Mwigulu: Tunamsubiri Tundu Lissu Apone ili Atusaidie Kukamilisha Upelelezi
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amezungumzia uchunguzi wa
tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akisema anaamini akipona atatoa mchango
mkubwa katika upelelezi.
“Lissu
tunamuombea akishapona atatupa mchango mkubwa wa kusaidia uchunguzi,
mtu akiwa kwenye maumivu makali huwezi kumuuliza lolote,” amesema
Mwigulu akizungumza leo Alhamisi katika kipindi cha Clouds 360.
Amesema
kutokana na upya wa uhalifu wa aina iliyotokea kwa Lissu, kuna mambo
wanaendelea kuyafuatilia ambayo hawezi kuyaeleza kwa sasa.
“Suala la Lissu kutokana na upya wake, kuna vitu tunaendelea kuvifuatilia, hivyo kuna mambo hatuwezi kuyasemea,” amesema.
Amewataka Watanzania waendelee kuwa na subira kwa kuwa kazi inaendelea kufanyika.
Mwigulu
amesema baada ya tukio la kushambuliwa Lissu Septemba 7, taarifa kadhaa
zilichukuliwa eneo la tukio ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ili
kupata undani wake.
“Wahalifu
hawajakamatwa wote, ukianza kusema itakuwa ni shida, kuna mambo
yanaendelea kufanywa na hayana ukomo. Ukomo utafikiwa endapo wote
waliohusika watakamatwa. Nikisema naweza kuvuruga kazi inayoendelea,”
amesema.
Akijibu
swali la mtangazaji wa kipindi hicho kuwa watu wanahoji kwamba askari
wanapouawa wahalifu wanakamatwa mapema Mwigulu amesema, “ Watu wakiwaza
hivyo watakuwa wanakosea, hatuweki madaraja, ni mazingira ya tukio tu.”
Akizungumzia
uchunguzi unaoendelea kuhusu kuvamiwa kwa Lissu amesema hawezi kueleza
waliokamatwa bali tayari kuna magari zaidi ya 10 yanayofanana na
lililohusika kwenye tukio yamekamatwa.
Mwigulu
amesema alimuona Lissu siku ya tukio Septemba 7 akiwa katika Hospitali
ya Rufaa Dodoma na baadaye uwanja wa ndege aliposafirishwa kwa ajili ya
matibabu jijini Nairobi nchini Kenya ambako yuko hivi sasa.
Amesema hajafika Nairobi kumjulia hali Lissu bali kwa Mkoa wa Singida, Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amefika.
“Katika
mazingira mengine tunaendelea kupata taarifa, kama Serikali tuna
balozi, kama waziri kwenda kumuona ni jambo jema katika utaratibu wa
uchunguzi hata dereva tutazungumza naye,” amesema.
Amesema dereva hivi sasa anapata tiba ya kisaikolojia na anaamini atakapokuwa tayari atazungumza na wanaokusanya taarifa.
Post a Comment