Kenyatta: Nawashukuru wananchi kwa kuwa na imani nami
Rais Uhuru Kenyatta, akihutubia baada ya kutangazwa mshindi wa urais wa Kenya, amewashukuru wananchi kwa kuwa na imani naye na serikali yake.
"Nawaahidi tutaendelea na kazi tuliyoianza. Nawashukuru sana Wakenya. Kadhalika, naishukuru tume ya uchaguzi kwa kazi nzuri waliyoifanya," amesema.
"Nawapongeza wote walioshinda, na kwa walioshindwa pia tutaishi kupambana siku nyingine."
Kwa upinzani amesema: "Sisi si maadui, ni raia wa nchi moja. Kila shindano, kutakuwa na washindi na wanaoshindwa, lakini tutasalia kuwa Wakenya. Nawapa moyo wa ushirikiano, twafaa kuungana pamoja. Wakenya wanataka sisi tufaulu.
"Sana kwa Raila Odinga, namuomba yeye, wafuasi wake, wote waliochaguliwa kupitia upinzani, tutafanya kazi pamoja, tutashirikiana, tutakua pamoja na kuendeleza nchi pamoja.
"Kwa Wakenya wenzangu, uchaguzi huja na kuondoka lakini Kenya itaendelea kuwepo, tukumbuke daima kwamba sisi ni ndugu na dada. Jirani yako bado ni jirani yako. Tuendelee kudumisha amani. Hakuna haja ya fujo, sisi wanasiasa pia huja na kuondoka. Lakini jirani yako atabaki."
Post a Comment