Zari Mambo Ya Mitandao Waachie Mabinti
Kuna ile Zari White Party, ni moja ya matukio machache kubuniwa na mdada huyo na kufanikiwa, likifanyika pale Mlimani City, miaka michache iliyopita. Anajiamini, anajua anachofanya na kizuri zaidi, anajua kutumia fursa. Unapozungumzia juu ya wanawake jasiri ambao ungependa binti yako aige, huyu ni miongoni mwa mifano hai, maana ni watoto wachache wa kike ambao wanaweza kuingia ‘front’ kusaka mkwanja sawa na wanaume! Lakini kuna jambo ambalo dada yangu huyu amelifanya, ambalo kidogo naona haliko sawa.
Pamoja na msiba mzito ambao ameupata kwa mumewe wa zamani, Zari amefanya vitendo ambavyo haviendani na utamaduni wa kiasili wa wabantu, bila kujali ni wa nchi gani. Kwa kawaida, mtu anapopatwa na msiba mzito, kama wa kufiwa na mume, tena mzazi mwenzio wa watoto watatu, unapaswa, angalau kwa muda, kuonyesha majonzi, siyo tu kwa sura, bali hata matendo.
Lakini Zari, baada ya mzazi mwenzake kuzikwa, siku mbili baadaye, akaja kwenye mitandao ya kijamii, akatupia video iliyomuonyesha anacheza kwa furaha kana kwamba alikuwa ametoka shughulini. Ni kweli kwamba kwa muda wote wa kuhani msiba huwezi kuwa na sura ya majonzi, kuna wakati mfiwa anaweza kujikuta akicheka, kutegemea na kinachotokea, lakini siyo kukata mauno halafu bila hata kufikiri, unatupia mtandaoni!
Ni wazi kuwa hakuwa sawa na watu wa ukoo wa mumewe, kitu ambacho pia ni tatizo. Angalau angebakia Kampala hadi ile sisi tunasema 40 ifike, ndipo aondoke. Lakini kama hiyo haitoshi, ndani ya siku 15 tu, tangu amzike mwenzake, tayari ameshaanza kujirusha kwa kuonyesha picha akiwa swimming pool na mwanaume, khaa! Hii haikai sawa, hasa kwa binti ambaye wengi tulimchukulia kama mfano.
Inapotokea hivi, ni rahisi kujenga hisia kuwa mtu huyu hana majonzi, kwa sababu mtu uliyefiwa na mwenza wako, unawezaje kupata faraja kiasi hiki ndani ya muda mfupi? Kuna taabu gani kusubiri siku 40 zipite halafu maisha mengine yaendelee kama kawaida? Zari ni kama mfano tu, lakini wako wadada wengi pia hata hapa Bongo ambao hukosa utu baada ya waume zao kutangulia mbele ya haki. Kama mtu hana hofu kwa mzazi mwenziwe, vipi rafiki, ndugu na jamaa? Kuna haja ya Zari kujitazama upya kwa sababu vitendo ndivyo vinavyotafsiri tabia ya mtu!
(STORI: OJUKU ABRAHAM, IJUMAA, ZA CHEMBE LAZIMA UKAE)
Post a Comment