ad

ad

Mpe Uhuru, Kama Hawezi Kujichunga Mwenyewe Basi Hakufa



MAPENZI yana changamoto nyingi sana! Wahenga wana msemo wao kwamba mapenzi ni kama bahari, unaweza kuwa unazuia watu wasiogelee Coco Beach lakini wengine wakawa wanaogelea Kunduchi Beach! Ipo misemo mingi lakini yote inamaanisha kitu kimoja, usipoteze muda wako kumchunga mpenzi wako kwa sababu yawezekana wewe unahisi kwamba jirani yako ndiyo mbaya wako, unatumia nguvu nyingi kumzuia mpenzi wako asiwe na mazoea naye lakini kumbe akitoka, huko mitaani wapo wajanja wanaofaidi mali zako. Nimeamua kuja na mada hii, baada ya kukutana na visa kadhaa, vya watu wanaojikuta wakiingia kwenye matatizo makubwa, kisa kikiwa ni kuwachunga wapenzi wao wasiwasaliti. 

Tukubaliane kwamba maisha yamekuwa magumu sana kwa sasa, changamoto za kupata pesa na mahitaji mengine ya kila siku zinazidi kuongezeka, sasa iweje wewe badala ya kupambana na maisha, utumie nguvu na akili zako kumchunga mwenzi wako asikusaliti? Jinsi ilivyo, binadamu ni kiumbe ambaye ni mgumu sana kumdhibiti pale anapoamua kufanya jambo fulani. 

Yaani kama mtu ana hulka ya usaliti, hata umuwekee mageti ya umeme, umtimizie kila kitu ndani na asipate hata muda wa kutoka nje, akiamua kukusaliti atakusaliti tu, pengine na hata watu wako wa karibu. Kwa hiyo jambo la msingi siyo kumchunga mwenzi wako kama unavyochunga ng’ombe au mbuzi, mpe uhuru! Haina maana yoyote kupekuapekua simu yake, kumfuatilia nyumanyuma anapotoka au kuweka ‘walinzi’ wa kuwa wanakuletea habari za kila anachokifanya. Mwache aishi maisha yake ya kawaida na kama ni msaliti, utamgundua haraka sana kwa sababu tabia ya mtu ni kama rangi ya ngozi, haijifichi. Unapoingia kwenye kazi ya kumfuatilia, unaweza kugundua mambo mengine yanayoweza kukuumiza sana moyo wako na kukuachia makovu yasiyofutika.

 Unaweza pia kujikuta ukigombana na kila mtu kwa sababu yake, wengine wanafikia hadi hatua ya kupigana, kujeruhiana na kusababishiana matatizo makubwa eti kisa amehisi anamuibia mali zake. Maisha ya kimapenzi hayapaswi kuwa hivyo na mtu wa namna hii, unayetumia nguvu zako nyingi kumchunga ili asikusaliti, pengine siyo chaguo sahihi. Jambo ambalo watu wengi hawalijui, hakuna hisia zinazoumiza moyo kama kushindwa kumuamini mwenzi wako na kutumia muda mwingi kumchunga.

 Mwache huru na kama kuna jambo lolote baya anakufanyia, utaligundua tu. Huna sababu ya kugombana na watu, kuwekeana visasi na majirani kwa sababu yake, kwa sababu mwisho wa siku mbaya siyo mtu anayemfuata mwenzi wako, bali yeye anayeamua kumkubalia wakati akijua wazi kwamba unampenda na yeye ndiyo kila kitu kwako.

 Kama na wewe ulikuwa miongoni mwa watu wanaowachunga sana wenzi wao, nakusihi kuanzia leo badilika, nasisitiza tena kama kuna jambo lolote baya analokufanyia, utagundua tu na hapo ndipo utakapokuwa na uamuzi wa nini cha kufanya, kama uendelee naye na tabia yake hiyo mbovu au utafute mtu atakayekuwa anajiheshimu na kuheshimu hisia zako. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

No comments

Powered by Blogger.