SOKA INA FEDHA KWELI LAKINI BADO TUNAISHI MAISHA YA KULALAMIKA TUKIWA NA KILA KITU
Na Saleh Ally, Manchester
BINAFSI
nimeamua kuchagua kujifunza kila kukicha hadi mwisho wa maisha yangu
yote. Huu ni uamuzi binafsi unaohusisha imani yangu kutokana na mambo
ambayo nimepitia kwa takribani miaka 20 ya kushiriki katika michezo.
Kujifunza
ni jambo jema zaidi kwa kuwa kila unapopokea mafunzo fulani basi
unagundua ulichokuwa unakijua awali kimepungukiwa jambo fulani ambalo
hukulitegemea.
Kabla
ya kujifunza jambo, wanadamu tuna tabia ya kuamini tuko vizuri na
tunajua vitu vingi. Lakini unapotoa nafasi ya kujifunza jambo jipya basi
unagundua kuwa haukuwa unajua kama ulivyokuwa unafikiri.
Elimu
ni jambo jema na wakati mwingine vizuri kuifuata kokote inapopatikana
kuliko kusubiri ikukute ulipo utafikiri yenyewe ndiyo ina shida na wewe.
Niko
jijini Manchester ambako nimeanza ziara yangu ya mafunzo, Mungu
akijaalia leo nitaondoka kwenda jijini London kumalizia ziara hii ya
mafunzo.
Nikiwa
Manchester siku ya nne leo, nimejifunza mambo mengi sana lakini kubwa
ni namna ambavyo wenzetu wanautumia mpira kama biashara kubwa kabisa
kuliko sisi tunavyoamini ni ushabiki kuonyesha machungu kuwa wewe ni
shabiki wa timu fulani.
Wengi tunaamini kuonyesha unaipenda timu fulani inatosha sana na wakati mwingine ndiyo jambo la mwisho kabisa.
Lakini
wako ambao hasa kwa upande wa viongozi wanaamini kuwa timu moja
kuifunga nyingine ndiyo kazi pekee ambayo inatakiwa kufanywa na
kiongozi.
Yote
haya ni sawa lakini kwa kiwango cha chini kabisa kwa kuwa ni sehemu
ndogo sana kwa viongozi na wengine yaani mashabiki kwamba wanatakiwa
kwenda zaidi ya hapo.
Unapofika
katika Jiji la Manchester, asilimia 60 ya watalii wa jiji hili
wanaonekana wako hapa kuutembelea Uwanja wa Old Trafford na kiasi Uwanja
wa Etihad ambao unamilikiwa na Manchester City.
Old
Trafford mali ya Manchester United ni kivutio cha utalii kama ambavyo
watalii hutua nyumbani Tanzania kwa ajili ya kwenda kuangalia wanyama
mbugani au kutembelea katika fukwe zenye mvuto kule Zanzibar.
Wenzetu
hawana wanyama kama ilivyo sisi ambao watu wangefika kuwaangalia. Hata
fukwe zao si zenye mvuto kama ilivyo za kwetu lakini wanaingiza fedha
nyingi za utalii kupitia mpira, jambo ambalo hawajapewa na Mungu kama
ilivyo kwetu lakini wametumia akili zao za ziada.
Akili
za ziada kwa kuwa wameangalia kibiashara zaidi jambo ambalo linataka
ubunifu na kujituma bila ya kuchoka. Lakini sisi bado tumebaki kwenye
kuamini soka ni burudani na mmoja kumfunga mwingine basi inatosha na
kazi inakuwa imeisha, hili si jambo jema hata kidogo.
Mmoja
wa dereva teksi wa hapa Manchester ameniambia wanaingiza fedha nyingi
kupitia watalii wanaokuja kuutembelea Uwanja wa Old Trafford pia Etihad
ingawa ni kwa kiwango kidogo sana.
Ameniambia
wanaona ushabiki wao una faida na wako tayari kusaidia kwa mawazo ili
kuhakikisha timu hiyo inafanikiwa kufanya vema badala ya kufa.
Yeye
ni shabiki mkubwa wa Man United na haipendi kabisa Manchester City.
Lakini angependa kuona Man City inaendelea kuwepo ili kuongeza ushindani
unaolitangaza jiji hili ili wapate mambo mawili.
Kitu
cha kwanza anachotaka ni furaha ya moyo ambayo hata mashabiki wa kwetu
wanaipata. Lakini pili ni fedha, anaingiza kutokana na timu hizo kuwa na
mashabiki wengi wakiwemo wale wanaotokea nje ya England ambao
wanaonekana ni wengi zaidi.
Shabiki
wa Tanzania unafaidika na nini na timu yako? Furaha pekee inaposhinda
na maudhi inapofungwa? Kingine? Umewahi kujiuliza pia unaisaidiaje
iendelee kuwepo pamoja na mpinzani?
Lazima
tujifunze kwamba soka ni fedha nyingi sana na klabu sasa zifanye kazi
kwa kushirikiana na wataalamu wa biashara wenye mlengo wa soka wanaoweza
kujua utajiri ulipojificha kuliko kuendelea kufanya kama tulivyo sasa.
Tunacheza ngoma, wimbo ni kilio cha njaa lakini ukumbi wa shoo yenyewe
uko juu ya mgodi.


Post a Comment