nobody!” (si mtu yeyote) alijibu Fareed,
ITAENDELEA KESHO

No comments

Powered by Blogger.