ad

ad

Kazi imeanza Ajibu Kutua Yanga mara baada ya kurejea kutoka nchini Misri

 
STRAIKA wa Simba mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, Ibrahim Ajibu, muda wowote atavaa uzi wa Yanga, mara baada ya kurejea kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa nchini Misri walipoenda kuweka kambi.

Hii imekuja siku chache baada ya Simba kudaiwa kumalizana na Mganda Emmanuel Okwi kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili, hivyo Simba sasa imefikisha wachezaji watatu iliowasajili wengine wakiwa ni John Bocco na Aishi Manula kutoka Azam.


Lakini Yanga nayo imeanza kazi, na kama Simba wanaweka jembe, basi na Jangwani nao inawawekea majembe ya maana yatakayowasumbua msimu ujao.


Tayari kamati ya usajili ya Yanga inadaiwa imeshafanya mazungumzo na Ajibu kiasi cha kumalizana naye, hivyo anasubiriwa arejee tu kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa ili amwage wino.


Chanzo cha habari hii kutoka ndani ya Yanga kimeeleza kwamba, Ajibu ni miongoni mwa wachezaji wa kwanza kabisa kuhitajika Yanga na kwamba mazungumzo yameshakamilika, zaidi zilikuwa zinasubiriwa siku za kumaliza mkataba wake ambao umemalizika rasmi Juni Mosi, mwaka huu.


“Ajibu na Mkude walikuwa kwenye mawazo ya kamati ya usajili wa Yanga na utakumbuka hata kwenye dirisha ndogo la msimu uliopita, hawa wote walitakiwa kutua Yanga lakini ilishindikana kufuatia wote wawili kuwa na mkataba na Simba ambayo tayari imemalizika na muda muafaka wa kuingia Yanga umewadia, japo wataingia kwa zamu,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka kuweka wazi ada ya usajili ya Ajibu.


Kwa upande wake Ajibu ameweka bayana kwamba punde atakaporejea hapa nchini akiwa na kikosi cha Taifa Stars, ndiyo atazungumzia mustakabali wa maisha yake ya soka, ingawa amekiri anaweza kuondoka Simba.


Ajibu ameliambia gazeti hili kuwa mpaka sasa bado hajafikia maamuzi ya kusaini wapi kutokana na kuwaza mechi ya kusaka tiketi ya kucheza Michuano ya Afrika (Afcon) dhidi ya Lesotho ambayo itapigwa Juni 10, katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.


“Kwa sasa ndiyo kwanza mkataba umemalizika, nahitaji kupata muda wa kutafakari juu ya hatima yangu ndani ya Simba na timu nyingine ambazo zimekuwa zikinihitaji.


“Ila sijafanya maamuzi ya wapi ambapo nitaenda kucheza hadi nimalize majukumu ya timu ya taifa, Taifa Stars, na baada ya hapo sasa rasmi ndipo nitaanza mazugumzo ya kuangalia ni timu gani ambayo nitaichezea kwa msimu ujao,” alisema.

No comments

Powered by Blogger.