Bill Gates Akutana na Rais Magufuli, Amwaga Mabilioni Bongo!
Taasisi ya Bill and Mellinda Gates
imetenga Dola za Marekani Milioni 350 sawa na takribani Shilingi Bilioni
777.084 za Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika
sekta ya kilimo, afya na mifumo ya kielektroniki ya upatikanaji wa
taarifa.
Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo Bw.
Bill Gates amesema hayo leo tarehe 10 Agosti, 2017 Ikulu Jijini Dar es
Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Bw. Bill Gates amesema kama ambavyo
taasisi yake imeshirikiana na Tanzania kwa kiasi kikubwa katika
kuimarisha huduma za afya hapa nchini, fedha hizo zitaelekezwa katika
utekelezaji wa miradi zaidi ya afya ikiwemo kupunguza vifo vya uzazi,
kukabiliana na ugonjwa wa malaria, kuimarisha lishe na kukabiliana na
utapiamlo, zitaelekezwa katika sekta ya kilimo ambako zitasaidia
kuongeza uzalishaji wa mazao, kuzalisha mbegu bora na kuboresha ufugaji
utakaoongeza chakula na pia zitasaidia kuweka mifumo ya kisasa ya
upatikanaji wa taarifa.
Bw. Bill Gates ameelezea kufurahishwa
na maendeleo ya uchumi wa Tanzania pamoja na uongozi na msimamo wa Rais
Magufuli juu ya kutaka miradi hiyo ilete matokeo yenye manufaa, na
amesema atakuja Tanzania mara nyingi ili kuimarisha zaidi ushirikiano na
kufuatilia utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli
amemshukuru Bw. Bill Gates kwa mchango mkubwa unaotolewa na taasisi ya
Bill and Mellinda Gates katika miradi mbalimbali hapa nchini ikiwemo
fedha ambazo taasisi hiyo itazitoa katika kipindi cha miaka mitano
kuanzia sasa na amemhakikishia kuwa Serikali yake itahakikisha fedha
hizo zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Mazungumzo kati ya Mhe. Rais Magufuli
na Bw. Bill Gates yamehudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Ufugaji na uvuvi
Dkt. Charles Tizeba na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
Wakati huo huo, Mhe. Magufuli
amekutana na kufanya Mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini
Mhe. Dkt. Inmi Patterson ambaye amesema Marekani itatoa fedha za
nyongeza kiasi cha Dola Milioni 225 sawa na Shilingi Bilioni 499.500 za
Tanzania katika mwaka ujao kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo itakayogusa sekta za elimu, afya, lishe bora, utawala bora.
Mhe. Inmi Patterson amesema Marekani
imeongeza fedha hizo katika miradi inayotekelezwa hapa nchini kwa sababu
ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na Tanzania na itahakikisha
uhusiano na ushirikiano huu unaendelezwa na kukuzwa zaidi.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli
amemshukuru Mhe. Balozi Inmi Patterson kwa mchango mkubwa ambao Marekani
imekuwa ikiutoa kwa Tanzania na amemhakiki kuwa Serikali ya Awamu ya
Tano itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano wake na Marekani, na pia
amemuomba awahimize wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi wa
Marekani waje kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini kutokana na fursa
lukuki zilizopo.
Mhe. Rais Magufuli pia ameiomba
Marekani kusaidia kujenga hospitali kubwa ya kitaifa katika makao makuu
ya nchi Mkoani Dodoma ili kuongeza uwezo wa Mkoa huo kutoa huduma za
matibabu ikilinganishwa na ilivyo hizi sasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Agosti, 2017
Post a Comment