SI KITU BILA PENZI LAKO-18
NYEMO CHILONGANI
SI KITU BILA PENZI LAKO-18
Patrick alibaki ndani ya kile chumba huku akitetemeka, hakuamini kama angeweza kutoka ndani ya chumba kile sala. Picha halisi ya chumba kile bado ilikuwa ikimtisha kupita kiasi, muonekano wa damu ambazo zilikuwa zimeganda ukutani zilizidi kumuogopesha.
Baada ya dakika kadhaa, Bwana Khan akaingia ndani ya chumba kile huku akiwa katika kiti chake cha mataili. Uso wake ulionekana kuwa na hasira kupita kiasi. Kila alipokuwa akimwangalia Patrick ambaye alikuwa akitetemeka na ndivyo ambavyo hasira zake zilivyozidi kuongezeka zaidi na zaidi.
“Nimfanye nini huyu mbwa?” Bwana Khan aliuliza huku akionekana kukasirika zaidi.
“Chochote tu utakacho bosi”
Bwana Khan akamwangalia vizuri Patrick, hasira zaidi zikampanda. Hakutaka kumuon mtu yeyote aliyekuwa na ngozi nyeusi mbele yake, aliwachukia watu hao kuliko kitu chochote katika maisha yake. Kitu alichokifanya kwa wakati huo ni kuwaambia vijana wake wamchukue Patrick na kumpeleka katika kisiwa kilichokuwa na wanyama wakali cha Rugen kilichokuwa katika bahari ya Baltic.
Patrick akachukuliwa na kutolewa nje ambako akaingizwa garini na vijana watatu kuingia pamoja nae. Amri ambayo ilikuwa imetolewa ya kuuawa ilikuwa ikimuogopesha sana Patrick. Akaanza kukumbuka maisha yake ya nyuma, toka siku ya kwanza aliponusurika kuuawa mpaka siku hiyo.
Hakuamini hata siku moja kwamba alikuwa akiuawa katika nchi ya ugeni. Alibaki akilia tu. Kuuawa pasipo kumuona Victoria kwa mara nyingine kulionekana kumuumiza kupita kawaida. Moyo wake ukaanza kujuta kwa hatua yake ya kukubali kuelekea nchini Marekani ambako ndiko ambako matatizo yalipoazia.
Wakafika katika ufukwe wa bahari ya Baltic ambako wakakutana na walinzi kadhaa, wakawapa fedha kiasi kikubwa cha kutosha. Walinzi hawakuwa na jinsi, fedha zikaonekana kuwalevya kupita kawaida. Wakawaruhusu vijana wale wachukue boti na kisha kuanza kuelekea katika kisiwa cha Rugen ambacho hakuruhusiwa mtu yeyote kuingia humo kutokana kuwa na wanyama wakali.
Wala hawakuchukua dakika nyingi, wakafika katika kisiwa hicho ambacho kilikuwa na miti tu iliyotengeneza msitu mkubwa. Wakateremka na kuanza kumpeleka Patrick katikati ya kisiwa kile. Milio kadhaa ya wanyama ilikuwa ikisikika mahali hapo hali iliyowafanya kuweka vizuri bunduki zao.
Waichokifanya kwanza ni kuyararua mavazi ambayo alikuwa ameyavaa Patrick na kisha kumuacha kama alivyozaliwa. Walitaka kumuua kifo cha aibu ambacho angekikumbuka mpaka siku ambayo angesimama mbele ya hukumu.
Wakachomoa bunduki zao na kisha kumlaza chini. Patrick alikuwa akilia huku akijaribu kuomba msamaha. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alimuelewa, wakachukua bunduki zao na kisha kujiandaa kumfyaulia.
“Tunaanzia miguuni, tunaelekea kiunoni, tumboni mpaka kifuani” Waliambiana huku Patrick akizidi kulia.
*****
Taarifa za kutekwa kwa Patrick zilikuwa za siri sana lakini siri hiyo ikaonekana kuwa si siri tena hasa mara baada ya watu kuufahamu ukweli na kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea nchini Ujerumani. Magazeti ya nchini Marekani kama New York Times na magazeti mengine yalikuwa yametoa taarifa hiyo ambayo ilionekana kumtetemesha kila aliyekuwa akiisoma.
Wamarekani hawakuamini kile ambacho kilikuwa kimetokea nchini Ujerumani, kitendo cha kutekwa kwa Patrick kilionekana kuwa kitendo kilicholeta aibu kuliko tukio lolote lililowahi kutokea. Kila Mmarekani akaonekana kuchukia, hawakutaka kusikia kitu chochote kutoka katika Serikali ya Ujerumani zaidi ya kumtaka Patrick wao.
Wamarekani hawakutulia nchini kwao, muda wote walikuwa kwenye mishemishe za hapa na pale huku hata baadhi yao wakidiriki kuandamana huku mabango ambayo yalikuwa yakionyesha dharau kwa serikali ya Ujerumani yakiwa yameshikwa vizuri.
Waandishi wa habari hawakuwa mbali, kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea nchini Marekani kilikuwa kikirushwa moja kwa moja katika vituo mbalimbali nchini humo ambavyo vilirusha matangazo hayo katika nchi mbalimbali duniani.
Dunia ikaonekana kushtuka mara baada ya kuangalia habari ile, kitendo cha kutekwa kwa Patrick na kutokupatikana kilionekana kumshtua kila mtu. Kila mtu alikuwa akijiuliza juu ya Serikali ya Ujerumani, kwa nini hawakutaka kuhakikisha ulinzi kwa Patrick mpaka kutekwa na watu wasiojulikana?
Kila walipofikiria kwamba kulikuwa na mauaji ya kimya kimya ya watu waliokuwa na ngozi nyeusi, kila mtu alionekana kuogopa kwa kuona kwamba hata Patrick alikuwa ameingia katika mkumbo huo. Maneno mbalimbali yalikuwa yakiongelewa na Serikali mbalimbali duniani juu ya tukio hilo ambalo lilikuwa limetokea.
Waziri mkuu wa Ujerumani hakutaka kulifumbia macho suala hilo, kitu alichokifanya ni kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kuanza kuzungumzia suala hilo kwa kuahidi kwamba ndani ya masaa arobaini na nane, Patrick atakuwa amepatikana.
Msako ukaanza katika kila kona, kutekwa Patrick kilionekana kuwa kitendo kilichowafanya kudharaulika kupita kiasi, sekta yao ya ulinzi ikaanza kupondwa kupita kawaida. Nchi ya Ujerumani ikaonekana kuwa na ulinzi feki ambao wala haukutakiwa kuaminika hata mara moja.
Nchini Tanzania kulionekana kuwa balaa, watu zaidi ya elfu mbili walikuwa wakiandamana barabarani huku wakiwa na mabango mbalimbali. Nchi ya Ujerumani ikaonekana kupoteza uaminifu katika sekta yake ya ulinzi. Watanzania wakaanza kwenda katika ubalozi wa Ujerumani, walionekana kukasirika sana juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea.
*****
Mara baada ya kumaliza kila kitu moja kwa moja wakaanza kuelekea katika mghahawa ambako wakaagiza chai na kuanza kunywa. Watu mbalimbali walikuwa katika mgahawa huo wakipata chai ya asubuhi. Walikuwa wakiendelea kunywa chai huku wakiwa na mipango ya kutoka na kwenda katika mbuga ya wanyama Ambilobe ambayo ilikuwa upande wa kaskazini wa kisiwa hicho.
Muda wote Bwana Mayemba na Bi Anna walikuwa wakiangaliana huku kila mmoja akiojaribu kumuonyeshea mwenzake tabasamu pana. Bwana Mayemba akaonekana kutokuridhika, akaupitisha mkono wake kwa chini na kuushika mkono wa mkewe, Bi Anna hali iliyomafanya kutoa kicheko cha chini.
“This is bullshit. Everything changes, they always kill us, they dont love us anymore. I hate white people (Huu ni upumbavu. Kila kitu kimebadilika, kila siku wanatuua, hawatupendi kabisa. Ninawachukia watu weupe)” Mwanaume mmoja alisikika akisema kwa sauti kubwa katika mgahawa ule huku akiwa ameshika gazeti.
Watu wote waliokuwa ndani ya mgahawa ule wakageuka na kuanza kumwangalia mwanaume yule ambaye alionekana kukasirika kupita kawaida. Wazungu ambao walikuwa katika mgahawa ule wakaonekana kushtuka zaidi, hawakuamini kuwa maneno kama yae yangetoka kinywani mwa mtu yeyote kwa wakati huo.
Kila mtu akaanza kusogea katika meza ile ambayo alikuwa amekaa mwanaume yule ambaye alikuwa ameondoka. Macho yao yakakutana na picha ya Patrick huku maneno makubwa yaliyosomeka WILL HE BE KILED?(ATAUAWA?) huku picha ya Patrick ikiwa mbele kabisa ya gazeti lile.
Gazeti ile lilielezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea. Kila mtu ambaye alikuwa akiisoma habari ile alisikitika, hawakuamini kama Patrick yule ambaye alikuwa amejipatia umaarufu mkubwa katika uchoraji ndiye ambaye alikuwa ametekwa na muda wowote angeuawa.
Kila mtu alikuwa akiliangalia lile gazeti, wote walipomaliza kuliangalia, Bwana Mayemba akasimama na kuanza kupiga hatua kuelekea katika meza ile na kisha kulichukua gazeti lile na kurudi nalo mezani. Akaanza kuiangalia habari ile huku picha ya Patrick ikionekana vizuri katika ukurasa wa mbele.
Bwana Mayemba akaanza kuiangalia picha ile na habari ile ambayo ilikuwa imeandikwa, akatikisa kichwa chake upande wa kushoto na kulia, alionekana kusikitika. Bi Anna alikuwa akiendelea kunywa chai huku akimwangalia mume wake ambaye alionekana kuwa katika hali ya masikitiko.
“Wazungu watu wa ajabu sana. Wamemteka kijana huyu wa kiafrika. Inasemekana wanaweza kumuua” Bwana Mayemba alimwambia mkewe.
“Kijana yupi?” Bi Anna aliuliza huku akiendelea kunywa chai.
“Huyu kijana mchoraji. Kwani wewe hujawahi kusikia habari zake?” Bwana Mayemba aliuliza huku akiwa amelishikilia gazeti lile.
“Hapana”
“Huyu kijana ni Mtanzania aliyepelekwa nchini Marekani. Akawa anachora sana. Amebahatika kuiwakilisha nchi ya Marekani katika mashindano ya dunia. Alipofika nchini Ujerumani, akatekwa na watu wasiopenda ngozi nyeusi” Bwana Mayemba alielezea.
“Masikiniiiii...yaani bado ubaguzi wa rangi unaendelea?”
“Ndio. Anaonekana kuwa kijana mzuri sana. Anaitwa Patrick. Anaonekana kuwa Mtanzania halisi” Bwana mayemba alimwambia Bi Anna.
“Nimefurahi sana. Jina lake limenikumbusha marehemu mtoto wangu” Bi Anna alimwambia.
“Pole sana mke wangu. Ila amefanana sana na wewe. Yaani hadi jina lake la pili linafanana na jina la marehemu mume wako. Anaitwa Patrick Christopher” Bwana Mayemba alimwambia mkewe.
Bi Anna akaonekana kushtuka, mfanano ambao alikuwa amepewa juu yake na Patrick pamoja na mfanano wa jina la pili ukaonekana kumshtua. Akashikwa na shauku ya kutaka kuliangalia lile gazeti. Akanyoosha mkono na kulichukua lile gazeti kutoka mikononi mwa mumewe, akayapeleka macho yake katika picha ile.
Bi Anna akashtuka, mapigo yake ya moyo yakaanza kwenda kasi, hakuamini picha ile ambayo alikuwa akiiangalia mbele yake. Kijasho chembamba kikaanza kumtoka. Ilikuwa ni sura ya Patrick ambayo ilikuwa ikionekana katika gazeti lile, picha ya mtoto wake ambaye alipotezana nae muda mrefu uliopita.
Taarifa ile ambayo ilionekana katika gazeti lile ikaonekana kumtisha kupita kawaida, hakutarajia kama angeweza kuiona picha ya kijana wake sehemu yoyote ile kwani kitu alichokuwa akikijua ni kwamba alikuwa marehemu kwa wakati huo.
Machozi yakaanza kumlenga na baada ya muda yakaanza kumtoka na kuyaloanisha mashavu yake laini. Bwana Mayemba akaonekana kushtuka, hakujua sababu iliyomfanya mkewe mpenzi kuwa katika hali ile. Akamsogelea karibu.
“Kuna nini mke wangu?” Bwana Mayemba aliuliza.
“Mtoto...mtoto wangu...” Bi Anna alisema, hapo hapo akaanguka chini kama mzigo.
*****
Muungurumo wa boti iliyowashwa ikaonekana kuwashtua wapelelezi ambao walikuwa mahali hapo, ufukweni. Kwa haraka haraka wakaanza kupiga hatua kuelekea kule ambako muungurumo wa boti ile uliposikika. Walinzi wawili wa hoteli ya Hugzifrey walikuwa wamesimama wakiiangalia boti ile huku mikononi mwao wakiwa wameshika fedha ambazo walikuwa wamehongwa.
Mara baada ya walinzi wale kuwaona wapelelezi wale wakija huku wakiwa wamevalia suti nyeusi, wakaonekana kuogopa kwani walijua kwamba tabia yao ya kuwaruhusu watu kuingia katika bahari ile usiku ilikuwa imejulikana.
“wer sind diese? (Wale ni nani?)” Mpelelezi Taylor ambaye alikuwa akikifahamu sana Kijerumani aliwauliza walinzi wale.
“Wir wissen nicht. Sie kamen hierher und bat um unser Boot, wir gaben ihnen (Hatuwajui. Walikuja hapa na kutaka boti yetu, tukawapa)” Mlinzi alijibu huku akitetemeka.
Wapelelezi wale hawakutaka kuendelea kuuliza maswali zaidi, moja kwa moja wakaanza kuifuata boti nyingine ambayo ilikuwa mahali pale na kuingia. Walinzi walikuwa wakitetemeka kwa kujua kwamba watu wale walikuwa wametoka katika serikali ya Ujermani kutokana na kutowaona vizuri usoni.
Taylor na wenzake walikuwa wakiendesha boti kwa kasi kubwa, boti ile ambayo walikuwa wakiifuatilia walikuwa wakiiona kwa mbali sana. Waliendelea kuifuatilia zaidi na zaidi mpaka walipofika ufukweni katika kisiwa kile cha Rogen na kuteremka.
Sauti za wanyama wakali zilikuwa zikiendelea kusikika mahali hapo, wakaandaa silaha zao tayari kwa chochote kile ambacho kingeweza kutokea mahai hapo. Walizidi kwenda mbele zaidi huku lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana.
Hawakujua ni mahali gani watu wale walipokuwa. Hawakukata tamaa, bado waliendelea kusogea mbele zaidi na zaidi. Hawakuamini macho yao mara baada ya kufika katika eneo moja ambako wakakuta damu zikiwa zimetapakaa mahali hapo.
Wakaangalia katika eneo lile, nguo za Patick zilikuwa zipo chini huku damu zikiwa zimetapakaa katika nguo zile. Kila mmoja akaonekana kushtuka kupita kiasi. Kila walipokuwa wakiangalia katika kila upande, hakukuwa na mtu yeyote zaidi ya zile nguo za Patrick zilizokuwa na damu ambayo iliwafanya kuona kwamba Patrick alikuwa ameliwa na wanyama wakali.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu mahali hapahapa.
Usisahau kushare au kutag kwa ajili ya marafiki zako.
Post a Comment