Nassari, Lema Wakubali Kupeleka Ushahidi wao TAKUKURU
Wabunge
wa Chadema, Godbless Lema na Joshua Nassari wamesema watapeleka kwa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ushahidi kuhusu
madiwani saba waliojiuzulu katika majimbo yao wanaowatuhumu kupokea
rushwa ili kujiuzulu nafasi zao.
Lema
ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini, amesema leo Jumatano kuwa,
wanashukuru Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola kuwakaribisha
kupeleka ushahidi.
"Tunashukuru
sana mkurugenzi mkuu wa Takukuru kutukaribisha, tutapeleka ushahidi
wetu ofisini kwake na tunaamini atafanyia kazi tuhuma hizi," amesema.
Amesema
mbunge mwenzake wa Arumeru Mashariki, Nassari ambaye madiwani watano
katika jimbo lake wamejiuzulu amekwenda Nairobi nchini Kenya kuonana na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ili kupata baraka zake kabla ya
kwenda Takukuru.
"Nassari
amekwenda Nairobi kuonana na Mwenyekiti Mbowe ili kumweleza tukio hili
na akirudi tutakwenda naye moja kwa moja kwa Mkurugenzi Mkuu wa
Takukuru, Mlowola," amesema.
Post a Comment