Kampuni za Simu Mtegoni, Rais Magufuli Aiagiza TCRA Kuzifuta Zisizojisajili DSE

Rais
 John Magufuli ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuta 
kampuni za simu za mkononi zote ambazo hazitaki kujiandikisha katika 
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Aidha,
 amezitaka kampuni mbalimbali kujisajili katika mfumo wa ukusanyaji kodi
 za serikali kwa njia ya kielektroniki, aliouzindua jijini Dar es Salaam
 jana, mfumo unaosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) na Mamlaka
 ya Mapato Tanzania (TRA). 
“Tulipitisha
 sheria kwamba makampuni ya simu yote lazima yasajiliwe kwenye soko la 
hisa la Dar es Salaam, wamesuasua weee, wamezunguka …TCRA msitoze faini,
 futeni hizo kampuni,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa faini ambayo imewekwa na TCRA ni ndogo, hivyo kampuni hizo haziogopi.
Alisema
 kituo hicho kilichoanza kazi Oktoba mwaka jana, mwitikio wa kujiunga 
sio mkubwa, ambapo ni kampuni tatu pekee ambazo zimejiunga na alihimiza 
zingine kujiunga. 
Rais
 Magufuli alisema kwa kutumia kituo hicho, makusanyo ya kodi hayatakuwa 
na malalamiko tofauti na huko awali kulikuwa na malalamiko kwa wakusanya
 kodi na pia walipa kodi wakidai kuongezewa viwango.
“Tulikuwa
 tukitumia makusanyo ya kodi ya mtu na mtu na huyo mtu inategemea 
uaminifu wake, wapo ambao sio waaminifu wanapokwenda kwa wateja 
wanawakadiria makadirio ya juu na pia walipakodi kudanganya 
wanachopata,” alisema Rais Magufuli. 
Rais
 Magufuli alisema mwarobaini wa malalamiko hayo ni mfumo huo, ambao ni 
mashine zinakokotoa na kwamba hakuna mwingilio wa mtu katika hesabu.
“Wengine wote ambao hamjajiunga mfanye hivyo kwa hiari, mlipa kodi na mkusanya kodi mnatakiwa kuishi kwa raha na upendo,”
 alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa kama wafanyabiashara hao 
wanataka mpaka sheria ibadilishwe ndipo watii agizo hilo, serikali 
inaweza kupeleka muswada kwa hati ya dharura. 
“Najua
 mnaweza kufafuta visababu kama mnataka mpaka tubadilishe sheria bado 
Bunge linaendelea kule, tunaweza kufanya mabadiliko,” alisema na 
kuziomba kampuni hizo kushirikiana na serikali, isionekane kwamba 
serikali haitaki kushirikiana na wawekezaji kwa kuanzisha mfumo huu.
Aidha,
 alisema serikali hii inawapenda wawekezaji ndio maana inawawekea 
mazingira bora ya biashara sambamba na ukusanyaji kodi ulio sahihi. 
“Niwaombe
 ndugu zangu, na hii nawaomba kutoka moyoni mwangu tunahitaji kodi, nchi
 zote zinalipa kodi, ni lazima kila mmoja alipe kodi awe anataka au 
hataki,” alisema. 
Rais
 Magufuli aliziomba kampuni za simu pamoja na kampuni nyingine, kuingia 
katika mfumo huo ili kuwe na usawa katika ukusanyaji wa kodi.
Alisema
 anachukia wawekezaji pamoja na ubinafsishaji wa mali za umma wa hovyo, 
ambao hauna faida kwa nchi ambapo alisema kuna zaidi ya kampuni 197 
zimekufa. 
“Naeleza
 yote haya ili muelewe serikali ninayoiongoza inataka nini, inataka 
kufanya biashara na wawekezaji ambao ni waaminifu, biashara yoyote 
lazima iwanufaishe na wenye nchi,” alisema.
Aidha,
 Rais Magufuli alizitaka wizara zote zisimamie kampuni kuingia katika 
mfumo huo, ambao utawasaidia pia katika biashara zao kujua mapato yao. 
“Hakuna
 mtu duniani anayependa kulipa kodi, hata enzi za Yesu, na walipa kodi 
katika enzi zote hawakupendwa, usitegemee wewe kamishna TRA, ZRA 
utapendwa, wewe kusanya tu,” alisema Rais Magufuli.
Alisema
 nchi inapoteza fedha nyingi kupitia mianya ya upotevu wa mapato, lakini
 serikali iliamua kujenga kituo hicho kwa lengo la kuhakikisha na 
kulinda usalama wa taifa na taasisi za serikali na kampuni binafsi 
pamoja na kuimarisha na kukuza sekta ya teknolojia ya habari na 
mawasiliano. 
“Kampuni
 ambazo zitatunza taarifa zao kwenye kituo hiki zitakuwa na uhakika wa 
usalama wa taarifa zao hata kama uharibifu wowote utatokea,” alisema.
Post a Comment