ad

ad

SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-04



SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-04
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
Uchawi upo ndugu yangu, tena umejaa sana katika nyumba za ibada. Kwa kile nilichokiona kwa mchungaji yule kiliyafumbua macho yangu na kuona kwamba hakukuwa na mtu aliyetakiwa kuaminika katika dunia hii.
Niliyoyaona yalitosha sana na hivyo kumwambia Yusnath kwamba alitakiwa kunitoa mahali pale na kunipeleka kule tulipotoka ili niweze kuwaona watu wengine, hilo halikuwa tatizo, akaniambia nifumbe macho, nikafanya hivyo na nilipofumbua tu, tayari tulikuwa tumefika.
Kwenye kundi lile la watu waliokuwa wamepiga magoti akiwemo mchungaji yule aliyependa kujiita mtume, kulikuwa na mtu mwingine ambaye nilimfahamu sana, alikuwa mwanasiasa mkubwa ambaye alipendwa na watu wengi.
Nilimwangalia, sikuamini kama na yeye alikuwa mahali pale, uso wangu ulionyesha kutokukubaliana na kile nilichokuwa nikikiona hivyo nikamuuliza Yusnath kama yule niliyekuwa nikimuona ndiye yule niliyekuwa nikimfahamu au macho yangu yalichanganya? Akaniambia ndiye mwenyewe.
Huyu alikuwa mwanasiasa mmoja mkubwa anayejulikana kwa jina la Abuzael John. Alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakitikisa sana Tanzania kutokana na umahiri wake katika kuteka akili za watu mara anaposimama jukwaani na kuzungumza.
Huyu naye alikuwa kule kuzimu akimuabudu shetani kitu kilichonishangaza sana. Yusnath alijua jinsi nilivyochanganyikiwa mara baada ya kumuona mtu huyo mahali hapo, hivyo alivyotaka kukifanya ni kunionyeshea maisha ya huyo mtu.
“Nataka nikuonyeshee maisha ya huyu mwanasiasa,” aliniambia.
“Sawa, hakuna tatizo.”
Kama kawaida akaniambia nifumbe macho, nilipofumbua baada ya sekunde kadhaa, tulitokea katika ule mlima wa kutisha ambapo mbele yetu kulikuwa na televisheni kubwa, ikawashwa na kuanza kumuona Abuzael akiwa ofisini kwake.
“Unataka kuona nini?” aliniuliza Yusnath.
“Nione jinsi anavyofanya kazi zake za kishirikina,” nilimjibu.
“Hakuna tatizo. Subiri.”
Yusnath akayafumba macho, sikujua alikuwa akifanya nini kwani alikaa kimya kwa muda fulani kisha kuyafumbua macho yake, nilipoyapeleka macho yangu katika televisheni ile, nikaona Abuzael akiwa sehemu moja iliyokuwa na msitu mnene sana.
Hapohapo Yusnath akanichukua na kuwa kule alipokuwa mwanasiasa yule yaani kila kitu alichokuwa akikifanya ni kama nilikuwa pembeni yake. Nilimuona akitembea huku akionekana kuwa na mawazo mno, alionekana kutokuwa na furaha hata mara moja.
Alikuwa akitembea kwa mwendo wa taratibu sana, alipokuwa akielekea, sikuwa nikipafahamu. Alizidi kupiga hatua mpaka katika kijumba fulani kidogo, kilikuwa kimetengenezwa kwa udongo na nje ya nyumba ile kulikuwa na fimbo kubwa iliyokuwa imesimikwa.
Alichokifanya Abuzael ni kugeuka nyuma, akavua suruali yake na kuyaacha makalio nje kisha kuingia ndani ya nyumba ile kinyumenyume. Mpaka hapo nikapata jibu kwamba pale alipokuwa kulikuwa kwa mganga, hivyo na mimi nikaingia huku nikitaka kujua alikwenda kufanya nini.
Kilio chake kikubwa kwa mganga yule kilikuwa ni kupata ubunge Aliongea huku akilalamika kwamba hakuwa akipendwa na watu wa jimboni kwake, wengi walimchukia na kumuahidi kwamba iwe isiwe asingeweza kurudi tena bungeni, yaani kipindi kile cha karibia na uchaguzi ndiyo ungekuwa wakati wake wa mwisho kuingia bungeni kule.
Alionekana kuhitaji sana msaada kwani hata uongeaji wake ulionyesha hilo. Mganga yule alibaki akimwangalia tu, kwa mtazamo alioutumia kipindi kile, ulionyesha kumuonea huruma mno.
“Ninataka ulete mkono wa albino,” alisema mganga yule huku akimkazia macho.
“Unasemaje?”
“Nadhani umenisikia, ukifanikiwa, utapata ubunge,” alisema mganga yule.
Abuzael alionekana kuwa na mawazo mno, hitaji alilopewa lilionekana kubwa sana lakini hakuwa na jinsi, alitakiwa kufanya kama alivyoambiwa afanye. Alionekana kumuamini sana mganga yule, nahisi ndiye aliyekuwa akimfanyia kazi zake katika kipindi alichokuwa akigombania kila mwaka na ndiyo maana alidumu sana katika ngazi ya ubunge.
Baada ya kuambiwa hivyo, mganga akamwambia kwamba ainuke na amfuate kule alipotaka kwenda, akamchukua na kuelekea naye porini zaidi. Walitembea huku kila mmoja akiwa kimya, kwa Abuzael alionekana kuwa mwingi wa mawazo, bado kichwa chake kilikuwa kikifikiria ni kwa namna gani angeweza kupata nafasi ile ambayo alikuwa akiililia kila siku.
Walitembea mpaka walipofika katika mti mmoja mkubwa. Katika mti ule, kulikuwa na tunguli nne zilizokuwa zimefungwa vitambaa vyekundu huku kukiwa na kitambaa kikubwa kilichokuwa na rangi nyeusi, kilifanana na kaniki.
“Subiri tuite nguvu zaidi ili upewe dawa ya kufanya kutokugundulika,” alimwambia mganga yule na kuanza kuzungumza maneno yasiyoeleweka.
Katika kila kitu kilichokuwa kikiendelea, niligundua kwamba watu walikuwa radhi kufanya jambo lolote lile lakini mwisho wa siku wafanikiwe maishani mwao. Mbunge huyu alionekana kuwa na uchu wa madaraka, hakutaka kuwa mwananchi wa kawaida.
Alichekwa sana jimboni kwake, watu walisema hafai hata kidogo hivyo kuamua kumfuata mganga huyo aliyempa sharti kubwa ambalo kwangu lilionekana kuwa kubwa ila kwake, halikuwa kubwa sana. Aliendelea kubaki kimya huku mganga yule kiendelea kuzungumza maneno yasiyoeleweka, ghafla nikaanza kuona moshi mkubwa na mzito ukifuka kutoka katika kitambaa kile. Nikaogopa.
*****
Sikujua ni kitu gani kilikuwa kinaendelea mahali pale kwani kufuka moshi kwa kitambaa kile kulizidi kuniongezea hofu zaidi. Niliendelea kumwangalia mzee yule huku macho yangu wakati mwingine yakikiangalia kitambaa kile.
Hapohapo huku moshi ukiendelea kufuka, ghafla nikaona kitu kama sura za watu zikitokea katika kitambaa kile. Mganga yule aliendelea kuzungumza maneno yasiyoeleweka na baada ya dakika chache sana, nikaona kitu kama kisu kikitokea chini ya mti ule mkubwa, kilikuwa kisu chenye makali pande zote na kilifungwa kwa kitambaa cheusi.
“Chukua hicho kisu,” alisema na hivyo mzee yule kuchukua kisu kile.
“Unachotakiwa ni kutumia kukatia viungo vya albino kwa kisu hiki,” alimwambia.
“Ooppss...!”
“Pia nitakupa dawa ambayo utawaambia watu wote watakaohusika kuwateka albino wasionekana kirahisi, yaani wawe wanapoteapotea machoni mwa watu. Na kazi yote itakayofanyika, ni lazima uwepo,” alisema mganga yule.
Mzee yule ambaye alikuwa mwanasiasa akapewa maelekezo yote ambayo alitakiwa kufanya mara baada ya kutoka mahali pale. Nilibaki nikimwangalia, watu walimchukulia kuwa mtu mpole na mara nyingi vyombo vya habari vilikuwa vikimpamba kwamba tangu nchi ipate uhuru hakukuwa na mtu aliyekuwa mpole bungeni kama yeye.
Nyuma ya pazia mzee huyo alikuwa mbaya mno, ilikuwa ni afadhali kumuamini tapeli kwa kumpa fedha zako akufikishie nyumbani lakini si kumwamini mzee huyu. Mara baada ya kukabidhiwa kila kitu, akaondoka mahali hapo.
Hatukuishia hapo, Yusnath akaanza kunionyeshea mambo mengine ya huyu mzee, tayari alikuwa amewaita vijana wake na kuwapa maagizo kwamba alikuwa akihitajika albino kwa ajili ya kumkata kiungo chochote kwa ajili ya kazi maalumu hivyo vijana wale wakaondoka kwa ajili ya kufanya kazi.
Ikaonyesha upande mwingine kwamba tayari vijana wale walikuwa mitaani, walikuwa katika mishemishe yao ya kumvizia mtoto mmoja wa kiukme ambaye alikuwa albino kwa ajili ya kufanya kile walichokuwa wameagizwa kukifanya.
Walikuwa wakijipitisha sana katika nyumba aliyokuwa akiishi albino huyo mtoto, baada ya dakika kadhaa alipotoka nje, wakajipaka unga maalumu ambao walipewa na yule mzee na kisha mmoja wao kumfuata kijana yule.
“We mtoto njoo,” alisema jamaa mmoja.
“Shikamoo kaka,” alisalimia mtoto yule.
“Marahabaaa....hujambo?”
“Sijambo.”
“Hebu twende huku,” alisema mwanaume yule.
Ndugu yangu, kila kitu kilichokuwa kikitokea nilikuwa nakifuatilia kwa macho yangu. Ule unga ambao alikuwa ameupaka kijana yule na wenzake ulikuwa na mvuto fulani wa kichawi ambapo hata mtu gani angeambiwa amfuate, asingeweza kukataa.
Mbali na hivyo, hata nyie watu mliokaa pembeni mlipokuwa mkimuona mtu huyo akiondoka na mtoto wala msingeshtukia kitu chochote kile, yaani mngechukulia kawaida sana.
Walimchukua mtoto yule na kuanza kuondoka naye. Hakuonekana kuwa na wasiwasi hata kidogo, uchawi aliokuwa amefanyiwa ulimfanya kuwaona watu wote kuwa ndugu zake kama walivyokuwa watu wengine, hivyo akaanza kutangulizana nao.
Walikwenda mpaka kwenye moja ya magari waliyokuja nayo na kuondoka naye. Moyoni nilihuzunika sana lakini Yusnath akaniambia kwamba nisihuzunike kwani kama ningefanya hivyo basi asingeendelea kunionyeshea mambo mengi zaidi.
“Usihuzunike...” aliniambia.
“Sasa nifanye nini kama naumia?”
“Fanya vyovyote lakini usihuzunike, kuna mengi nitakuonyeshea,” aliniambia Yusnath.
Kabla ya kuona kile kilichokuwa kikitokea mara albino walipokuwa wakichukuliwa, nilikuwa nawalalamikia polisi kwamba ilikuwaje mpaka hao watu wasikamatwe? Siku hiyo ndiyo nikagundua kwamba ushirikina unatumika sana.
Waliondoka na yule mtoto mpaka katika mkoa aliokuwa akitokea yule mzee na huko ndipo walipomwambia kwamba mzigo aliokuwa akiutaka tayari ulikuwa umekwishaletwa mahali hapo.
“Hakuna cha zaidi, fanyeni kazi,” alisema.
“Lakini na wewe si utakuwepo au?”
‘Ndiyo! Ni lazima nishuhudie,” alisema na kisha kuelekea huko.
Ndugu yangu, naweza kukwambia kwamba katika dunia hii tuna watu wenye roho mbaya mno. Madaraka yanatafutwa kwa nguvu sana, watu wanauawa kinyama kwa sababu ya fedha na vyeo. Ninachokuhadithia hapa, si kwamba nimeahadithiwa bali ninakwambia kile kitu kilichokuwa kikitokea na nilikishuhudia kwa macho yangu.
Mpaka katika kipindi hicho, tayari niliwaona watu wawili, mchungaji na mwanasiasa. Yusnath aliniambia kulikuwa na watu wa aina mbalimbali ambao duniani waliheshimika sana, hivyo sikutakiwa kuwa na haraka kwani angeniambia mmoja baada ya mwingine.
Baada ya kwenda kule alipokuwa yule mtoto, wakaanza kumkata mkono kitu kilichousisimua sana mwili wangu. Mtoto yule ambaye alifungwa kitambaa machoni kwa ajili ya kutomuona mzee yule aliyekuwa akijulikana sana, alikuwa akilia lakini hakukuwa na mtu aliyejali chochote kile, walichokuwa wakikitaka ni kukamilisha kazi zao.
Niliyashuhudia yote hayo kwa macho yangu mawili na wala sikuhadithiwa. Baada ya kuukata mkono ule huku damu zikiendelea kumtoka huku akilia kwa maumivu makali mno, wakamuacha kwanza apumzike.
“Kuna chochote kinahitajika?” aliuliza kijana mmoja.
“Ndiyo! Tunahitaji miguu pia, unajua hawa watu ni mali sana, nikipata viungo vyote, nitavuiuza kwa wenzangu wengine,” alisema mzee yule na hivyo kuanza kuikata miguu ya mtoto yule. Kila nilivyokuwa nikiangalia, mwili ulinisismka mno. Hayo ndiyo maagizo aliyokuwa amepewa na mganga kwamba viungo vya albino vilikuwa vikihitajika kwa hali na mali.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu hapahapa.

Unaweza kushare kwa ajili ya marafiki zako pia.

No comments

Powered by Blogger.