SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-05
NYEMO CHILONGANI
ILIPOISHIA
“Ndiyo! Tunahitaji miguu pia, unajua hawa watu ni mali sana, nikipata viungo vyote, nitavuiuza kwa wenzangu wengine,” alisema mzee yule na hivyo kuanza kuikata miguu ya mtoto yule. Kila nilivyokuwa nikiangalia, mwili ulinisisimka mno. Hayo ndiyo maagizo aliyokuwa amepewa na mganga kwamba viungo vya albino vilikuwa vikihitajika kwa hali na mali.
ENDELEA NAYO...
Niliyoyaona, yalitosha kabisa, sikutaka kuendelea kuona zaidi kuhusu maisha ya mwanasiasa huyu bali kitu nilichokifahamu kwa wakati huo ni kwamba mwanasiasa huyo alikuwa mtu mbaya sana na hakutakiwa kupendwa hata mara moja.
Walimkata viungo vilivyobakia kitu kilichopelekea kifo cha yule mtoto, moyo wangu uliumia sana lakini sikuwa na jinsi, sikujua ni kwa jinsi gani ningeweza kumsaidia kwani nilichokuwa nikikiona pale hakikuwa kitu kilichokuwa kikitokea wakati huo, ni kama kilirekodiwa.
Nilimwambia Yusnath kwamba ninahitaji anitoe hapo na kama kulikuwa na mtu mwingine wa kumuona basi afanye hivyo, basi akanichukua na kunirudisha kulekule kuzimu, mtu ambaye alitaka kunionyeshea ambaye alikuwa mahali hapo ni mwanaume mmoja mwenye ndevu nyingi nyeupe, kwa kumwangalia usoni, hakuonekana kuwa mpole sana lakini inawezekana alikuwa mkali hasa wakati wa kuongea. Nilimwangalia mzee yule, hakuonekana kuwa mgeni machoni mwangu, kila nilipomwangalia, nilihisi kwamba niliwahi kumuona mahali fulani japokuwa sikupakumbuka.
“Huyu ni mtu mwenye heshima kubwa, unamfahamu?”
“Hapana! Ila sura yake si ngeni machoni mwangu.”
“Anaishi Manzese Midizini,” aliniambia Yusnath.
Hapo ndipo nilipata kumbukumbu juu ya mtu huyu aliyekuwa amesimama mbele yangu. Niliweza kumgundua kwamba alikuwa Muislamu mkubwa ambaye alipewa cheo kikubwa na msikiti mmoja maeneo ya Manzese. Kama ilivyokuwa kwa mchungaji yule aliyepita, hata huyu shekhe naye alikuwa kule kuzimu.
Nilihuzunika sana, viongozi hawa wa dini hizi mbili walipewa majukumu makubwa ya kuwafanya watu kwenda peponi lakini mwisho wa siku, nao walikuwa kule kuzimu wakiendelea kumuabudu yule shetani.
Mzee huyu, kila siku ya Ijumaa alisimama mbele ya waumini wa dini hiyo na kuwasisitizia watu kwamba walitakiwa kumswalia Mungu. Ndugu zangu, kila nilichokiona kule kuzimu kilinisikitisha sana na kuona kwamba dunia ilipokuwa ikielekea si pazuri kabisa.
Sikutaka kujali sana, nilimwambia Yusnath kwamba nilitaka kuangalia maisha ya mzee huyo kama nilivyoyaona maisha ya mchungaji na mwanasiasa yule, hapo ndipo aliponichukua na kunipeleka kule kulipokuwa na televisheni.
Huko, nilimuona mzee yule akiwa amesimama sehemu moja iliyokuwa na giza totoro, alikuwa amevalia kanzu yake kubwa na macho yake aliyapeleka juu huku akiongea maneno yasiyoeleweka. Nilijaribu kumwangalia mikononi nikagundua kwamba alikuwa na hirizi moja kubwa iliyofungwa na kitambaa chekundu.
Muda, ilikuwa ni saa nane na nusu usiku. Yusnath akaniambia kwamba alikuwa akijiandaa kwa ajili ya kwenda kuswalisha. Alikaa katika hali ile kwa dakika kadhaa, ghafla nikaanza kusikia sauti za miungurumo, ilifanana na miungurumo ya radi.
Huku nikiendelea kuangalia kila kitu kilichokuwa kikitokea, ghafla nikamuona mwanamke mmoja akija mbele yake. Alikuwa mwanamke mzuri sana, naweza kusema kwamba sikuwahi kumuona mwanamke mwenye sura nzuri kama aliyokuwa nayo huyo.
Alimsogelea mzee yule aliyekuwa ameyapeleka macho yake juu na kisha kumshika ndevu zake. Ghafla, nikaanza kuona vitu kama shotishoti vikiiingia mwilini mwake kupitia ndevu zake zile.
“Ndiyo nini ile?” niliuliza.
“Anaingiziwa nguvu ili aendee kuwapoteza watu wengi zaidi duniani,” alinijibu Yusnath.
Sikiliza ndugu yangu, nilipelekwa kuzimu kwa kuwa kulikuwa na baadhi ya vitu nilitakiwa kuonyeshwa, nilitaka kufahamu mengi sana hivyo akaanza kuniambia mambo mengine kuhusu huyu mzee.
Heshima kubwa aliyokuwa nayo duniani ilionekana si lolote lile, alikuwa akisifiwa kutokana na ukarimu wake mkubwa lakini ukweli ni kwamba huyu mzee hakuwa lolote lile. Watu wengi walimheshimu, walimuita katika sherehe za Maulidi mbalimbali huku akipewa sifa kubwa lakini mzee huyo hakuwa kama watu walivyomfikiria.
Alikuwa mtu hatari sana ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kuviua vyuo vya madrasa vingi kama moja ya njia zake za kuweza kusimamisha kazi zao.
Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake ambayo aliifanya mara kwa mara. Vyuo hivyo viliongezeka lakini hakukuwa na maendeleo yoyote yale. Ukiachana na hivyo, kulikuwa na misikiti mingi ambayo ilikuwa na kusudio la kuendelea zaidi lakini shehe huyu alikuwa na kazi moja ya kuhakikisha misikiti haikui zaidi.
Alisababisha roho chafu kwa watu wengine misikitini, unapoona watu wanagombana wenyewe kwa wenyewe, ilikuwa ni kazi ya huyu mtu. Hapo ndipo nilipoamini kwamba shetani alikuwa bize kuhakikisha kwamba kila kitu kinaokwenda sawa kwa upande wake.
Migogoro mingi, majivuno na vitu vingine misikitini vilisababishwa na huyu mzee. Fedha zake zilitumika kujenga matabaka na kufanya vitu vingine.
Alipomaliza kupewa nguvu na mwanamke yule mrembo, nikamuona mzee yule akiondoka mahali hapo, kuja kuonyeshwa, nilimuona akiwa amesimama katika uwanja mmoja mkubwa wa wazi, ulikuwa ni uwanja wa mpira wa miguu lakini sikujua ulikuwa maeneo gani.
Mzee yule alisimama akiwa mtupu huku mkononi akiwa na tunguli moja kubwa iliyofungwa kitambaa chekundu. Alikuwa akizungumza maneno ya ajabuajabu, mbali na ule mkono aliokuwa ameshika tunguli, mkono mwingine ulikuwa umeshika kuku mwekundu ambaye akamuweka chini kuanza kumchinja.
“Kwa nini anachinja kuku mahali hapa? Naye anahitaji kunywa damu?” nilimuuliza Yusnath.
“Hapana.”
“Sasa kwa nini anafanya hivyo?”
“Anatafuta nguvu ya ziada ya kusonga mbele.”
“Sasa kupitia kuku!”
“Ngoja nikwambie kitu, hakuna kitu chenye nguvu duniani kama kutoa kafara ya damu. Kitu kinapowekwa kwa kutumia damu huwa na nguvu sana. Mtu anapotaka kuua kwa kutumia damu, kazi hufanyika kwa haraka sana, mtu anapotaka mafanikio kwa kutumia damu, hufanyika kwa haraka zaidi ya kitu chochote kile,” aliniambia Yusnath.
Niliwahi kusikia hilo kipindi cha nyuma kwamba kafara ya damu huwa na nguvu na hata Yusnath alivyokuwa akiniambia, nilikubaliana naye kwa asilimia mia moja kwamba huo ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe.
Mbali na hayo aliyokuwa akiyafanya, mzee huyu alikuwa mfuga majini nyumbani kwake. Mambo mengi aliyokuwa akiyafanya, alielekezwa na majini ambayo yalikuwa ndani ya nyumba yake.
Hakuwa mzee wa kuchezewa, alichokifanya Yusnath alitaka kunionyeshea roho mbaya ya huyu mzee. Nilimuona akiwa amesimama nje ya nyumba yake, alionekana kuangalia kitu ambacho wala sikukiona, uso wake ulikunjwa kwa hasira na hakutoa tabasamu hata mara moja.
Sikujua aliangalia nini lakini alionekana kuchukizwa na kitu fulani hivi. Huku nikimwangalia kwa makini, ghafla nikamuona mwanaume mmoja akija kwa kasi kule alipokuwa, alionekana kukasirika sana. Kijana huyo alikuwa na panga mkononi.
“Wewe mzee nitakuua,” alisema kijana huyo huku akisimama na akionekana kuwa na hasira mno. Kila alipokuwa akiongea, alimnyooshea panga lile.
“Na wewe nitakuua, tena kuwa makini kijana,” alisema mzee yule, hakuonekana kuogopa kitu chochote kile.
Kwa kuwa walikuwa wakiongea kwa sauti kubwa, watu waliokuwa pembeni waliposikia wakaanza kusogea kule walipokuwa wale watu na hatimaye vita vya maneno kuanza kuzuka mahali hapo, kila mtu aliyekuwa akimwambia mwenzake, walipeana vitisho vya kuua tu pasipo kujua tatizo lolote lile. Ghafla mzee yule akazidi kupandwa na hasira, nikajua kuna kitu kingetokea mahali hapo.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho usiku hapahapa.
Post a Comment