Mambo 10 Anayotakiwa Kuwa Nayo Mwanaume Katika Umri Wa Miaka 30
Na Jumia Travel Tanzania
Watanzania
wana misemo mingi inayoendana na umri lengo likiwa ni kukumbushana
katika kuwajibika na kujipanga katika maisha ya kawaida. Miongoni mwa
misemo hiyo ni, ‘Ujana maji ya moto, fainali uzeeni.’ Msemo huu una
maana kubwa kama ukiutafakari kwa makini, lakini kwa tafsiri ya haraka
ni kwamba ujana ndio kipindi ambacho mtu huwa na nguvu za kutosha
kufanya masuala tofauti yatakayomuwezesha kuishi vema uzeeni. Licha ya
kuwa na nguvu hizo lakini huwa na changamoto kadhaa zinazomuandama
ambapo kama asipokuwa makini atakuja kujuta akiwa uzeeni.
Mojawapo
ya changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi ni kutokujua vitu gani
vya kuweka kipaumbele katika wakati waliopo. Kulingana na umri waliokuwa
nao huona kwamba muda unawatosha na hivyo kufanya masuala yasiyo na
tija wala kujijengea misingi mizuri ya kuwasaidia katika maisha yao ya
baadaye. Kwa kuliona hilo, Jumia Travel imeona ni vema kukushirikisha
wewe kama kijana wa kiume ni mambo gani ya msingi unatakiwa kuwa nayo
ukiwa katika umri wa miaka 30.
Kupevuka
kiakili. Ingawa suala la kupevuka kwa akili halihusiani na umri lakini
kufikia umri wa miaka 30 kama mwanaume unatakiwa kuonyesha ukomavu wa
akili wa hali ya juu. Hili huweza kupimwa kutokana na misimamo uliyonayo
na uwezo wa kufanya maamuzi juu ya masuala mbalimbali yanayoathiri
maisha yako. Maisha hutofautiana kwani kuna wengine hupevuka kiakili
wakiwa katika umri mdogo na wengine huwachukua muda. Kwa mfano, katika
umri huu kushindwa kujua ni nini unakitaka katika maisha yako kinaweza
kuibua wasiwasi kwa wazazi, ndugu au jamii nzima inayokuzunguka.
Kuwa
katika mahusiano ya kudumu. Kuna ule usemi unaosema, ‘Vunja mifupa kama
meno bado ipo,’ ulijipatia umaarufu pia kupitia mwanamuziki mashuhuri
wa muziki wa bolingo, Samba Mapangala. Semi huwa zina maana tofauti
kulingana na watu wataamua kuzitafsiri na kuzitumia kwa malengo gani.
Lakini itapendeza kuzitumia katika njia zenye manufaa zaidi. Vijana
wengi huubeba usemi huo na kuutafsiri kama ukiwa kijana pengine huwa ni
fursa ya kujihusisha na mahusiano na wanawake tofauti tena kwa nyakati
tofauti. Lengo, eti, ni kupata uzoefu na kupata mambo ya kuhadithia enzi
za ujana wako zilikuwaje pindi uzeekapo. Kama unafanya hivyo
unajiongopea. Kuwa na mahusiano ya kudumu na msichana mmoja hukupatia
fursa mwanaume ya kutulia na kujipanga na maisha yako.
Kuelimika
(darasani au njia nyinginezo). Zipo njia nyingi za kujielimisha sio
lazima mpaka upitie darasani na kupata astashahada, stashahada au
shahada juu ya taaluma mbalimbali. Vipato na fursa hutofautiana katika
kulifanikisha hilo, lakini kama unapata fursa hiyo ni vema kuitumia
ipasavyo. Elimu pia hupatikana kwa njia ya mafunzo, semina, warsha au
kufundishwa na watu wa kawaida ambapo fursa ni nyingi katika jamii
inayokuzunguka. Zipo fursa za kujifunza katika jamii tunamoishi lakini
watu hupuuzia tena zingine huwa ni bure kabisa. Mwanaume katika umri wa
miaka 30 hakikisha unakuwa na elimu, ujuzi au ufahamu juu ya mambo
tofauti ambayo yatakurahisishia katika kupata kipato kwa urahisi.
Kuwa
na makazi maalum au ya kudumu. Siyo lazima mpaka ujenge kwani hilo
linategemeana na uwezo wa mtu lakini unaweza kupanga pia. Itakuwa ni
vema katika umri huu mwanaume unakuwa unaishi kwako. Hii itakurahisishia
zaidi kujipanga zaidi katika maisha yako. Ingawa kuna familia zingine
huwa zina namna tofauti za kuwaruhusu vijana wao kujitegemea lakini hata
kama mnamiliki nyumba kubwa au kadhaa za kuishi basi angalau unakuwa na
sehemu yako ukijtegemea.
Kuwa
na shughuli ya kujiingizia kipato (kuajiriwa au kujiajiri). Katika
jamii yoyote ile hatutegemei kumuona kijana wa umri wa miaka 30 bado
akiwa yupo nyumbani hajishughulishi na shughuli yoyote ya kujiingizia
kipato. Sio lazima mpaka uajiriwe ila kama una fursa hiyo ni vizuri
lakini pia unaweza kujiajiri kwa kufanya biashara zako mwenyewe.
Kujitegemea.
Kwa familia zetu za kiafrika hususani kitanzania kuna umri ukifikia
wazazi huwa hawajihusishi kabisa na wewe kwa kukuhudumia. Jitihada zote
huelekezwa kwa wengine wadogo na tena huhitajika wewe kama mkubwa
kuwasaidia kwa masuala madogomadogo. Itakuwa ni jambo la aibu kwa
mwanaume wa miaka 30 analalamika eti hapewi hela ya matumizi na wazazi
wake au ananyimwa fedha za kununulia hata mavazi yake mwenyewe.
Kuwajibika.
Kuna mambo fulani kama vijana huwa tunayafanya kwa kujiamini kwamba
umri una ruhusu na muda upo wa kutosha wa kuja kutulia siku za usoni.
Lakini katika umri wa miaka 30 inabidi sasa ubadilike kwa kuachana na
baadhi tabia ambazo unaona hazikusaidii katika maisha yako ya sasa na
baadaye. Inabidi ufikie muda sasa uanze kuwajibika kwako wewe mwenyewe
na watu wako wa karibu wanaokuzunguka.
Kujiwekea
malengo. Kama unamfuatilia mwanzilishi wa kampuni ya Alibaba ambayo
inajihusisha na manunuzi kwa njia ya mtandao duniani, Bw. Jack Ma, basi
utakuwa umekumbana na msemo wake unaosema, ‘Ukiwa masikini katika umri
wa miaka 35 basi utakuwa umejitakia mwenyewe.’ Msemo huu una maana kubwa
sana katika kutukumbusha kwamba ili kufanikiwa katika maisha lazima
tujiwekee malengo na mikakati ya namna ya kuyafanikisha. Kama kijana
kamwe usitarajie miujiza ya mafanikio kama unaishi bila ya kujiwekea
malengo. Haijalishi iwe ni ya mwaka mmoja, mitano au kumi, ni vema
kujiwekea na kuwekeza bidii na jitihada katika kuhakikisha
unayafanikisha.
Kujua
kuendesha chombo cha moto (gari au pikipiki). Kuna msemo maarufu wa
wazungu unaosema, ‘Mafanikio huja pale maandalizi yanapokutana na
fursa.’ Nadhani utakuwa umekwisha kukutana na simulizi za mtu kukosa
kazi kwa sababu tu ya kutokuwa na ujuzi fulani. Katika dunia ya sasa
miongoni mwa ujuzi ambao mtu anatakiwa kuwa nao ni udereva wa chombo cha
moto iwe ni pikipiki au gari. Kwanza ni rahisi kujifunza, pili vyuo
vipo vingi vya kujinza na tatu haihitaji gharama kubwa kufanya hivyo.
Kuwa na ujuzi huu ni faida kubwa kwa mwajiri kwani pengine inaweza
kumrahisishia gharama za kumuajiri na kumlipa mtu mwingine kufanya
hivyo.
Kujiwekea
akiba. Kama kijana lazima uwe na mpango wa kujiwekea akiba sasa kwa
ajili ya maisha yako ya baadaye. Zipo njia nyingi za kuweka akiba kwa
sasa zinazotolewa na taasisi mbalimbali ukiachana na ile ya lazima
ambayo serikali huwataka waajiri kuwaunganisha wafanyakazi wao na mifuko
ya hifadhi za kijamii. Kama kijana pia unaweza kufanya hivyo kwa
kutembelea benki na mifuko tofauti na kujua ni namna gani unaweza
kufanya hivyo.
Nafikiri
utakuwa umejifunza au angalau kufunguka akili juu ya masuala ya msingi
ya kuyazingatia kama kijana unayeingia au tayari una umri wa miaka 30.
Kama bado haujafanya au kufanikikisha jambo lolote miongoni mwa
yaliyotajwa hapa, Jumia Travel inaamini bado haujachelewa. Fanya maamuzi
na ujipange sasa ili kuwa kijana mfano wa kuigwa kwa jamii na taifa kwa
ujumla.
Post a Comment