ad

ad

SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-14


 
 NYEMO CHILONGANI
Aliyesimama mbele yao alionekana kuwa kiumbe wa ajabu kuliko viumbe vyote alivyowahi kuviona tangu waingie huko kuzimu. Kiumbe huyu mwenye mwili mkubwa alikuwa na sura ya paka, alikuwa na masikio makubwa, ngozi yake haikuwa ya kawaida, kuna sehemu ilikuwa na mabakamabaka kama chura lakini sehemu nyingine alikuwa na manyoya mengi kama kondoo.
Ukiachana na hayo, miguu yake ilikuwa ni kwato za ng’ombe, nyuma alikuwa na mkia mkubwa uliokuwa na ncha kali kama mshale kwa kule mwisho. Alikuwa akitembea kwa kupiga hatua ndefu, alitisha sana kwani hata macho yake yalikuwa menkundu mithili ya moto mkali uliokuwa ukiwaka.
“Karibuni sana,” ilisikika sauti ya kiumbe hicho, alikuwa Lusifa mwenyewe.
Sauti yake ilikuwa na utetemeshi mkubwa, aliposema hivyo tu, mara ghafla miale kama ya radi ikaanza kuonekana mahali hapo. Ardhi ikaanza kutetemeka, kwa kifupi shetani alikuwa na utisho, kila sehemu alijaribu kujifananisha na Mungu.
Watu wote walikuwa kimya, walikuwa wakimsikiliza tu, kitu cha kwanza alichokisema ni kuwapongeza watu wale kwa kuwa kazi yao inaendelea vizuri duniani kwa kuwa idadi kubwa ya watu hawaendi makanisani wala misikitini, walikuwa wamemsahau Mungu kwa kuwa walisimama imara kuhakikisha Mungu haabudiwi kwa chochote kile.
Kwa watu waliokuwa matajiri, aliwapongeza kwa kuwa kupitia fedha zile alizowapa, watu wengi walishawishika na hivyo kuzitumia fedha hizo kwa kuwa tayari walizibania fedha nyingine zisiweze kupatikana kwa urahisi ili waendelee kuitawala dunia.
Hakuishia hapo, akawashukuru na wanasiasa ambao kila siku walihakikisha jina lake linakuwa juu, akawashukuru wanamuziki kwa kazi kubwa waliyokuwa wakiifanya kwa kuweka alama zake katika video zao zote walizokuwa wakizitoa kitu kilichoonyesha kwamba walikuwa wakifanya kazi kwa juhudi kubwa.
Akawashukuru na wachungaji waliokuwa wakitumia nguvu zake katika kuponya magonjwa, aliwasifia kwa sababu walikusanya washirika wengi kwa kile kilichokuwa kikitokea na hivyo kuwapotosha watu kumfahamu Mungu wa kweli, akaendelea kuwasisitiza kwamba wasihubiri kuhusu kuacha dhambi bali makanisa yao yahubiri kuhusu mafanikio tu na baraka tu ili waendelee kuyapenda.
Akawashukuru mashehe wote ambao nao walihakikisha misikiti haisimami kama inavyotakiwa kwa kuanzia ugomvi wa hapa na pale. Huko kote, alikuwa ameweka watu wake waliokuwa wakiaminika kwa asilimia mia moja.
Siku hiyo ilikuwa ni siku ya shangwe mno, damu ikaletwa na kisha kila mtu kuanza kugaiwa na kuanza kunywa. Kitendo cha kunywa damu ile tu, shetani akabadilika, akawa na muonekano kama wa malaika japokuwa hakuwa mweupe, yeye alikuwa malaika mweusi tii mwenye macho mekundu.
Mabawa yake nayo yalikuwa yamechanikachanika kama yule kiumbe waliyekutana naye kule walipotoka. Mzee Hamisi akatamani kuuliza lakini akashindwa kufanya hivyo.
“Nahisi kuna mtu ana swali,” alisema Lusifa huku akiwaangalia.
“Nitakwenda kuwajibu. Hapo zamani kulikuwa na vita kati yangu, wenzangu na bwana mkubwa, katika vita ile, tulionekana kushinda kwa asilimia kubwa lakini hatujui ni wapi tulijichanganya, tukashtuka tukipigwa na kisha kushushwa huku tulipo. Ile moto waliyokuwa wakiitumia ndiyo iliyoyafanya mbawa zetu kuwa kama hivi mnavyoona,” alisema Lusifa huku jina bwana mkubwa akimaanisha MUNGU!
“Nitakwenda kuwapa nguvu.”
Aliposema hivyo, miale ya mwanga ya rangi ikaongezeka na kisha kujikusanya sehemu moja na kuingia ndani ya chungu kimoja kikubwa, alichokifanya baada ya kuona hivyo ni kukifuata na kisha kuingiza mkono wake ulikuwa na vidole vyenye kucha ndefu na kutoa kitu fulani ambacho kilifanana na usinga ila hicho kilikuwa kikubwa na kisha kuanza kukipiga kuelekea kwa watu watu.
“Hiyo ndiyo nguvu yenu,” alisema Lusifa huku akiendelea na kazi ile.
Watu walikula na kunywa, katika kipindi chote hicho hawakutakiwa kuongea, ni Lusifa peke yake ndiye aliyetakiwa kuzungumza mahali hapo, wote walifanya vitu kwa ishara tu, hata kama utakuwa unahitaji kikombe cha damu, ulitakiwa kuonyesha ishara na kisha kukabidhiwa.
Hicho ndicho kilichoendelea kule kuzimu, watu walisherehekea kwa kuwa kila kitu kule duniani kilikwenda kama kilivyotakiwa. Baada ya sherehe hiyo fupi kumalizika ndipo watu walipopewa ruhusa ya kuzungumza na kuulizwa kile walichotaka kufanyiwa.
“Ninataka utajiri wangu uongezeke.”
“Ninataka niwe na nguvu kubwa zaidi.”
“Ninataka niwe na heshima kubwa.”
“Ninataka niogopwe.”
“Ninataka umaarufu wangu uongezeke.”
Kila mmoja alizungumza lake, na kila alilolisema mahali hapo, alipewa nguvu ya kupokea. Zamu ya mzee Hamisi ilipofika, akaweka wazi kwamba alihitaji nguvu zaidi, na pia alitaka kuongezewa majini mengi, yenye nguvu kwa ajili ya kupambana na wabaya wake,.
Watu wote waliokuwa mahali hapo wakaangua vicheko, hata Lusifa mwenyewe akaanza kucheka. Mzee Hamisi akashangaa juu ya vicheko vya watu wale kwani hata mzee Hamadi naye alikuwa akicheka.

Je, nini kitaendelea?
Kipi kimewafanya watu hao kucheka?
Tukutane Jumatano hapahapa.

No comments

Powered by Blogger.