ad

ad

SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-08


 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
Ilikuwa ni mvua kubwa, ilishuka tena kwa kasi kubwa kiasi kwamba kila mmoja akadiriki kusema hakukuwa na mvua kubwa iliyowahi kunyesha kama ile. Radi ziliendelea kupiga, kila mmoja akaanza kuogopa.
Mzee Maliki alionekana kushtukia kitu, kila alipoiangalia mvua ile, haikuwa ya kawaida, ilionekana kuwa na chembechembe za uchawi hali iliyomfanya kugundua kwamba kazi ilikuwa imeanza hivyo hakutakiwa kupuuzia.
Abiria ndani ya basi waliogopa, wengine wakaanza kulalamika kwamba dereva alitakiwa kuliondoa gari mahali hapo haraka iwezekanavyo. Kwa mzee Hamisi, hakugundua kitu chochote kile, kwake, mvua ile ilionekana kuwa ya kawaida sana.
Mzee Maliki akarudi kule kulipokuwa na kiti chake na kisha kuchukua mkoba wake aliouacha, mzee Hamisi alishangaa, alijua vitu vilivyokuwa ndani ya mkoba ule vilikuwa nini, sasa kwa nini mzee huyo aliuchukua.
“Kuna nini?” aliuliza mzee Hamisi.
“Unadhani hii mvua ni ya kweli?”
“Ndiyo!”
“Hapana! Nahisi huyo mtu kashaanza kufanya kazi.”
Aliposema hivyo tu ikawa kama mzee Hamisi amefunguliwa macho, mvua ile iliyokuwa ikinyesha, haikuonekana kuwa ya kawaida kabisa, hivyo naye akajiandaa kwani tayari alijua kwamba muda wa mapambano ulikuwa umefika.
Mzee Hamisi akatoa tunguli zilizokuwa ndani ya mkoba wake, kila abiria akaonekana kuogopa, hawakujua mzee huyo alitaka kufanya nini. Hakutoa tunguli peke yake bali pia alichukua na usinga kisha kushuka garini na kuanza kuchezacheza huku akizunguka kwa staili ya mduara.
Kila mtu alibaki akimshangaa lakini wala hakuonekaa kujali, alichokifanya ni kuendelea vilevile. Katika hali ambayo kila mtu aliishangaa, mvua ikakatika ghafla huku ardhi ikiwa haijalowana hata mara moja. Watu wote wakapigwa na butwaa.
“Eeeeh!”
Huo ndiyo ulikuwa uchawi aliokuwa akiutumia Ramadhani, ulikuwa uchawi wa hali ya juu sana na uliotisha ambao ulihitaji nguvu ya ziada kuweza kuusimamisha. Baada ya hapo, akarudi ndani ya basi kwa ajili ya kuondoka lakini bado basi lile halikuweza kuondoka mahali hapo.
Hilo wala halikuwa tatizo, kwa sababu walikuwa wamekwishafika Segera, wakateremka kwa ajili ya kuchukua basi jingine ambalo lilikuwa likielekea Tanga ili wasiweze kukwamba njiani na wakati kutoka hapo mpaka Tanga wala hakukuwa mbali.
Walitulia kituoni wakisubiri basi. Ndugu yangu, uchawi upo na mtu anaweza akaroga sehemu yoyote unapokuwa. Kwa wale waliowahi kufika Segera watakuwa wanaelewa kwamba mahali hapo huwa hakukauki mabasi hata mara moja, kila siku na kila saa magari yanapita yakielekea Moshi, Dar au Tanga.
Lakini huwezi amini, siku hiyo watu hao walikaa zaidi ya masaa mawili, hakukuwa na basi lolote lile lililopita kuelekea Tanga. Hiyo wala haikuwa kawaida kabisa, walijaribu kuangalia huku na kule lakini hakukuwa na basi lolote hali iliyowafanya kutoka pale kituoni na kuwafuata watu waliokuwa wamekaa pembeni na kuwauliza.
“Samahanini?” alisema mzee Maliki.
“Bila samahani.”
“Mbona leo magari hayapiti hapa?”
“Magari ya kwenda wapi?”
“Tanga!”
“Unamaanisha mabasi?”
“Ndiyo!”
“Mmefika muda gani?”
“Tangu masaa mawili yaliyopita.”
“Eeeh! Sasa mabasi hayo yote yanayopita hamuyaoni au mnatufanyia kusudi wazee wetu?” aliuliza kijana mmoja, wote wakabaki wakiwashangaa wazee wale.
“Mabasi yanapita?”
“Ndiyo! Tangu lini umeona Segera ikakaukiwa na mabasi?” alihoji kijana mmoja.
Mpaka hapo wakajua kwamba tayari walichezewa mchezo hivyo mzee Maliki akaulizia choo kwani alisema alishikwa na haja. Akaonyeshewa choo cha kulipia na kwenda huko. Mbele yake tayari aliona kulikuwa na kazi kubwa sana ya kufanya hivyo pasipo kufanya kitu wangeweza kukesha barabarani.
Alichokifanya mara baada ya kufika chooni ni kuchukua usinga wake na tunguli lake, akasimama wima kuelekea upande wa kusini na kisha kuanza kuzungumza maneno fulani yaliyofanana na lugha ya Kiarabu, alipomaliza, akajipiga na ule usinga kifuani, miguuno na mabegani kisha kujipulizia unga fulani.
Alipomaliza, akatoka ndani ya choo kile, kitu ambacho kilimpa uhakika kwamba kweli walikuwa wamerogwa alianza kuyaona mabasi yakiwa mengi kituoni huku mengine yakiitia abiria kwamba yalikuwa na safari ya kwenda Tanga.
Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwake, akamwambia mzee Hamisi kwamba walipaswa kuendelea na safari kwani bado hawakuwa wamefika. Garini, mzee Hamisi alibaki akiuliza tu, hakuamini kama mambo yote hayo yaliyokuwa yametokea yangetokea siku hiyo.
Hapo ndipo alipoamini zaidi kwamba Ramadhani hakuwa mtu wa mchezo hata mara moja na alikuwa na uchawi uliokuwa na nguvu kuliko hata ule aliokuwa akimiliki yeye. Safarini, hawakutaka kupiga stori, kila mtu alikuwa anawaza lake kichwani, kwa mzee Hamisi, alikuwa akijifikiria ni kwa jinsi gani angeweza kummaliza Ramadhani ambaye alionekana kuwa moto wa kuotea mbali.
Kadiri alivyojifikiria, ndivyo alivyoingiwa na hofu moyoni hata kuona kwamba huyo mzee waliyekuwa wakimfuata, hakuwa kitu mbele ya Ramadhani.

Je, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.