Rais Magufuli afanya ziara ya kushtukiza Feri Dar na kutoa maagizo kwa RC Makonda
Baada
ya kukata tiketi yake Mhe. Rais Magufuli alipata wasaa wa kuzungumza na
wananchi aliosafiri nao katika kivuko cha MV Kigamboni na baadaye
kuzungumza na wananchi wa Kigamboni ambapo ameulizwa na kujibu mambo
mbalimbali.
Kuhusu
ubovu wa barabara Mhe. Rais Magufuli alisema Serikali imechukua hatua
ya kukabiliana na tatizo hilo kwa kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini
na Mijini (TARURA) ambayo itafanya kazi ya kutengeneza barabara kwa
kiwango cha lami.
Kuhusu
tatizo la kukatika kwa umeme alisema Serikali inatekeleza miradi
mbalimbali itayoongeza kiwango cha umeme katika gridi ya taifa pamoja na
kurekebisha miundombinu yake na amewaomba kuwa na subira wakati juhudi
hizo zinaendelea.
Akiwa
katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere Mhe. Rais Magufuli alikutana
na vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka vyuo na vyuo vikuu vya
Mkoa wa Dar es Salaam waliopiga kambi katika chuo hicho, ambao
wamempongeza kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kuiongoza Serikali ya
Awamu ya Tano ambayo kwa muda mfupi imeonesha uongozi unaoacha alama.
Vijana
hao walimhakikishia kuwa wanamuunga mkono na wamemuahidi kuwa wapo
tayari kuitumikia nchi kwa jukumu lolote watakalopewa na kwamba daima
watatanguliza maslahi ya nchi.
Akizungumza
na vijana hao Mhe. Rais Magufuli aliwapongeza kwa moyo wa uzalendo
waliouonesha, na amewataka kuwa nguzo imara ya mabadiliko ya kweli
nchini ili juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kurekebisha
mambo yaliyosababisha kukiuka misingi ya Waasisi wa Taifa zizae matunda.
Mhe.
Rais Magufuli alieleza baadhi ya juhudi hizo kuwa ni kukabiliana na
rushwa inayodhohofisha uchumi na huduma za kijamii, kudhibiti mianya ya
matumizi mabaya na upotevu wa fedha na mali za umma, kuondoa watumishi
hewa na wenye vyeti vya kughushi, kuongeza bajeti ya maendeleo katika
bajeti ya Serikali, kuongeza uzalishaji wa umeme, kujenga viwanda,
kujenga reli, kununua ndege za Serikali, kuongeza ukusanyaji wa kodi na
kuchukua hatua kali dhidi ya wahujumu uchumi.
“Nataka
niwahakikishie vijana wote kuwa nawapenda sana, hata mimi nilikuwa
Umoja wa Vijana, yote yaliyotokea kinyume na misingi ya chama hiki na
misingi ya waasisi wetu wakiongozwa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere
nimeamua kuyanyoosha na yatanyooka, na nyinyi simameni imara,
kitumikieni chama na msitumikie watu au vikundi vya watu, mkifanya hivyo
kila kitu kitakwenda vizuri kabisa” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli aliwataka vijana hao kujitokeza kugombea nafasi
mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa chama utakaofanyika baadaye
mwaka huu, na amebainisha kuwa wasiwe na hofu ya kuwepo kwa rushwa kwa
kuwa wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa hawatapitishwa kuwania
nafasi za uongozi ndani ya chama.
Pia
aliwaambia viongozi wa Secretarieti ya CCM aliowakuta wakizungumza na
vijana hao kuwa anazo taarifa zote juu ya watu waliojimilikisha mali za
chama na amesema anasubiri wakati ukifika achukue hatua zinazostahili.
Baada
ya kuzungumza na vijana hao Mhe. Rais Magufuli alitembelea Daraja la
Nyerere na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo, ambapo alimuagiza Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda kufanyia kazi ombi la wananchi
kujengewa kituo cha Daladala.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Agosti, 2017
Post a Comment