Maajabu Hukuwahi Kuyasikia Kuhusu Uwanja Wa Old Trafford
Na Saleh Ally, Manchester
JUNI
2015 wakati Manchester United ikiivaa Southampton katika mechi ngumu ya
Premier League alikatisha panya uwanjani. Hii ilisababisha malalamiko
makubwa kwa mashabiki kwa kuwa lilionekana ni kama jambo la aibu kwa
klabu.
Januari
2016, Kocha Louis van Gaal alilalamika kwamba utengenezaji wa uwanja
sehemu ya kuchezea yaani pitch ulikuwa unachelewa licha ya klabu kutoa
pauni 800,000 (Zaidi ya Sh bilioni 2.3). Wakati mwingine wanalazimika
kuchelewa kufanya mazoezi kwa kuwa kunakuwa na mambo ya matengenezo.
Suala
la uwanja huo wa kuchezea kuonekana una matatizo lilionekana kuukerea
uongozi na Bodi ya Manchester United ambayo kikubwa inachotaka ni
kulinda heshima ya klabu hiyo maarufu kuliko zote England na moja ya
klabu tatu kubwa zaidi duniani, nyingine mbili zikiwa ni Real Madrid na
Barcelona zote za Hispania.
Baada
ya hapo, aliyepewa fedha kwa ajili ya kazi hiyo akahimizwa na yeye
akafanya kweli na awali, ilionekana ulitakiwa kuwa kama ule wa Wembley
ambao ni mali ya Serikali ya Uingereza lakini safari hii, pitch ya Old
Trafford inaonekana ndiyo bora zaidi England na ikiwezekana Ulaya na
inawezekana kufananishwa na ile iliyo katika Uwanja wa Emirates pekee.
Emirates unamilikiwa na wapinzani wakubwa wa Man United. Hawa ni Arsenal walio katika Jiji la London.
Nikisema
ni kati ya watu wachache ambao si wachezaji waliofanikiwa kufika kwenye
uwanja huo katika pitch ni mimi. Huenda hii ni bahati kubwa na
imenisaidia kujifunza ambacho nachangia nanyi wasomaji ili tujifunze
wote.

Kilichonivutia
ni baada ya kuwa pale katika pitch na wachezaji wakongwe wa
Barcelona na wale wa Man United. Wale wa Barcelona walianza kushangazwa
na namna ubora wa pitch ulivyo na mwisho nilimsogelea Eric Abidal na
kumuuliza kama ile ya Nou Camp haifanani na hiyo?
Abidal aliyekuwa tegemeo la FC Barcelona na sasa ni mmoja wa magwiji wa klabu hiyo aliniambia;
“Huu
ni uwanja wa aina yake, haufanani hata kidogo na ule wa Camp Nou.
Unajua, Camp Nou wana uwanja bora wa kuchezea, lakini huu ni bora zaidi.
Hata wa kule Madrid pia si kama huu.”
Hii
ikanifanya nivutiwe zaidi na hasa kwa kuwa niliona utaratibu wa
maandalizi siku moja kabla ya mechi namna majani yalivyokuwa yanakatwa
lakini wakati wa mapumziko. Waliingia vijana takribani 18 haraka na
kuanza kufanya marekebisho wakirudishia nyasi sehemu zilipong’oka.

Mwisho
niliwaona wakirudi mara tu baada ya mechi kwisha na kuanza kuzikata
nyasi na mashine nane zilizokuwepo tena wakienda kwa utaratibu maridadi
kabisa. Yaani kwa msitari na kila mmoja alijua anatakiwa kukata kona
kushoto au kulia.
Lakini
kabla mechi haijaisha, nilianza kumtafuta msimamizi mkuu wa uwanja
aliyejitambulisha kwa jina la Allah Smith ambaye alinithibitishia kuwa
pitch yao ndiyo bora zaidi duniani kwa kipindi hiki kutokana na
teknolojia mpya.
Akasema
hata kwa huduma inakuwa tofauti kwa kuwa Manchester United na Arsenal
ndiyo timu zilizoanza kutumia teknolojia mpya ya majani ya kawaida au
asili wenyewe wanasema natural kuchanganywa na yale ya bandia.
Unajua
kuna viwanja vya asili kama Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na ule
wa bandia kama ulivyo wa Uhuru lakini nyasi za Old Trafford ni asili
asilimia 97 na asilimia 3 ni bandia na hii ni kuyafanya majani kuwa
imara zaidi na mfumo mpya unaowafanya wachezaji kuwa salama zaidi.
Lakini
kama hiyo haitoshi, uwanja huo kwa chini una mabomba maalum yenye uwezo
wa kutengeneza joto kunapokuwa kipindi cha baridi au kuwa ya baridi
sana kunapokuwa kipindi cha joto kali ili kuufanya uwanja kuwa na hali
ya hewa isiyowapa tabu wachezaji.
Katikati
uwanja umeinuliwa kwa inchi nane ili maji ya mvua yamwagike pembeni
kutowasumbua wachezaji wakati wa mechi au kipindi cha mvua kubwa.
Mabomba
ya plastiki yaliyozungushwa chini ya uwanja huo yana urefu wa Kilomita
37 kama yatanyooshwa moja kwa moja. Ukubwa wa pitch ya Old Trafford goli
hadi goli ni mita 105 na upana ni mita 68.
Mara
ya kwanza uwanja huo wa kuchezea wa Old Trafford kufanyiwa marekebisho
ilikuwa ni mwaka 1999 baada ya Man Unted kushinda makombe matatu
likiwemo la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kocha Sir Alex Ferguson akataka
ufanyiwe marekebisho makubwa ili kuwapa nafasi ya wachezaji kupambana
vema wakiwa nyumbani.
Klabu
ikamwaga pauni 250,000 (zaidi ya Sh milioni 716) na ukarabati mkubwa
ukafanyika na kuanzia hapo haukufanyika tena hadi msimu huo wa 2012-13.
Post a Comment