Video: Lowassa, Sumaye na Waliyoyasema Kwenye Msiba wa Ndesamburo Moshi Mjini
Kufuatia kifo cha mmoja wa waasisi wa Chadema, mzee Philemon Kiwelu Ndesamburo (82) na shughuli ya kuagwa kuhamishwa kutoka Uwanja wa Mashujaa hadi Kiwanja cha Majengo, jana mwili wake uliagwa na kuacha vilio na majonzi katika mji wa Moshi na kuacha historia.
Vilio vilisikika wakati mwili unapelekwa kwenye Uwanja wa Majengo ambapo misururu ya watu ilijipanga pande mbili za barabara wakati gari lililokuwa na mwili wa Ndesamburo likipita huku likiwa limezungukwa na walinzi wa chama pande zote na kufuatiwa na msururu mrefu wa magari.
Yapo madai kwamba jeneza lake lilitoka Kenya na liligharimu mamilioni ya fedha japokuwa hakukuwa na mtu aliyethibitisha thamani halisi. Jeneza hilo lilikuwa gumzo kutokana na ukweli kwamba, muonekano wake si wa kawaida, msalaba wake ulionekana kunakshiwa kwa aina fulani ya madini, hali iliyozusha minong’ono msibani hapo.
Kama ilivyo ada kwenye matukio mazito kama hayo, watu wa rika mbalimbali waliangua vilio wakati wa zoezi la kutoa heshima za mwisho kwa mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Moshi ambaye ni maarufu kwa jina la Ndesa Pesa walipofika uwanjani. Wanaye Ndohorio Ndesamburo na Lucy Owenya ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema, walionekana kuwa wenye huzuni kufuatia kuondokewa na baba yao aliyekuwa kipenzi cha watu wengi. Mwasisi mkongwe wa Chadema, Edwin Mtei naye alikuwepo kwenye shughuli hiyo ambapo alisema walisaidiana na marehemu kwa moyo mkunjufu kukikuza chama.
WABUNGE WA CHADEMA
Wabunge wa Chadema walikuwa wengi wakiongozwa na mwenyekiti wa chama wa taifa na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, ambaye katika Kiwanja cha Majengo alisema analaani vikali kitendo cha serikali kuhamisha shughuli za kuaga kutoka Kiwanja cha Mashujaa na kufanyika Uwanja wa Majengo. Baadhi ya waliokuwepo kwenye msiba huo ni Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Mbeya,na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
Wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa. Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa shughuli za mazishi akishirikiana na Mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa ambaye alisema kifo hicho ni pigo kubwa kwa chama chake.
Pia alikuwepo Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu na Meya wa Manispaa ya Moshi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Longuo, (Chadema), Raymond Mboya na madiwani wengi wa Chadema mkoani hapo ambao walionekana kuhuzunika, Mbunge Komu kwa niaba yao alisema mzee Ndesamburo hakuwa mlezi wa chama tu bali alikuwa mlezi wa watu wengi.
“Wanafunzi aliowasomesha ni wengi, shule alizofadhili ni nyingi na vijiji alivyovinufaisha ni vingi, hivyo kote huko wana majonzi na kifo chake,” alisema Mbunge Komu.
WABUNGE WA CCM Wabunge wa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), hawakuonekana wengi isipokuwa Ester Mmasi wa viti maalum.
GWAJIMA ATEMA CHECHE
Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima alitema cheche kwa kulaani kitendo cha kuyumbishwa kwa msiba huo kuhusiana na sehemu ya kuagia. Alimshutumu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwa kusababisha usumbufu na upotevu wa pesa kwani alidai ndiye aliyeamuru kuhamishwa sehemu ya kuagia.
“Huyu bwana hata kwenye msiba wa wanafunzi 32 wa Lucky Vinsent hakumpa nafasi Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuzungumza. Namuomba Rais Magufuli amuonye kiongozi huyu,” alisema Gwajima. Aliongeza kuwa anaamini tabia ya Gambo inatokana kuambukizwa na kiongozi mmoja wa mkoa na akasema kama rais hatawaangalia basi tabia hiyo ya kutenga wapinzani itaenea nchi nzima.
BULAYA ANENA Wakati jana akifungiwa kuhudhuria vikao vya bunge mpaka mwaka 2018, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya alihutubia waombolezaji kwa niaba ya wabunge naye alilaani kitendo cha serikali kuyumbisha msiba huo.
LOWASSA ALIZUSHA JAMBO Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa alizusha jambo mara tu alipoingia uwanjani, shangwe zililipuka huku waombolezaji wakinyoosha mikono na kuonesha alama ya V. Akizungumza katika shughuli hiyo alisema Ndesamburo alikuwa ni mtu wa watu na ameumia sana kumpoteza.
NAIBU SPIKA Juzi Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson alikwenda kuwapa pole wafiwa na alimsifu marehemu Ndesamburo kwa kusema alifanya kazi nzuri kwa taifa wakati mfumo wa vyama vingi unaingia nchini. Mzee Ndesamburo alizaliwa Februari 19, 1935. Mwaka 2000 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Moshi Mjini mpaka mwaka 2015 alipoamua kwa hiari yake kutogombea tena jimbo hilo.
Post a Comment