Chirwa Akutana na Rungu la TFF Mechi ya Simba
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF)
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemzuia kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mzambia Obrey Chirwa kucheza mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itakayopigwa keshokutwa Jumatano.Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema leo katika mkutano na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kwamba, Chirwa hawezi kucheza mchezo huo kwa sababu katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC alimsukuma refa mjini Mwanza.
“Chirwa atakukosa mchezo wa Jumatano dhidi ya Simba utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa saa 11:00 mjini Dar es Salaam kutokana na kesi inayomkabili ya kumsukuma mwamuzi aliyechezesha mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu dhidi ya Mbao FC,” alisema Alfred Lucas.
Lucas amesema mshambuliaji huyo aliyejiunga na Yanga msimu uliopita kutoka FC Platinum ya Zimbabwe, atalazimika kuendelea kuwa nje hadi hapo Kamati ya Masaa 72 itakapokutana na kutoa maamuzi dhidi yake.
Pamoja na Chirwa, ambaye hata hivyo ni majeruhi na hayupo kambini kisiwani Pemba, wengine watakaoukosa mchezo huo upande wa Yanga ni majeruhi ni kipa Beno Kakolanya na kiungo Goffrey Mwashiuya.
Lucas amewataja marefa watakaochezesha mechi hiyo kuwa ni Elly Sasii kutoka Dar es Salaam, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha na Hellen Mduma.
Viingilio katika mchezo huo ni Sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu, 10,000 viti vya Orange, 20,000 kwa VIP B na 25,000 kwa VIP A . Na Esther Msofe
Post a Comment