Mtibwa Sugar Kuijipima Kwa Lipuli
Mtibwa Sugar inakwenda mkoani Iringa kesho Jumamosi tayari kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Lipuli utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Samora Iringa.
Timu hiyo inakwenda kwenye mchezo huo bila kipa wake namba moja Shaban Kado ambaye yupo Dar es Salaam akiendelea na matibabu ya mguu baada ya kuumia katika mchezo uliopita wa kirafiki dhidi ya Simba.
Msemaji wa Mtibwa Sugar,Thobias Kifaru alisema wamepata mwaliko kutoka kwa Lipuli ambao Jumapili wanazindua jezi zao watakazotumia kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi.
"Lipuli wameomba kucheza na sisi na tumeona ni nafasi nzuri kwa timu yetu kucheza mchezo huo kwa ajili ya maandalzi ya ligi ambayo karibu inaanza, hivyo utatusaidia kukijenga kikosi chetu.
"Wachezaji wote watasafiri kwenda Iringa isipokuwa kipa Shaban Kado na mshambuliaji Stamil Mbonde ambao wanaendelea na matibabu na tunawaombea warejee mapema kabla ya ligi kuanza," alisema Kifaru.
Mtibwa Sugar imeonekana kuwa itakuwa moja ya timu tishio msimu ujao kutokana na usajili iliofanya licha ya kuondokewa na wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza.
Timu hiyo imewasajili Shaban Kado,Riphat Hamis, Hassan Isihaka, Salum Kanoni, Kelvin Sabato, Hassan Dilunga, Hussei Iddi na Salum Ramadhani.
Mtibwa Sugar itafungua Ligi Kuu Bara Agosti 26 kwa kucheza na Stand United kwenye Uwanja wa Manungu Turiani, Morogoro.
Post a Comment