ad

ad

SI KITU BILA PENZI LAKO-22

 
NYEMO CHILONGANI
Kila siku Victoria alikuwa mtu wa kwenda kazini, kutokwenda kazini lilionekana kuwa suala gumu katika maisha yake. Kila siku alikuwa akipata usumbufu kutoka kwa wafanyakazi mpaka kwa bosi wake ambaye bado alikuwa akimlaghai kwa fedha alizokuwa nazo.
Victoria alionekana kuwa tofauti na wasichana wengine, ingawa katika kipindi hicho alikuwa na uhitaji mkubwa wa fedha lakini hakutaka kujirahisisha kwa ajili ya fedha. Bado alikuwa na msimamo mkali katika maisha yake, msimamo wa kutomkumkubalia mwanaume yeyote zaidi ya Patrick.
Patrick bado alikuwa kichwani mwake, siku zote alikuwa akimkumbuka kupita kawaida, majonzi ya kutokumuona Patrick ndio yalikuwa sehemu ya maisha yake. Hakujua ni kitu gani ambacho kiliendelea katika maisha ya Patrick mara baada ya kuondoka pale porini na kuelekea asipopafahamu.
Victoria alkuwa ametoka kazini huku akionekana kuchoka kupita kawaida, kazi ambazo alikuwa amezifanya kwa siku hiyo zilionekana kumchosha. Alionekana mpweke huku akitembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea nyumbani alipokuwa akiishi na nesi Getrude.
Watu zaidi ya mia moja walikuwa wamesimama nje ya nyumba yao kwa mtindo wa duara. Victoria akaonekana kushtuka kupita kawaida, akaanza kupiga hatua kuelekea kule ambako umati wa watu ulipokuwa umesimama. Kitu cha kwanza mara baada ya kuufikia umati ule, akaanza kupenya penya mpaka mbele kabisa.
Macho yake yakatua kwa nesi Getrude ambaye alikuwa amelala chini huku mapovu yakimtoka mdomoni. Victoria akaonekana kushtuka kupita kiasi, akapiga magoti chini na kumshika Getrude. Tayari macho yake ambayo yalikuwa makavu yakaanza kutoa machozi.
Victoria hakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea mahali hapo. Wasiwasi ukaanza kumshika, akayapaleka macho yake kwa watu ambao walikuwa wamesimama kuwazunguka, macho yake tu yalionyesha kwamba alikuwa akitaka kufahamu ni kitu gani ambacho kilitokea mahali hapo.
“Alianguka ghafla, nafikiri kama ana kifafa” Mwanaume mmoja alimwambia Victoria.
Victoria akapigwa na mshtuko, hakuwa na taarifa yoyote kama Getrude alikuwa na kifafa cha aina yoyote ile. Hakutaka kuyapuuzia maneno yale, akasaidiana na watu waliokuwa mahali pale na moja kwa moja kuanza kumpeleka hospitalini.
“Haitowezekana kumtibia mahali hapa. Alipoanguka, aliangukia uti wa mgongo, kwa vyovyote vile ni lazima asafirishwe na kupelekwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam” Dokta alimwambia.
Victoria akaonekana kuishiwa nguvu, maneno aliyoambiwa na dokta yalionekana kumsikitisha. Hakuwa na fedha za kutosha na hata nauli tu ya kumsafirisha Getrude kwenda Dar es Salaam pamoja nae hkuwa nayo kabisa. Akajiona kuwa na uhitaji wa kupata fedha.
“Sisi kama wafanyakazi wenzie hospitalini hapa, tutamsaidia fedha za matibabu. Cha msingi wewe tafuta fedha za nauli tu” Dokta alimwambia Victoria.
Victoria akajiona kushushiwa mzigo mkubwa, ingawa hakuwa na fedha za kutosha za kukata tiketi ya treni lakini akaona ahueni. Kitu alichokifanya ni kuondoka hospitalini hapo na moja kwa moja kuelekea kazini kwake. Lengo lake kubwa lilikuwa ni kuonana na bosi wake, Bwana Mayayu ambaye kila siku alikuwa akimtaka Victoria.
“Nitakusaidia Victoria...” Bwana Mayayu alimwambia Victoria huku akimwangalia kwa macho yaliyojaa mahaba.
Bosi Mayayu akasimama kutoka katika kiti chake na kisha kuanza kupiga hatua za taratibu zilizojaa mapozi kumfuata Victoria, kabla hajaongea kitu chochote kile, akaupeleka mkono wake begani kwa Victoria na kuanza kumpapasa papasa Victoria.
Victoria akaonekana kukasirika, akasimama na kumwangalia bosi Mayayu kwa macho yaliyojaa hasira. Mayayu akaachia tabasamu pana ambalo aliamini lingemlegeza kabisa Victoria. Victoria akageuka kwa lengo la kutoka ofisini mule, Bwana Mayuya akamshika mkono.
Victoria alipogeuka, akageuka na kofi zito ambalo lilimuingia hasa Bwana Mayuya ambaye akayumba. Victoria akaufungua mlango na kutoka nje ya ofisi ile. Bwana Mayuya akaonekana kukasirika kupita kiasi, kitendo cha kupigwa kofi na mtu kama Victoria ambaye alikuwa mfanyakazi wake aliyeishi kwa kutumia fedha zake kilionekan kuwa dharau katika maisha yake.
Akaanza kupiga hatua kumfuata secretari wake ambaye alikuwa amebaki na mshangao baada ya kumuona Victoria akiwa ametoka ofisini kwa bosi wao huku akioekana kuwa na hasira.
“Huyu mbuzi sitaki kumuona tena akija mahali hapa.....umesikia?” Bwana Mayuya alimwambia sekretari wake.
“Ndio bosi. Tatizo nini?”
“Nimekwambia asije...ebo...haunielewi?”
“Nimekuelewa” Secretari aliitikia.
Njia nzima Victoria alikuwa akilia, hakuamini kama kule ambako alitakiwa kupata msaada ilishindikana. Alipofika nyumbani, akaanza kuelekea katika nyumba za majirani zake na kisha kuanza kuwaomba msaada wa fedha za nauli.
Kutokana na kila mtu kujua kila kilichotokea, wakaamua kumsaidia kwa moyo mmoja. Victoria akapata kiasi cha shilingi elfu thelathini na tano ambacho alikiona kumfaa kwa kusafiri kutoa Tabora mpaka Dar es Salaam. Victoria hakutaka kuchelewa, siku iliyofuata akaanza safari kutoka Tabora kwenda Dar es Salaam.
******
Mawasiliano kati ya hospitali ya Nzega na Muhimbili yakafanyika kiasi ambacho wala haikuwa shida kwa Victoria. Alipofika katika stesheni ya Railways iliyokuwa jijini Dar es Salaam, gari la wagonjwa lilikuwa mahali pale likiwasubiri.
Victoria hakuonekana kuwa na fahamu, muda wote alikuwa kimya. Victoria hakuonekana kuwa na furaha kabisa, alijiona kupitia katika kipindi kigumu sana maishani mwake. Kila wakati aipokuwa akimwangalia Getrude, sala ya kimoyo moyo ilikuwa ikiendelea moyoni mwake.
Gari ile la wagonjwa lilifika katika hospitali ya Muhimbili baada ya dakika nne kutoka Railways. Moja kwa moja akateremshwa na kuwekwa juu ya machela ambayo ikaanza kusukumwa kuelekea katika jengo la hospitali ile.
Huduma ya kumuhudumia Getrude ikaanza mara moja. Kila kitu kilikuwa kimefika katika ofisi ya dokta mkuu juu ya hali ambayo alikuwa nayo Victoria. Akaruhusiwa kulala hospitalini hapo mpaka katika kipindi ambacho Getrude atapata nafuu na kuruhusiwa.
Siku ya kwanza ikapita, siku ya pili, ya tatu mpaka wiki, bado Getrude hakuwa amefumbua macho yake, alikuwa amelala katika usingizi wa kifo. Victoria bado alikuwa akiendelea kulala hospitalini pale huku dokta mkuu akitumia kiasi cha fedha katika kumnunulia chakula cha kila siku.
“Kuna nini? Mbona mnaonekana tofauti sana leo?” Victoria aliwauliza manesi ambao walionekana kuwa haraka haraka.
“Mmarekani amekuja. Yule Mtanzania aliyeshinda shindano la uchoraji” Nesi mmoja, Fatuma ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Victoria toka afike hapo, alimwambia.
“Mbona mimi simfahamu” Victoria alimwambia
“Utamuona tu”
“Sasa nyie mnaelekea wapi?”
“Nje. Tunakwenda kumpokea, si kila siku kumuona kwenye televisheni” Nesi Fatuma alisema na kuondoka.
Victoria alijikuta akibaki peke yake mahali pale alipokuwa amekaa benchini. Ukimya ndani ya hospitai ile ulikuwa mkubwa huku kwa mbali kelele za watu zikiwa zinasikika kwa nje. Victoria hakutaka kutoka nje kumuona mtu huyo ambaye hadi kufikia hatua hiyo, aliona mtu huyo kuwa maarufu ambaye kila mtu alitamani kumuona na hata kumgusa.
Victoria alibaki benchini huku akiangalia chini. Mawazo yake yalikuwa juu ya Getrude ambaye bado hakuwa na fahamu kabisa. Mara kelele zile zilizokuwa zikisikika nje zikaanza kuhamia ndani. Mtu huyo ambaye alikuwa amepokelewa na manesi pamoja na madaktari alikuwa ameingia ndani ya jengo lile. Kwa haraka haraka daktari mmoja akaanza kupiga hatua kumfuata Victoria pale alipokuwa amekaa benchini.
“Binti. Ungekwenda kidogo hapo nje...kuna kazi inaanyika mara moja” Dokta yule alimwambia Victoria ambaye akasimama na kuanza kuondoka kuelekea kule ambako watu wale walikuwa wamepitia.
Uso wake ulikuwa ukiangalia chini huku kwa mbali machozi yakianza kumlenga. Hakutarajiwa kama angeweza kutolewa mahali pale kwa ajili ya kumpisha mtu ambaye alikuwa ametoka nchini Marekani. Victoria akapishana na watu wale ambao walikuwa zaidi ya ishirini pamoja na waandishi wa habari.
Victoria alikuwa akipiga hatua za haraka haraka kuelekea nje huku uso wake ukiangalia chini, hakutaka kumwangalia mtu yeyote usoni kwa wakati huo kutokana na kuonekana kwamba alikuwa akilia. Aliendelea zaidi na zaidi kupiga hatua kuelekea nje, mara akashtuka baada ya kusikia akiitwa kwa nyuma.
“Victoria.....Victoria....Victoria...” Alisikia vilivyo akiitwa.
Mara ya kwanza Victoria alipuuza, aliendelea kupiga hatua kuelekea nje. Bado sauti ile ilikuwa ikiendela kumuita. Victoria akapigwa na mshangao, hakujua kama kulikuwa na mtu yeyote Dar es Salaam ambaye alikuwa akimfahamu zaidi ya baadhi ya madaktari waliokuwepo hospitalini pale.
Aliisikiliza vizuri sauti ile ambayo ilikuwa ikimuita, haikufanana na sauti ya daktari yeyote yule hospitalini pale lakini sauti ile wala haikuwa ngeni masikioni mwake, akajaribu kukumbuka mahali ambapo alikwishawahi kuisikia sauti ile. Victoria akashtuka kupita kawaida mara baada ya kuikumbuka sauti ile, mwili wake ukapigwa ganzi, kijasho chembamba kikaanza kumtoka.
Akasimama huku kwa mbali akionekana kutetemeka kupita kawaida. Akauinua uso wake. Kila alipotaka kugeuka nyuma kumuangalia muitaji, alisita kufanya hivyo japokuwa sauti ile alionekana kuikumbuka vlivyo ingawa miaka miwili ilikuwa imepita tangu aisikia.
“Ni mimi, Victoria. Naomba ugeuke nyuma mpenzi” Sauti ile ilisikika.
“Patrick........” Victoria alijisemea moyoni hata kabla hajageuka na kumuangalia muitaji.
******
Maisha ya Patrick yalikuwa hatarini, hakuonekana kumuaini mtu yeyote katika kipindi hicho. Kila wakati alikuwa akiishi kwa wasiwasi. Alimfahamu vilivyo muuaji yule ambaye alikuwa amefanya mauaji mengi kwa watu weusi. Alikuwa akimuogopa sana mtu huyo kuliko kitu chochote.
Aliamini kwamba huo haukuwa mwisho wake wa kumtafuta, alijua fika kwamba ni lazima agemtafuta tena. Maisha yake yalikuwa yakfanya kila kitu mara moja moja tu mpaka pale ambapo angerudi nchini Marekani na kuwaeleza Polisi juu ya mtu ambaye alikuwa amemteka nchini Ujerumani.
Baadhi ya vitu ambavyo alikuwa akivifanya hakuwa akififanya mara mbili mbili. Njia ambayo alikuwa akipita wakati anaondoka basi wakati wa kurudi alikuwa akipita njia nyingine. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake siku zote, hakutaka kuyabadilisha staili ya maisha yake mpaka pale ambapo mtu yule angetiwa nguvuni.
Gari ambalo alikuwa akilitumia katika kipindi ambacho alikuwa akiingia katika katika sehemu fulani, basi alikuwa akiondoka na gari jingine. Hayo ndio yalikuwa maisha yake kila siku, hakutaka kuyakatisha maisha yake hasa katika nchi ya kigeni.
“Siwezi kuingia katika gari lile” Patrick alimwambia Vanessa.
“Kwa nini?” Vanessa aliuliza.
“Haya ndio maisha yanguniliojiwekea katika maisha yangu ya sasa. Haukumbuki nilivyokuwa nikifanya nchini Marekani Vanessa?” Patrick alimuuliza Vanessa.
“Nakumbuka”
“Safi sana. Hayo ndio maisha yangu. Nitaingia ndani ya gari lenu” Patrick alimwambia Vanessa.
Kila mmoja alionekana kushangaa utaratibu ambao Patrick alikuwa amejiwekea juu ya maisha yake. Patrick pamoja na Vanessa wakaanza kupiga hatua kulifuata gari ambao alikuwa amepakizwa Vanessa katika kipindi ambacho walikuwa wameingia katika hospitali ile.
Mara mlio wa bomu ukasikika, gari lile ambalo alitakiwa kuingia Patrick lilikuwa limelipuka. Watu wakaanza kutawanyika huku wengine wakiita jina la Patrick kwa kudhani kwamba Patrick alikuwa amelipuliwa katika lile gari.
“Mungu wangu! Patrick! Umejuaje?”
“Kila siku Mungu yupo pamoja nami” Patrick alimwambia Vanessa.
Safari ya kuelekea Ikulu ikaanza mara moja ambako huko wakakaribishwa chakula cha usiku. Ilikuwa ni furaha kubwa kwa rais wa Misri Bwana Mahomoud kula chakula pamoja na Patrick ambaye alikuwa mtu maarufu sana duniani.
Siku iliyofuata, safari ya kuelekea nchini Tanzania ikaanza. Safari ya kuelekea nchini Tanzania haikuwa katika ratiba ila iliingia ghafla baada ya Patrick kutaka iwe hivyo. Tayari akaonekana kuwa na wasiwasi mkubwa. Alitamani kwanza afike nchini Tanzania hata kabla ya kuelekea katika nchi mbili zilizobakia.
Safari kutoka nchini Misri iliwachukua masaa manne, wakaanza kuingia katika nchi ya Tanzania. Watu wengi walikuwa wamesimama uwanja wa ndege. Ingawa taarifa zilikuwa zimefika kwa kuchelewa sana kuingia kwa Patrick nchini Tanzania lakini watu wakajitoa vilivyo, masaa sita ambayo walipewa kwa kujiandaa yalikuwa yametosha kabisa kwa wao kufika uwanja wa ndege kwa ajili ya kumpokea mtu wao, ndugu yao na mtoto wao, Patrick.
Patrick akayapeleka macho yake chini, fuaha kubwa ikamtawala, machozi yakaanza kumtoka, hakuamini kama kweli kwa wakati huo alikuwa akitarajiwa kutua katika ardhi ya nchi ya Tanzania, nchi ambayo alikuwa amezaliwa na kukulia.
Ndege ikatua na kuanza kutembea kwa mwendo fulani na kisha kusimama. Mlango ukafunguliwa. Patrick hakutaka kuwa wa mwisho kama ambavyo alifanya katika sehemu nyingine, alikuwa wa kwanza kufika mlangoni. Kelele za shangwe zikaanza kusikika mahali hapo, Patrick akaanza kupiga hatua kushuka ngazi huku akijifuta machozi ambayo yalikuwa yakimtoka.
Vanessa, Matilda na Simpson ndio ambao walikuwa wamefuatia kwa nyuma. Patrick akajiona akishuka ngazi taratibu, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua za haraka haraka mpaka alipofika chini ambako akapiga magoti chini.
Tayari shati lake ambalo alikuwa amelivaa lilikuwa limeloanishwa na machozi ambayo yalikuwa yakimtoka. Waandishi wa habari wakaanza kumpiga picha Patrick ambaye bado alikuwa akiendelea kulia mahali pale. Baada ya muda, akasimama na kuanza kumpa mkono Mheshimiwa Peter Charles, ambaye alikuwa Waziri wa Mkuu.
Watoto waliokuwa na maua wakafika mahali hapo na kumgawia Patrick maua ambayo walikuwa nayo mikononi. Muda wote Patrick alikuwa akionekana kuwa na furaha kupita kawaida..
Patrick pamoja na wakina Vanessa wakaingia ndani ya gari ambalo likaanza safari ya kuelekea katika jengo la uwanja wa Taifa ambako Watanzania zaidi ya elfu themanini walikuwa wamekusanyika wakimsubiri yeye. Patrick alikuwa akipunga mikono kwa Watanzania ambao walikuwa wamekusanyika barabarani.
Muda wote Patrick alikuwa akilia, kila alipokuwa akiliangalia jiji la Dar es Salaam alikuwa akizikumbuka siku zile ambazo alikuwa akiishi kwa Gibson.
Safari ile ikaishia katika eneo la uwanja wa ndege. Ulinzi ulikuwa mkubwa kwa kila mtu ambaye alitaka kumgusa patrick. Patrick na wenzake wakaanza kupiga hatua kuelekea ndani ya uwanja ule. Mara baada ya kuonekana tu, uwanja mzima ukaanza kupiga kelele za shangwe.
Patrick hakutakiwa kukaa zaidi ya dakika thelathini uwanjani hapo kitu ambacho kilimfanya kupelekwa mpaka katika jukwaa mbele kabisa na kuanza kuongea. Kitu cha kwanza ambacho alikuwa amekiongea mahali hapo ni kuhusu maisha yake.
Alieleza kila kitu ambacho kilitokea katika maisha yake. Kila mtu mahali pale alionekana kusikitika. Historia ya Patrick ilionekana kumgusa kila aliyekuwa akiisikiliza mahali pale.
“Wazazi wangu waliuawa kwa kuteketezwa na moto. Jambo hilo liliniuma na kila siku litaendelea kuniuma” Patrick alisema huku umati wote ukiwa umegubikwa na huzuni.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatano mahali hapa.

No comments

Powered by Blogger.