Manji Kurudi Yanga, Atangaza Bonge la Neema Klabuni Wachezaji Wasitisha Mgomo Fasta
WAKIJIANDAA na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara, wachezaji wa Yanga jana asubuhi waligomea mazoezi ya timu hiyo.
Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo irejee jijini Dar es Salaam ikitokea Songea kuvaana na Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji na matokeo kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Yanga wikiendi hii inatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar katika mchezo wa ligi kuu.
Tukio hilo la mgomo lilitokea dakika chache tangu wachezaji wa timu hiyo waanze kufika kwenye mazoezi ya timu hiyo saa mbili asubuhi katika Uwanja wa Uhuru.
Mara baada ya wachezaji kuwasili walionekana kukaa makundi huku wengine wakiwa wamekaa kwenye majukwaa na wengine wakisimama pembezoni mwa uwanja.
Ilipofika saa tatu muda ambao ulipangwa mazoezi yaanze, kocha mkuu wa timu hiyo, Mzambia, George Lwandamina akiwa na wasaidizi wake Shadrack Nsajigwa, Juma Pondamali na Noel Mwandila waliingia uwanjani tayari kwa kuanza mazoezi wakiwa wamevalia nguo za mazoezi.
Wakati makocha hao wanaingia uwanjani, wachezaji walionekana kugoma kuingia uwanjani na badala yake waliendelea kukaa makundi majukwaani wakiendelea kupiga stori. Ilipofika saa 3:30 asubuhi, wachezaji hao walianza kuondoka kwa mafungu kwa kuingia kwenye magari yao na wengine wakipanda bodaboda huku basi la timu hiyo likiondoka likiwa na Nsajigwa pekee.
Chanzo ambalo kilikuwepo uwanjani hapo lilizungumza na baadhi ya wachezaji kwa sharti la kutotajwa majina, wakasema wamegomea mazoezi hayo kutokana na kudai malipo ya mishahara yao ya miezi miwili.
“Ni ngumu kwetu kuendelea kufanya mazoezi tukiwa katika hali ngumu ya kiuchumi, wachezaji wote tunadai mishahara ya miezi miwili na mwezi huu wa Septemba ukimalizika tutafikisha miezi mitatu.
“Na kingine kinachotufanya tugomee mazoezi ni viongozi kutokuwa wakweli, wao walitakiwa watuahidi lini wanatulipa mshahara, kama unavyojua hali ya maisha imekuwa ngumu sana,” alisema mmoja wa wachezaji.
Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten, kuzungumzia hilo alisema: “Ni kweli kabisa timu haijafanya mazoezi leo (jana) asubuhi kutokana na maelekezo maalumu waliyopewa benchi la ufundi.
“Kuna jambo ambalo tulilifanya ambalo lilisababisha timu ishindwe kufanya mazoezi ya asubuhi.” Wakati wachezaji hao wakigoma, aliyekuwa mwenyekiti wa timu hiyo, Yusuf Manji ametuma ujumbe kuwa anaweza kurejea ndani ya klabu hiyo mara baada ya matatizo yake kumalizika.
“Manji amekubali kurudi lakini mpaka matatizo yake yatakapomalizika,” kilisema chanzo kutoka Yanga.
Post a Comment