ad

ad

PENZI LA GWAJIMA, FLORA JIPU PWAA!

Askofu Gwajima.

TAKRIBAN miaka miwili iliyopita kuliibuka sarakasi ya aina yake  katika ndoa ya waimba Injili wawili Bongo, Emmanuel Mbasha na Flora Mbasha ambazo zilisababisha mastaa hao kutalikiana mahakamani.

Katika sakata hilo, Mbasha alishusha tuhuma nzito zisizobebeka kwamba Flora alikuwa na uhusiano wa kimapenzi (penzi la Gwajima Flora) na baba mchungaji wao ambaye ni Askofu wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church almaarufu Ufufuo na Uzima, Dk Josephat Gwajima.

KIMYA KIREFU

Baada ya tuhuma hizo palipita kimya kirefu bila ufafanuzi toshelezi wa skendo hiyo ‘hevi’ lakini kwa mara ya kwanza, Flora amepasua jipu pwaa juu ya ni nini kilichotokea. Kupitia kitabu chake ambacho Ijumaa Wikienda lina nakala yake kilichoingia sokoni wiki iliyopita, pamoja na mambo mengine yasiyoandikika gazetini, Flora alimtuhumu Mbasha kwa mambo mazito ikiwemo hilo la kumpa penzi Askofu Gwajima.

TUJIUNGE NA FLORA

“Wakati tatizo lile linatokea tulikuwa tunasali kwa Askofu Gwajima ambaye tulikuwa tukimuita uncle (mjomba). Kwa hiyo tulikuwa tukisali kwa Uncle Gwajima. “Kabla ya kuondoka nyumbani (kuachana na Mbasha), nakumbuka ilikuwa Jumamosi, siku hiyo nililala sebuleni kwa kuwa nikilala chumbani
alikuwa akinipiga sana na alishaniambia hanitaki.

“Kulipokucha asubuhi, niliwaandaa watoto, nikamuomba atupeleke kazini lakini alikataa na ulitokea ugomvi mkubwa sana. Alinipiga sana.Madam Flora.

ASHINDWA KUIMBA

“Basi niliondoka na wanangu nikaenda kanisani (kwa Gwajima), siku hiyo sikuweza hata kuimba. Nilikuwa ninalia tu na kwamba nilisema siwezi kurudi tena nyumbani (Tabata). “Baada ya ibada nilimfuata Uncle Gwajima pale madhabauni, akaniuliza kwa nini ninalia? Nilimwambia twende nyumbani kuna tatizo kubwa mwenzangu ataniua, ananitesa sana.

GWAJIMA ASHINDWA KUAMINI

“Lakini Mchungaji Gwajima alikataa kabisa maana hakuamini ninachomueleza, akasema mwenzako huyu unayeimba naye hapa kila siku? Nikamwambia ndiyo! Akasema Flora unamsingizia mwenzako, haiwezekani! Gwajima hakuamini, alikuwa na pesa kidogo, akanipa, akasema nenda mkale chakula na watoto kisha urudi nyumbani na kama likitokea tatizo kubwa usiku nimpigie au nipite kituo cha polisi nichukue namba ili niwapigie.

ACHANGIWA LAKI 9

“Siku nyingine sikuwa na pesa kabisa maana akaunti yangu alikuwa ameishikilia mwenzangu na nakumbuka mara ya mwisho ilikuwa na kama shilingi milioni 50. Nilimweleza uncle (Gwajima) hali yangu. Ikabidi Jumapili iliyofuata akaniita, nikaimba, akaomba kanisa linichangie kwa sababu nimepata matatizo lakini hakusema ni matatizo gani. “Ni kweli kanisa lilinichangia pesa laki tisa ambayo ilinisaidia sana.

UHUSIANO NA GWAJIMA (penzi la Gwajima Flora)

“Sasa kuhusu uhusiano na Gwajima, mwenzangu ndiye aliyeanza kuzisambaza habari hizo kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. “Hata alipopigiwa simu na Mchungaji Gwajima alimwambia kuwa ana maadui wengi na hao ndiyo wanamchafua. “Tulikaa vikao vingi na watu mbalimbali akiulizwa kuhusu uhusiano wangu wa kimapenzi na Mchungaji Gwajima. Alikuwa akikataa kwamba si yeye aliyesema maneno hayo bali ni maneno ya watu tu.

NGOMA DROO

“Aliambiwa aeleze kwenye media (vyombo vya habari) ili watu wajue habari hizo siyo za kweli lakini alikuwa anakataa. Akasema yeye amechafuka na skendo ya ubakaji (alidaiwa kumbaka mdogo wa Flora) hivyo alitaka watu tuchafuke kama yeye ili ngoma iwe droo.


Emmanuel Mbasha.
“Ukweli ni kwamba aliamua kumsingizia Mchungaji Gwajima akijua kuwa ataogopa kuchafuka hivyo angemsaidia kufuta kesi yake (ya ubakaji) iliyokuwa polisi lakini hakujua kuwa kwa kufanya hivyo ndiyo alikuwa anajiharibia zaidi. “Pamoja na hayo yote, Uncle Gwajima aliendelea kunishauri sana nirudi kwangu, lakini nilikataa kwa maana nilijua kuwa iwapo nitarudi ninakifuata kifo na siyo ndoa.

“Unajua mwanzoni sikutaka kumshirikisha Mchungaji Gwajima kwenye misukosuko hiyo kwa sababu hiyo tu, mwenzangu alikuwa tayari ameanza kuzusha kuwa nina uhusiano naye, jambo ambalo halikuwa na ukweli wowote. Binafsi nilikuwa ninajisikia vibaya sana kusingiziwa juu ya mtumishi huyo wa Mungu.

MKE WA GWAJIMA

“Baada ya misukosuko kuzidi, Mchungaji Gwajima pamoja na mke wake (mke wa Gwajima alijua kila kitu kinachoendelea juu ya sakata hilo) na watumishi wasaidizi walikuwa wakiniita na kunisihi sana nimsamehe mwenzangu ili nirudi nyumbani lakini nilisimamia ukweli wangu kwa maana maumivu niliyoyapata, niliyapata mimi na siyo wao.

WAMSIHI ASAMEHE

“Pamoja na mwenzangu kuendelea kutangaza kuwa nina uhusiano (wa kimapenzi) na Mchungaji Gwajima (penzi la Gwajima Flora) lakini bado mchungaji huyo, pamoja na mke wake na wasaidizi wao, waliendelea kunisihi nimsamehe kwa kuwa walikuwa wanaamini kuwa uongo uliokuwa unaendelea kusambazwa lilikuwa ni pepo na kwamba siku moja ataacha.

Sikuwahi kuwa na uhusiano na Mtumishi wa Mungu Josephat Gwajima, hivyo kusambaa kwa uongo kuwa nimezaa naye ni kumkosea sana Askofu Gwajima, waumini wake pamoja na Mungu anayemtumikia,” alimalizia Flora kupasua jipu juu ya madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Gwajima. (penzi la Gwajima Flora).

MBASHA ATAFUTWA

Alipotafutwa Mbasha kuulizwa kama amepitia maudhui ya kitabu hicho na kwamba kinamtuhumu mambo mazito hakupokea simu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu. Hata hivyo hivi karibuni, Mbasha alilihoji Ijumaa Wikienda: “Kwani hicho kitabu hakiwezi kuuzika bila kunitaja mimi?”

SASA MADAM FLORA Kwa sasa Flora ameolewa na mwanaume mwingine, Daud Kusekwa na kubadili jina ambapo kwa sasa siyo Flora Mbasha bali ni Madam Flora.
Stori: Waandishi Wetu | IJUMAA WIKIENDA |Dar

No comments

Powered by Blogger.