ad

ad

Kujilinganisha ni kosa kubwa kwa wapendanao


KUTAMANI kitu cha mwingine kwa mtazamo chanya yawezekana ikawa ni jambo jema katika maisha. Yaani ukaona mwenzako ana maendeleo fulani, mfano ana nyumba na wewe ukapambana kuhakikisha unapata nyumba. Yawezekana ukaona mwenzako ana gari, ukajifunza mbinu alizopitia nawe ukazipita na kuhakikisha nawe unamiliki gari. Huo tunauita wivu wa maendeleo. Unamuona mwenzako ana kitu, haumuwekei chuki.

Unajitahidi kukipata. Akili inawaza. Inalinganisha hatua iliyonayo kwa kumtazama mtu mwingine. Inajipa jibu kwamba kuna kitu kwake hakipo sawa, kimepungua. Mathalan, mwenzake ana gari zuri ambalo akililinganisha na la kwake, anaona la kwake si zuri. Anatamani la mwenzake. Marafiki zangu, tunaruhusiwa kutamani vitu vya wenzetu kwa kujilinganisha na tulipo katika masuala mbalimbali ya maendeleo lakini si suala la
uhusiano. Uhusiano una kanuni zake.

Bahati mbaya sana hizo kanuni hazifanani, kila mtu ana zake. Unaweza kuona kanuni za mwenzako zinakufurahisha, ukaamua kuzitumia lakini zisifae kwako. Uhusiano unapaswa kuwa wako na mpenzi wako. Si vyema sana kujilinganisha na uhusiano wa mtu mwingine.

Watu wengi sana wamekuwa wakifanya makosa katika uhusiano. Wanajilinganisha na wengine. Mathalan, mwanaume anatamani  namna ambavyo pengine rafiki yake wa kike anavyomjali mpenzi wake. Anatamani jinsi anavyomheshimu. Anatamani jinsi anavyomwonesha mahaba hata mbele za watu. Hana aibu.

Popote pale anakuwa tayari kumbusu, kumuonesha kwamba hakuna mwingine zaidi yake. Yaani ni mahaba motomoto. Upande wa pili, mwenzangu na mimi mwanamke wake anakuwa mkali. Haoneshi ‘makeke’ kama ambayo mwanaume wake anayaona kwa rafiki yake.

Anaumia kweli. Anatamani uhusiano wa mwenzake. Akijilinganisha na wa kwake, anajiona kama yuko nyuma. Anajiona kama hayupo na mtu sahihi. Anakinukisha kwa mpenzi wake kwa kumhoji kwa nini yeye hamfanyii kama rafiki yake anavyomfanyia mwenzi wake.
Matokeo yake wanajikuta wakiishi maisha ya ugomvi.

JIFUNZE HAPA
 Kujilinganisha katika uhusiano kama nilivyoeleza awali ni kosa. Hupaswi kujilinganisha hata siku moja katika suala zima la uhusiano. Ishini nyinyi kama nyinyi. Penzi lenu linapaswa kuwa la kwenu. Msilinganishe na la watu wengine. Yawezekana mkaona wenzenu wanaishi vizuri au penzi lao ni zuri kumbe nao wana changamoto kubwa ambayo nyinyi hamuioni. Wanaifanya siri lakini machoni wanawaonesha ‘mapichapicha’ ambayo yanawavutia nyinyi.

Yawezekana nao wanavutiwa zaidi na uhusiano wenu nyinyi hamjui. Njia bora kabisa ya kuishi vizuri katika uhusiano ni kutolinganisha uhusiano wa watu wengine. Kama mnaona kuna kitu hakipo sawa kwenu, tumieni lugha rafiki kujirekebisha.

 Kama lengo ni kupiga hatua za uhusiano wenu, mfano labda mnataka kufikia hatua ya uchumba na baadaye ndoa, zungumzeni kwa lugha rafiki. Elekezaneni kwa kuzingatia uwezo wenu. Msilazimishe mambo. Linalowezekana leo, elekezaneni lifanyike. Linalowezekana kesho basi lifanyeni kesho.

 CHANGAMOTO HAZIFANANI
Kila mtu ana changamoto zake kwenye uhusiano. Wengine wanaonekana nje wanacheka kumbe moyoni wanateseka. Huwezi kuwajua. Boresha uhusiano wako. Kuwa na msimamo. Shikilia mahali ulipo, hata kama kuna upungufu unaouona, zungumzeni. Tatueni changamoto, mtafikia kilele cha mafanikio mkiwa pamoja

No comments

Powered by Blogger.