ad

ad

SI KITU BILA PENZI LAKO-17

 
NYEMO CHILONGANI
SI KITU BILA PENZI LAKO-17

Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akimiliki utajiri mkubwa nchini Ujerumani kama alivyokuwa Bwana Khan Miloslovic ambaye alikuwa na asili ya Poland. Bwana Khan alikuwa akimiliki viwanda vingi vikubwa nchini Ujerumani, viwanda ambavyo vilikuwa vikitengeneza magari yaliyokuwa na thamani kubwa duniani.
Bwana Khan hakuonekana kuwa na wasiwasi na utajiri wake, kila siku fedha zilikuwa zikiingia katika akaunti yake ambazo zilimfanya kuwa tajiri wa ishirini kwa utajiri mkubwa. Kila mtu nchini Ujerumani alikuwa akimheshimu, Majumba yake makubwa na ya thamani yalikuwa yakilindwa na walinzi ambao walikuwa na bunduki muda wote.
Mzee huyu hakuonekana kuwa na furaha, muda mwingi alikuwa ni mtu wa majonzi, hali hii ilitokana na kupenda sana wanawake katika enzi za ujana wake. Alichukua wanawake mbalimbali ambao walikuwa wakizisujudia fedha zake. Msichana kwake hakuweza kukatiza, kila siku alikuwa akilala na wanawake tofauti tofauti mpaka pale ambapo alimpata msichana aliyeitwa Latifa ambaye alitokea nchini Ghana.
Latifa ndiye ambaye alimsababishia matatizo ya ulemavu ambayo alikuwa nayo baada ya kumgonga na gari katika kipindi ambacho walikuwa wamekorofishana.
Hatua ile ilimpelekea Bwana Khan kumuua Latifa kwa kumtumbukiza ndani ya pipa la asidi. Kuanzia kipindi hicho, Bwana Khan hakuonekana kuwapenda watu waliokuwa na ngozi nyeusi. Kila siku alikuwa akiwauwa watu hao kwa kuamini kwamba walikuwa na roho mbaya hata zaidi ya Latifa.
Watu wengi wenye ngozi nyeusi walikuwa wakiuawa nchini Ujerumani na miili yao kutupwa katika bahari Baltic. Matukio mbalimbali ya kuuawa watu waliokuwa na ngozi nyeusi yalikuwa yakiendelea kuongezeka nchini Ujerumani hali ambayo iliwapelekea watu kuandamana kwa kutaka watu ambao walikuwa wakihusika katika mauaji hayo kukamatwa na kupelekwa katika vyombo vya sheria.
Upelelezi ulikuwa ukizidi kuendelea kila siku lakini cha ajabu wale wapelelezi ambao walikuwa katika hata ya mwisho kukamilisha upelelezi walikuwa wakiuawa na miili yao kutupwa ndani ya bahari ya Baltic.
Serikali ya nchini Ujerumani ikaonekana kuchanganyikiwa, mauaji yale yalionekana kuwachanganya kupita kawaida. Watu ambao walikuwa wakiishi nchini Ujerumani wenye ngozi nyeusi walikuwa wakiishi kwa wasiwasi, mauaji yalikuwa yakiendelea kushamiri katika kila kona.
“Ich hasse schwarze Menschen (Nawachukia watu wenye ngozi nyeusi)” Hayo yalikuwa maneno ambayo yalikuwa yakitoka kwa Mjerumani mwenye roho mbaya, Bwana Khan.
Kitendo cha Patrick kuwa maarufu kilionekana kumuuzi kupita kawaida, hakuamini kama kuna mtu mweusi ambaye alistahili kuwa maarufu kupita kiasi, roho ya uuaji ikaanza kumuandama moyoni. Hakutaka kumuacha Patrick, ilikuwa ni lazima amuue.
Akaandaa watu wake ambao aliwatuma kwenda kumpokea Patrick katika uwanja wa ndege wa Hamburg na kisha kumpeleka katika mji wa Sassnitz kabla ya kumpeleka katika kisiwa kidogo cha Aland ambacho kilikuwa katika bahari hiyo.
Moja kwa moja vijana wake wakaanza kuelekea katika uwanja wa ndege wa Hamburg ambako baada ya kuwafahamu watu waliofika mahali hapo ambao walikuwa wamekuja kumpokea Patrick, wakawaweka chini ya ulinzi na kuwafungia katika gari lao walilokuja nalo na kisha wao kuelekea katika sehemu ya watu waliokuwa wakisubiri abiria waliokuwa wakishuka na ndege zilizokuwa zikiingia katika uwanja huo.
Saa moja kamili usiku, ndege ya kukodi ambayo alikuwa amepanda Patrick na wenzake ikaanza kuingia katika uwanja huo wa ndege. Kwa haraka haraka wakainuka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu ambayo wala hakukuwa na mtu na kisha kuanza kujipanga upya.
Wala hazikupita dakika nyingi, Patrick, Vanessa na Simon wakaanza kuonekana wakiingia katika sehemu ile. Kwa mwendo wa haraka haraka pasipo kupoteza muda wakaanza kuwafuata na kujitambulisha kwao.
“Ila kuna kitu inabidi kifanyike” Votz aliwaambia.
“Kitu gani?”
“Kuna hoteli mbili zimeandaliwa. Moja ni kwa ajili ya washiriki na moja kwa ajili ya waliomleta mahali hapa. Hii imefanyika hivi kwa ajili ya usalama zaidi” Votz aliwaambia.
“Hakuna shaka” Simon alisema.
Patrick akachukuliwa na kuingizwa ndani ya gari, ingawa kwa mbali alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi lakini upande mwingine wa moyo wake hakuonekana kuwa na wasiwasi. Alionekana kuanza kuwaamini watu hao ingawa wakati mwingine uaminifu wake ulionekana kuyumba.
Votz na wenzake hawakuonekana kuamini kama kazi ilikuwa ni rahisi namna ile. Walichokifanya kwa wakati huo ni kuchukua barabara ya Luberk na kuelekea katika mji wa Sassnitz, mji ambao ulikuwa ni kisiwa.
Kadri muda ulivyokuwa ukienda mbele na ndivyo wasiwasi ulivyoanza kumuingia Patrick, alijishangaa kwa nini hakuwa huru garini mule, alitamani kuuliza lakini kila alipotaka kufanya hivyo, aliamua kukaa kimya.
Gari lile likaanza kuingia katika eneo la nyumba moja kubwa ya kifahari. Watu zaidi ya ishirii waliokuwa na bunduki walikuwa wamesimama katia eneo la nyuma hiyo huku wakiendelea kuimarisha ulinzi mahali hapo.
Patrick akateremshwa na moja kwa moja kupelekwa katika chumba kimoja ambacho kilionekana kuwa na damu nyingi zilizoonekana kuganda ukutani. Chumba kile kilionekana kumtisha sana, amani yote ikatoweka, picha iliyokuwa ikionekana katika chumba kile ilionekana kumuogopesha.
*****
Kila alipotaka kusimama kwa ajili ya kuipinga harusi ile, Maria alijiona miguu ikikosa nguvu na kurudi chini. Machozi yake bado yalikuwa yameloanisha mashavu yake. Akabaki chini na kuinamisha kichwa chake chini na kuendelea kulia.
Bwana Mayemba akabaki akiwa na wasiwasi, akalirudia swali lake lile kwa mara ya pili na ya tatu, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa amesimama kuipinga harusi ile. Vigelegele vikaanza kusikika kanisani mule, mchungaji akafungisha ndoa, Bwana Mayemba na Bi Anna wakawa mke na mume.
*****

Watanzania walikuwa na furaha sana kila siku ambazo Patrick alikuwa akitangazwa katika vyombo vya habari kuwa kama mchoraji ambaye alikuwa akitarajiwa kuiwakilisha Marekani katika kinyeng’anyiro cha uchoraji bora ambacho kilitakiwa kufanyika nchini Ujerumani katika jji la Hamburg.
Kila Mtanzania alikuwa akijivunia juu ya Patrick ambaye kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo jina lake lilivyozidi kuwa kubwa zaidi na zaidi. Watanzania wengi wakaanza kuvaa fulana ambazo zilikuwa na picha za Patrick
Kila siku taarifa za habari nchini Tanzania zlikuwa zikitangaza mambo mbalimbali ambayo yalikuwa yakiendelea katika maisha ya Patrick. Patrick akaonekana kuwa lulu nchini Tanzania kuliko mtu yeyote yule. Walitamani Patrick angekuwa nchini Tanzania ambako angeanza kazi ya uchoraji na kuwa mchoraji mkubwa huku akiwa chini ya Watanzania.
Magazeti na vyombo mbalimbali vya habari vilikuwa vikimtangaza Patrick ambaye wengi walimuita uwa kijana wa maajabu ambaye alikuwa ameanza kuingiza kiasi kikubwa cha fedha katika kipindi kichache sana.
Kila Mtanzania alitamani Patrick ashinde katika kinyang’anyiro cha ubingwa wa dunia ambacho kilitakiwa kufanyika nchini. Sala zao zote zilikuwa kwa Patric kwani waliona kuwa hiyo ni nafasi kubwa ya kuweza kitangaza nchi ya Tanzania duniani kote.
******
Bwana Mayemba hakuonekana kuwa na furaha, muda wote alikuwa mpweke huku akionekana kuwa na mawazo kupita kawaida. Ukumbini hakutulia, mara kwa mara macho yalikuwa yakiangalia katika kila kona kumtafuta Maria japokuwa alikuwa akifahamu kwamba hakumpa kadi iliyomruhusu kuwa ndani ya ukumbi ule.
Kitendo cha kumuona Maria ndani ya ukumbi ule kulimkumbusha mbali sana, hakuamini kama angeweza kumuona Maria katika harusi yake huku akionekana kuwa tayari kuipinga harusi ile kufanyika. Mawazo yake yakaenda mpaka katika kipindi ambacho aliambiwa kwamba ana ujauzito wake.
Akatamani kumuona mtoto ambaye alizaa nae, hakujua kama mtoto huyo alikuwa hai au alikuwa marehemu. Bwana Mayemba akataka kusikia kila kitu kuhusu Maria na mtoto wake, moyo wake kwa upande mwingine ukaanza kujuta kwa kitendo chake cha kutokuwasiliana na Maria kwa kipindi kirefu hali iliyoonekana kuwa kama alimtenga.
“Mbona uko hivyo mume wangu?” Bi Anna alimuuliza Bwana Mayemba.
“Niko vipi? Mbona kawaida tu” Bwana Mayemba alijitetea.
“Hapana mpenzi. Ninakufahamu vizuri sana, hauko hivyo, hiyo si kawaida yako” Bi Anna alimwambia mzee Mayemba.
“Kuna vitu vinanichanganya sana”
“Vitu gani?”
“Kuna ripoti sijaziandika halafu wiki hii inabidi niziwasilishe katika ofisi ya rais. Ni kazi kubwa sana ambayo inaniweka katika mawazo, anaweza asinielewe” Bwana Mayemba alijaribu kudanganya.
Bi Anna hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya huku akiendelea kumsikiliza Mc ambaye alikuwa akiendelea kutangaza. Muda ulikwenda zaidi na zaidi mpaka muda wa zawadi kufikia, maharusi wakapewa zawadi zao na kisha baada ya hapo muziki kuanza kupigwa na watu kusherehekea.
Mara baada ya sherehe ya harusi kumalizika ukumbini, moja kwa moja maharusi wakapelekwa hotelini ambako huko walicheza michezo yote kama wanandoa. Kila mmoja alionekana kumfurahia mwenzake kwa kile ambacho alikuwa amefanyiwa katika usiku huo.
Siku iliyofuata, safari ya kuelekea katika visiwa vya Madagaska kama sehemu ya fungate yao kuanza. Bwana Mayemba akarudi katika hali ya mawazo tena, bado alikuwa akimkumbuka Maria, moyo wake ulikuwa ukimuuma sana kila alipoyakumbuka matendo ambayo alikuwa amemfanyia mwanamke yule.
Mara baada ya kuteremka kutoka katika ndege, moja kwa moja wakachukua taksi ambay iliwapeleka mpaka katika hoteli ya kitalii ya nyota tano iliyoitwa Tasmania Palace. Wakachukua chumba ambacho tayari walikuwa wamekwishawekewa na kuingia kitandani.
Mchezo ambao ulikuwa umefanyika katika hoteli ya Travertine jijini Dar es Salaam ndio ambao ulikuwa umeanza kufanyika mahali hapo. Kitanda kilikuwa kikilalamika tu huku kila mmoja akitokwa na jasho kutokana na kazi nzito ambayo ilikuwa ikifanyika.
Baada ya masaa mawili, kila mtu alikuwa hoi, moja kwa moja wakainuka kutoka kitandani na kuelekea bafuni ambako wakaoga na kuelekea katika mghahawa kupata chakula cha usiku.
*****
Mwalimu Simon na Vanessa wakapelekwa katika hoteli ya Lochamm ambako wakaingizwa mpaka katika vyumba ambavyo vilikuwa vimeandaliwa kwa ajili yao. Kila mmoja alijisikia huru kuwapo mahali humo kwa kuamini kwamba kila kitu kilikuwa salama.
Baada ya nusu saa, mratibu wa mashindano yale, Bwana Petersen akafika hotelini pale na moja kwa moja kuanza kuelekea katika chumba ambacho alielekezwa huku akiwa pamoja na wasaidizi wake. Bwana Petersen akabonyeza kengele ya mlangoni na baada ya sekunde chache mlango ukafunguliwa.
Wakaingia ndani huku wakianza kuangalia huku na kule. Kila walipokuwa wakiangalia ndani ya chumba kile, hakukuwa na dalili ya kuwepo kwa mtu mwingine.
“Patrick alichukua chumba kingine?” Bwana Petersen alimuuliza mwalimu Simon.
“Alipelekwa hotelini kama mipango ilivyopangwa”
“mipango gani?”
“Ya kutaka washiriki kukaa katika hoteli moja waliyopangiwa” Mwalimu Simon alimwambia Petersen ambaye akaonekana kushtuka.
“Hoteli ambayo wote waliyopangiwa kukaa ni hoteli hii. Hamkuambiwa chochote na wapokeaji?” Bwana Petersen aliuliza.
“Ndio waliotuambia hiki tunachowaambia”
Kila mmoja akanekana kushtuka, hawakuamini maneno yale ambayo waliambiwa. Kitu walichokifanya ni moja kwa moja kuelekea mpaka katika sehemu ya mapokezi kwa ajili ya kuuliza. Washiriki wote walikuwa wamefika hotelini pale isipokuwa mshiriki mmoja, Patrick.
Wasiwasi ukaanza kuwaingia kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kinaendelea. Hali ya hatari ikaanza kuonekana, wakaonekana kuchanganyikiwa kupita kawaida.
Wakaanza kuwapigia simu wale watu ambao walikuwa wamewapa jukumu la kwenda kuwapokea Patrick, Simon na Vanessa. Simu zilikuwa zikiita lakini wala hazikupokelewa jambo ambalo lilionekana kumtia wasiwasi kila mtu.
Wakaamua kwenda nje ya hoteli ambako wakachukua magari waliyokuja nayo hotelini pale na kuanza kuelekea uwanja wa ndege. Bwana Petersen na wenzake wakaonekana kutokuwa na raha kabisa, tayari walionekana kuwa na tatizo ambalo lilikuwa limetokea.
Mara baada ya kufika uwanja wa ndege, wakaanza kuangalia huku na kule kuona kama wangeweza kuwaona watu ambao walikuwa wamewatuma kuja kumpokea Patrick na wenzake. Hakukuwa na mpokeaji hata mmoja ambaye alionekana mahali hapo jambo ambalo liliwafanya kutokuelewa sehemu ambayo alikuwepo Patrick.
Hali ikaanza kuonekana kuwa ngumu kwao, walichokifanya ni kupiga simu katika kituo cha polisi jijini hapo, Hamburg na moja kwa moja Polisi kufika mahali hapo. Hawakujua ni kitu gani ambacho walitakiwa kuwaambia Polisi.
“Wir haben zu beruhigen und sagen Sie uns, was passiert ist (Inabidi tukae chini mtuambie ni kitu gani kilichotokea)” Polisi aliwaambia.
Wote wakachuliwa na kupelekwa kituo cha polisi ambako walitakiwa kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea. Bwana Petersen alionekana kuchanganyikiwa, hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kufanya kwa wakati huo.
Kwanza akaanza kuifikiria serikali ya Marekani ambayo ilionekana kuwa mwiba sana kwa wakati huo. Hakujua ni maelezo gani ambayo alitakiwa kutoa japokuwa yeye ndiye ambaya alikuwa amewatuma wale wapokeaji kwenda kuwapokea Patrick na wenzake.
“Ich denke, es ist Problem ( Nafikiri kuna tatizo)” Polisi aliwaambia mara baada ya kusikiliza maelezo yao.
Tayari kila mtu akaonekana kuwa na wasiwasi kwamba Patrick alikuwa amechukuliwa na watu ambao kazi yao ilikuwa ni kuwauwa watu waliokuwa na ngozi nyeusi ambalo lilikuwa likiongozwa na Bwana Khan pasipo kumfahamu.
Kitu walichokifanya ni kutoa taarifa katika serikali ya Marekani juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea. Taarifa ile ikaonekana kuwa kama mwiba mkali katika serikali ya Marekani, hawakuamini kile ambacho walikuwa wakielezwa kwa wakati huo.
Kwa haraka haraka pasipo kupoteza muda, wapelelezi watatu, Taylor, Filbert na Andrew kutoka katika kitengo cha upelelezi cha F.B.I wakatumwa kwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya kufanya upelelezi kujua mahali ambapo Patrick alikuwa amepelekwa.
Ndege ya rais, Air force One ikawabeba wapelelezi hao na kuanza kuelekea nchini Ujerumani. Kutokana na mwendo wa kasi uliokuwa nao ndege hiyo, ni saa moja tu wakawa wamekwishafika nchini Ujerumani na kuelekea katika hoteli ya Gasthof.
“Tuanzie wapi?” Tylor aliwauliza wenzake.
“Kwanza uwanja wa ndege”
Wala hawakuwa na muda wa kupoteza, moja kwa moja wakaanza kuelekea uwanja wa ndege ili kuangalia mazingira jinsi yalivyo. Waliangalia kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea mahali pae, waliporidhika, wakaondoka zao.
“Kuna kitu nimefikiria” Taylor aliwaambia.
“Kitu gani?” Filbert aliuliza.
“Hapa Ujerumani kuna ubaguzi mkubwa wa rangi. Watu wengi huuawa na miili yao kupelekwa katika bahari ya Baltic kutupwa. Kwa nini tusingeanzia huko?” Taylor aliwaambia.
“Hiyo sawa sawa” Andrew aliitikia.
Moja kwa moja wakatoka nje ya hoteli ambako wakachukua taksi na kutaka kupelekwa Ruberk ambako huko wangekwenda mpaka katika ufukwe wa bahari hiyo.
Safari ikaanza huku kila mmoja akiwa na bunduki yake, tayari wasiwasi ukaonekana kuwashika, hawakuamini kama wangeweza kumpata Patrick pasipo kutumia bunduki. Safari yao iliwachukua nusu saa, wakafika katika mji huo ambako wakaonganisha mpaka ufukweni.
Wakaanza kuangalia katika ufukwe ule kuona kama wangeweza kuona kitu chochote, hakukuwa na mtu yeyote yule zaidi ya walinzi ambao walikuwa wakionekana kulianda maeneo kadhaa ya hoteli ambazo zilikuwa zimejengwa pembezoni mwa bahari.

Je, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.