Aliyemwibia Kardashian jijini Paris Atuma Barua Kuomba Radhi
POLISI wamesema mtu aliyeongoza wizi dhidi ya mwanamitindo na mtangazaji maarufu wa Marekani, Kim Kardashian, akiwa jijini Paris, ameandika barua akimwomba radhi, lakini mrembo huyo amekataa.
Timu ya wanasheria wa Kim nchini Ufaransa ilipokea barua kutoka kwa Aomar Ait Khedache anayedaiwa kuongoza wizi huo Oktoba 2016. Inasemekana barua hiyo ilikuwa imeandikwa kwa mkono katika Kifaransa na ikafasiriwa na wanasheria wa Kim.
Sehemu ya barua hiyo inasema: “Baada ya kutambua masikitiko yako na matatizo ya kisaikolojia niliyokusababishia… Niliamua kukuandikia, si kwa ajili ya kutaka kujikomba kwako. Ninataka kuja kwako kama binadamu nikueleze ninavyojuta kwa kitendo changu, jinsi nilivyosikitika kutokana na kukuona ukilia.
“Fahamu kwamba ninasikitishwa na maumivu unayoyapata, wanao, mumeo na marafiki zako. Ninatumaini barua hii itakufanya usahau taratibu matatizo yaliyokukumba kutoka na kosa langu.”
Ni karibu mwaka umepita tangu Kim atishiwe kwa bunduki wakati anaibiwa vito vyake vyenye gharama ya Dola milioni 10 (sawa na zaidi ya Sh. 22 bilioni). Suala hilo limekuwa likionyeshwa kila mara katika televisheni nchini Ufaransa.
Vyanzo kutoka kwa Kim vinasema maneno ya Khedache ni ya kutaka kujifanya anasikitika tu kabla ya mashitaka kuanza. Inasemekana barua hiyo ilitumwa kwanza kwa jaji ambaye aliipeleka kwa wanasheria wa Kim.
Post a Comment