Waziri Mkuu Majaliwa Akutana Na Wadau Wa Zao La Korosho Dodoma
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wadau wa zao la Korosho kwenye
ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma Septemba 5, 2017. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja
na Bodi ya Korosho Tanzania zifanye tathimini ya maandalizi ya msimu
ujao kwa wakati na zimpatie taarifa mara moja.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana usiku (Jumanne, Septemba 5, 2017) wakati
akizungumza na wadau wa zao la korosho kwenye kikao alichokiitisha
ofisini kwake mjini Dodoma kujadili mwenendo wa zao la korosho na
ununuzi wa pembejeo.
“Lipo
tatizo la tathmini ya maandalizi ya msimu kutofanyika kwa wakati na
kusababisha matatizo kutotatuliwa kwa wakati. Bodi na Wizara zitoe
tathimini ya maandalizi ya msimu ujao kuhusu vyama vya ushirika
vilivyojipanga, upatikanaji wa vifaa kama magunia na nyuzi, maghala,
masoko, mizani, minada, malipo na mfumo wake,” alisema.
Waziri
Mkuu pia alizitaka Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Korosho zitoe
tathimini ya maandalizi ya msimu ujao katika maeneo ya mashamba, miche,
pembejeo na viatilifu. Alisema tangu Serikali iamue kusimamia mazao
makuu matano ya pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku hajapata muda wa
kukaa na kuongea na wadau wote. “Serikali imeamua kufuatilia usimamizi
wa mashamba; kusimamia upatikanaji wa mbegu, miche na pembejeo;
kufuatilia uvunaji na mfumo wa masoko ya korosho na pia kufuatilia mfumo
wa ushirika katika baadhi ya mazao,” alisema.
Alisema
hivi sasa zao la korosho linalimwa katika wilaya 50 kwenye mikoa 11 ya
Dodoma, Iringa, Lindi, Mbeya, Morogoro na Mtwara. Mingine ni Njombe,
Pwani, Ruvuma, Singida na Tanga.
“Katika
msimu wa mwaka 2016/2017 zao la korosho lilikuwa ni moja kati ya mazao
ya kibiashara yenye tija na faida nyingi kwa kuliingizia Taifa fedha za
kigeni kiasi cha dola za Marekani milioni 346.6,” alisema na kuongeza
kuwa katika msimu wa mwaka 2017/2018 watendaji hawana budi kujipanga
vizuri ili zao la hilo liendelee kuliingizia Taifa dola nyingi zaidi kwa
kuwa Serikali imetoa viatilifu bure.
“Ninasisitiza
eneo hili kwa sababu tumebaini kuwa korosho inachangia zaidi ya
asilimia 50 ya mapato kwenye Halmashauri zinazolima kwa wingi zao hilo.
Kwa kuwa zao hili ni la kimkakati, naitaka Wizara inipatie taarifa
sahihi na kwa wakati,” alisisitiza.
Alisema
Agosti mwaka huu, alipofanya ziara mkoani Tabora, alielezwa kwamba
wilaya ya Uyui na Tabora Manispaa zimeanza kulima zao hili kama zao
mbadala ili kuinua uchumi wa wananchi wake. “Tabora itakuwa mkoa wa 12,
kwa hiyo Wizara ya Kilimo itembelee maeneo haya na kuona inawezaje
kuwasaidia, ikaangalie uzalishaji ukoje kwani mti unaweza kukubali kuota
pale Tabora lakini usizae kwa wingi kama ilivyo kwa mikoa mingine,”
aliongeza.
“Viongozi
wa juu Serikalini hadi kwa mtendaji wa kijiji ni lazima tusimamie zao
la korosho, kila mtendaji ashirikiane na taasisi ambata, wizara mama
iimarishe vyuo vya kilimo na utafiti. Kila mtendaji ni lazima ajue na
wakulima wangapi, je kila mkulima ana ekari ngapi na kila ekari ina
miche mingapi,” aliongeza.
Ili
kurekebisha dosari zilizojitokeza katika msimu uliopita na kuboresha
utendaji katika msimu ujao, Waziri Mkuu alisema Wizara na Bodi zinapaswa
kufanya tathmini ya uhakika kwa kushirikiana na ofisi za mikoa.
“Tumepata
matatizo ya msimu kutoanza kwa wakati kwa sababu ya kukosekana kwa
tathmini za nyuma, hatuna pa kuanzia kufanya marekebisho kwa sababu
hatuna uzoefu wa yaliyojiri kwenye msimu uliotangulia. Siyo Bodi, Wizara
wala Ofisi ya Mrajisi ambayo imekwishafanya tathmini. Kazi zote
zimeacha kwa Wakuu wa Mikoa kupitia Sekretarieti za Mikoa.”
Akielezea
kuhusu mwenendo wa biashara ya zao hilo, Waziri Mkuu alisema ili
wakulima waweze kuwanufaika zaidi, Serikali imeendelea kuimarisha mfumo
wa malipo wa stakabadhi ghalani na kupambana na watu wasio waaminifu
wanaotumia kangomba. Kangomba ni kopo linalotumiwa na wanunuzi binafsi
ambalo ujazo wake haufikii hata kilo moja, lakini wao wanalitumia kama
kipimo cha kilo moja kununulia korosho kwa wakulima.
“Kuanzia
sasa, biashara ya kangomba ni marufuku, kangomba ni wizi na yeyote
atakayekamatwa, achukuliwe hatua za kisheria. Kila mkoa uweke mkakati
makini wa kudhibiti biashara ya kangomba,” aliagiza.
“Hatutaki
kusikia biashara ya kangomba. Viongozi wa Serikali msiwatumie vijana
kwa kuwapa mitaji ili wafanye biashara hii. Mkizikamata korosho za
kangomba, piga mnada na fedha ziende kwenye chama cha ushirika cha pale
zilipokamatwa,” alisema.
Kuhusu
makato ya unyaufu (shrinkage), Waziri Mkuu alisema kuanzia sasa, vyama
vya ushirika vya msingi (AMCOS) na Chama Kikuu haviruhusiwi kutoza hela
ya unyaufu kwa wakulima.
“Sheria
ya unyaufu inasema utauza korosho kwa asilimia 0.5 ya bei halisi ya
korosho iliyokaa kwa zaidi ya miezi sita. Sasa hapa kwetu msimu wa kuuza
ni Oktoba hadi Desemba, unyaufu hapo unatoka wapi? Hili haliwahusu
wakulima wetu kabisa,” alisema.
Alisema suala la unyaufu litawahusu wanunuzi ambao watakuwa wamenunua korosho na kuzihifadhi kwenye maghala kwa muda mrefu.
Kikao
hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Nchi OR- TAMISEMI, Bw. George
Simbachawene; Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles
Mwijage; Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha;
Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule; Mwenyekiti wa Bodi
ya Korosho, Mama Anna Abdallah; Warajis Wasaidizi wa Mikoa; Mkurugenzi
wa Bodi ya Korosho, Mkurugenzi wa Maghala na Mizani, Wajumbe wa Bodi ya
Korosho, Wenyeviti wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi, na
Mameneja wa Vyama Vikuu.
Post a Comment