Mbowe Apata Pigo Tena Kutoka Serikalini
Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amezidi kukumbwa na matukio mbalimbali baada ya jana Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kung’oa mitambo ya umwagiliaji iliyopo katika shamba lake na kumtoza faini kwa kuendesha kilimo eneo lisiloruhusiwa.
NEMC imemtoza faini ya Tsh 18 milioni Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kosa la kuendesha shughuli za kilimo ndani ya eneo la mita 60 kutoka kilipo chanzo cha maji.
Akizungumzi tukio hilo jana, Mbowe ambaye yupo Dodoma ambapo vikao vya bunge la bajeti vinaendelea alisema kuwa, zoezi zima limeendeshwa kisiasa na hii kuthibitisha kuwa nchi yetu inaongozwa kwa chuki na husda.
Mbowe alisema kuwa walipopewa taarifa mara ya kwanza, walikata rufaa kwa waziri husika kwa sababu sheria inaruhusu hivyo hadi sasa walikuwa wakisubiria majibu ya rufaa hiyo. Baada ya tukio hilo, Mbowe alieleza kuwa atawasiliana na wanasheria wake ili kujua hatua zitakazofuata.
Zoezi hilo la kung’oa miundombinu kwenye shamba hilo la Kilimanjaro Veggies lilifanyika jana chini ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa na maofisa wa NEMC.
Shamba hilo la Mbowe liko katika Kijiji cha Nshara, Machame ambapo Januari 20 mwaka huu, DC Hai alifika shambani hapo na kusitisha shughuli zote za kilimo kutokana na eneo hilo kuwa ndani ya chanzo cha maji.
Kwa siku za hivi karibuni, Mbowe amekumbwa na matatizo kadhaa ambapo jengo ilimokuwa ofisi yake ya Bilicanas na Free Media lilivunjwa na kuamriwa kutoka, kisha siku chache baada alituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya, tuhuma ambazo alikanusha.
Post a Comment