ad

ad

Okwi: Kwa Pasi za Niyonzima, Wanakufa Mapema



KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi amefunguka kuwa kitendo cha timu yao kukamilika kila idara huku ikiwa na wachezaji wengi wenye uwezo kama Haruna Niyonzima, hawana wasiwasi wakikutana na timu yoyote ile hata iwe Yanga watamaliza mchezo mapema. 

Okwi ambaye amesajiliwa klabuni hapo hivi karibuni, amesema kuwa watakachokifanya katika kila mchezo ni kufunga mabao kadiri wawezavyo kutokana na Niyonzima kuwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho. Simba kwa sasa ipo kisiwani hapa ikiwa katika kambi ya maandalizi yake kuelekea katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga utakaopigwa Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar. 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Okwi alisema kuwa
uwepo wa mchezaji huyo ndani ya timu yao ni faraja kubwa kwa kuwa ana uwezo wa kupiga pasi za mwisho nzuri ambazo zitawafanya wafunge mabao ya kutosha msimu huu. “Kwangu ni kitu cha faraja kucheza timu moja na mchezaji kama Niyonzima kwa sababu kwanza anajua halafu ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho kitu ambacho naamini kitatuongezea uwezo wa kufunga mabao mengi msimu huu. “Naamini wapinzani tukikutana nao tutawafunga mapema tu kutokana na kikosi chetu kukamilika kila idara kwa maana kwamba kila mmoja wetu anatimiza majukumu yake ipasavyo,” alisema Okwi. 


Wakati huohuo, Kocha wa Simba, Joseph Omog amebadilisha mbinu za wachezaji wake na sasa wamekuwa wakifanya mazoezi ya kufunga kutoka umbali wa mita 20. Katika mazoezi ya jana yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Ngome uliopo Fuoni, Omog na msaidizi wake, Jackson Mayanja walitoa maelekezo kwa beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na kiraka Ally Shomary kupiga mipira ya krosi za juu wakitokea pembeni. 

Kisha waliwapanga wachezaji wote kutoka nusu ya uwanja  kwa umbali wa mita 20 wakiwa na mipira ambayo waliwataka wapige mashuti golini kulipokuwa na makipa watatu waliokuwa wakibadilisha kudaka ambao ni Aishi Manula, Said Mohamed ‘Nduda’ na Emmanuel Mseja. Baadaye walisogezwa hadi katika mstari wa eneo la 18 na kutakiwa kupiga mashuti makali, walitekeleza hilo kwa ustadi.

CHANZO: CHAMPIONI

No comments

Powered by Blogger.