ad

ad

SI KITU BILA PENZI LAKO -16


 

NYEMO CHILONGANI
SI KITU BILA PENZI LAKO-16

Watanzania walikuwa wakikusanyika katika sehemu za kupigia kura. Kila mtu alikuwa na hamu ya kumchagua yule mtu ambaye aliamini kuwa angeyaweka maisha yake kuwa katika uafadhali. Maisha yalikuwa magumu kwa Watanzania wengi.
Watanzania walionekana kuchoka, hawakuonekana kabisa kuutaka uongozi ambao ulikuwa madarakani. Kadri dakika zilipokuwa zinasonga mbele na ndivyo ambavyo watu walikuwa wakizidi katika vituo vya kupigia kura.
Mchakato wa kupiga kura uliendelea zaidi na zaidi mpaka kumalizika. Watu ambao hawakutaka wizi wa kura utokee, walikuwa wakiyalinda maboksi ya kuhifadhia kura kuliko kitu chochote kile. Uchaguzi ulifanyika na muda wa kuhtangazwa mshindi wa uchaguzi ule kutangazwa.
Jina la Hidifonce Mayemba likatangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura zaidi ya laki mbili. Mitaani hakukukalika, watu wa wilaya ya Kinondoni hawakubaki majumbani, wakaanza kupita mitaani huku wakishangilia kwa shangwe.
Hivyo ndivyo kila kitu kilivyokuwa, Hidifonce Mayemba akachaguliwa na kuwa diwani. Mbele yake kulionekana kuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha kufanya kila kitu ambacho alikuwa amewaahidi wananchi kukifanya kwa nguvu zote kwa ajili ya kuleta mabadiliko maishani mwao.
Ingawa kila siku alikuwa akijiona kuwa na mafanikio lakini hakuweza kumsahau Maria, kila siku alikuwa akimkumbuka japokuwa hakutaka kabisa kumpigia simu kwani aliamini kuwa watu wangefahamu na hivyo kupata skendo kwamba alikuwa na mtoto na wakati hakuwa ameoa.
Kila siku alikuwa akipitia pitia majina katika simu yake, alipokuwa akilifikia jina la Maria, alikuwa akiliangalia kwa muda. Alitamani kupiga simu lakini alisita kufanya hivyo. Ni kweli alipmenda sana Maria, lakini kwa upande mwingine alikuwa makini sana kwa kutokutaka skendo za aina yoyote ile.
Siku ziliendelea kukatika mpaka katika kipidi ambacho akamsahau kabisa Maria, hakumkumbuka kabisa na hii ilitokana na kazi kubwa ambayo alikuwa akizifanya usiku na mchana.
Miaka mitano ikapita, watu wakaonekana kuvutiwa na kazi zake alizozifanya na hiyo ndio ikawafanya kumchagua kugombania nafasi ya ubunge. Kwa Hidifonce ilionekana kuwa kazi kubwa lakini kwa kuwa alikuwa na watu ambao walikuwa wakimsaidia, alijipa moyo kwamba angeweza tu.
Uchaguzi katika mwaka huo ukafanyika, Bwana Mayemba akafanikiwa kuutwaa ubunge wa Kinondoni jambo ambalo lilionekana kumpa furaha kupita kawaida. Maisha yake yalizidi kubadilika na hatimae kuchaguliwa na kuwa Waziri wa Wanawake na Watoto.
Kwa mara ya kwanza ambayo alimuona Bi Anna, akaonekana kuvutiwa nae, hakutaka kumkosa hata kwa nini. Alihitaji kufanya kila kitu ambacho alitakiwa kukifanya ili kumuweka mwanamke huyo katika mikono yake, ni kweli alimpata mpaka pale ambapo alikuwa akitarajiwa kufunga nae ndoa katika kanisa kubwa kuliko yote, Praise And Worship.
Kadi zilikuwa zimesambazwa katika kila sehemu na baada ya siku kadhaa, watu wakaanza kuelekea katika kanisa hilo kwa ajili ya kuangalia harusi hiyo ambayo ilikuwa ikitangazwa sana katika vyombo vya habari.
*****
Maria alionekana kuwa mgumu sana kumkubalia Jonas, bado moyo wake ulikuwa ukimkumbuka sana Hidifonce. Siku ziliendelea kukatika na hatimae kumkubalia Jonas na kufunga nae ndoa. Tukio hilo lilikuwa ni tukio kubwa ambalo lilibaki kuwa katika historia yamaisha yake.
Alimpenda sana mumewe, Jonas lakini kila alipokuwa akimuona binti yake, Natalia alikuwa akimkumbuka Hidifonce. Hidifonce alikuwa amekaa moyoni mwake sana na hii ilitokana na alama ya mtoto ambayo alikuwa amemuachia maishani mwake.
Miaka iliendelea kukatika mpaka kufikia katika kipindi ambacho akapata mtoto wa kwanza katika ndoa yake, huyu alikuwa wa kike ambaye yeye na mumewe walimpatia jina la Angelina. Mtoto huyu alionekana kuwa furaha sana katika familia hii, kila siku wanandoa hawa walikuwa wakikaa karibu kupita katika kipindi chote.
Mpaka katika kipindi ambacho Bwana Mayemba alikuwa akitangaza kuachana na ukapera miaka mitano iliyofuata, Maria alikuwa akiangalia taarifa hiyo ya habari. Moyo wa Maria ulimuuma japokuwa alijua fika kwamba alikuwa ameolewa na mwanaume ambaye aliyafanya maisha yake kuwa ya kitajiri sana.
Hakutaka kuendelea kubaki mkoani Kigoma, alihitaji kufanya kitu ambacho aliamini kuwa kingempa furaha katika maisha yake. Akapanga safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuipinga harusi hiyo na kisha kurudi Kigoma na kuendelea na maisha yake.
Ni hapo ndipo alipoamua kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya kile ambacho alikuwa amekikusudia kukifanya kwa wakati huo. Angani, aliiona ndege kwenda taratibu sana, alitamani kufika jijini Dar es Salaam haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuipinga harusi hiyo ambayo ilikuwa ikitangazwa sana katika vyombo vya habari.
“Nipeleke New Afrika Hotel” Maria alimwambia dereva teksi ambaye akampandisha na kuanza kumpeleka katika hoteli hiyo.
Maria hakutaka mtu yeyote hasa ndugu zake wafahamu kwamba alikuwa amekwenda jijini Dar es Salaam, kila kitu ambacho alikuwa akikitaka kukifanya kwa siri kubwa mpaka pale leng lake litakapokamilika.
Mara baada ya kufika hotelini, moja kwa moja akajipumzisha kitandani huku mawazo yakianza kufikiria mbali toka kipindi kile ambacho alikuwa pamoja na Hidifonce au Bwana Mayemba.
Usiku alipoamka, akachukua kitabu cha simu za mezani na kisha kuanza kuangalia namba za viongozi mbalimbali, alipoipata namba ya Bwana Mayemba ya simu ya nyumbani, akaanza kumpigia. Simu ilikuwa ikiita huku moyo wake ukiwa unamuuma kupita kawaida.
“Halooo...” Sauti nzito ya Bwana Mayemba ilikuwa ikisikika, Maria akajikuta akianza kutaasamu. Sauti ile ilikuwa imemkumbusaha maisha yake ya mbali sana, miaka mitano iliyopita. Moyo wake ukagawanyika, upande mwingine ulitamani kumwambia kile ambacho alikuwa amekusudia kumwambia lakini upand wake mwingine wa moyo wake wala haukutaka kufanya vile. Akaupiga moyo wake.
“Naongea na nani?” Sauti ya Bwana Mayemba ikasikika ikiuliza.
“Unanifahamu Mayemba. Ila kuna kitu nataka kukuambia” Maria alimwambia Bwana Mayemba.
“Kuna kitu unataka kuniambia! Kitu gani?” Mzee Mayemba alisikika akiuliza.
“Ni lazima nitaipinga harusi yako. Harusi haitofungika” Maria alimwambia Bwana Mayemba.
“Utapinga harusi isifanyike? Wewe ni nani na kwa nini unataka kufanya hivyo?” Mzee Mayemba huku sauti yake ikisikika kuwa na wasiwasi.
“Utanifahamu siku hiyo” Maria alisema na kukata simu.
Akarudi kitandani na kutulia. Mawazo yake bado yalikuwa yakimkumbuka Bwana Mayemba. Siku mbili zilipita na hatimae siku yenyewe kuwadia.
Maria alianza kupiga hatua kuelekea katika kanisa lile ambalo lilikuwa na idadi kubwa ya watu. Ulinzi mkubwa ulikuwa umeimarika kutokana na uwepo wa viongozi wa nchi pamoja na rais kanisani hapo. Maria akakifuata kiti ambacho hakikuwa na mtu yeyote na kisha kutulia.
Mara baada ya dakika kadhaa, maharusi wakaanza kuingia kanisani mule. Maria akajihisi akiumia moyoni mara baada ya kumuona Bwana Mayemba akiwa ndani ya suti nyeusi huku pembeni yake akiwepo mwanamke ambaye baada ya dakika kadhaa angekuwa mkewe.
Machozi yakaanza kumtoka Maria, alitamani nafasi ile ingekuwa yake na hivyo kuolewa na Bwana Mayemba. Mara baada ya maharusi kufika mbele ya kanisa mchungaji akaanza kuhubiri na kisha kuagiza pete ziletwe mahali pale.
“Kabla sijafungisha ndoa hii...kuna mtu ana sababu ya kuipinga harusi hii isifungike?” Lilikuwa swali ambalo lilimshtua Maria. Akayapeleka macho yake mbele ya kanisa. Bwana Mayemba alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi mkubwa.
Machozi yakaanza kumtoka Maria, kila alipokuwa akimwangalia Bwana Mayemba na ndivyo ambavyo alikuwa akikumbuka maisha yake ya nyumba pamoja na Bwana Mayemba. Mara wakagonganishiana macho na Bwana Mayemba ambaye alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi.
Machozi ambayo yalikuwa yakimtoka Maria yalikuwa yameloanisha mashavu yake. Kanisa zima lilikuwa kimya huku watu wakiangalia huku na kule kuona ni nani ambaye angesimama na kupinga ndoa hiyo. Maria akaanza kuinuka kitini taratibu kwa ajili ya kupinga harusi hiyo huku Bwana Mayemba akionekana kuwa na wasiwasi.
*****
Mishemishe ya kumwandaa Patrick kwa ajili ya kwenda nchini Ujerumani kushiriki shindano la uchoraji bado ilikuwa ikiendelea nchini Marekani. Kila siku Patrick alikuwa akitangazwa katika vipindi mbalimbali vya televisheni nchini Marekani. Jina lake likawa kubwa na kujulikana na watu wengi duniani.
Mtayarishaji wa kipindi cha mahojiano na masupastaa, Larry King akaamua kumuita Patrick na kumuhoji katka kipindi maalumu ambacho kilikuwa kikirushwa na kituo cha televisheni cha CNN ambacho makao yake makuu yalikuwa jijini Atalanta.
Kila mtu alikuwa akitaka kumuona Patrick ambaye alikuwa na mvuto kuliko mshindani yeyote, na hii ilitokana na jina lake ambalo lilikuwa likitangazwa mara kwa mara na picha zake kuwekwa mitandaoni. Kila mtu ambaye alikuwa akiziangalia picha zile alionekana kuvutiwa nazo na kujisemea kuwa Patrick alikuwa akistahili kuwa mshindi wa shindano lile lililopita.
Vituo vya televisheni vya nchini Uingereza, BBC na Sky News vilikuwa bize vikimtangaza mshindi wao katika bara la Ulaya aliyitwa Benard jnr. Benard alikuwa akitangazwa mara kwa mara na picha zake ambazo zilimpa ubingwa wa kuwa mchoraji bora barani Ulaya zilikuwa zikiwekwa katika mitandao mbalimbali.
Waingereza hawakutaka kushindwa, bado walielekeza nguvu zao kwa Benard ambaye alikuwa amechukua ushindi wa dunia katika uchoraji kwa mara mbili mfululizo. Waingereza walimtambua Benerd kama bingwa wao ambaye alistahili kuchukua ubingwa huo mpaka pale ambapo angejitoa katika mashindano hayo ambayo yalikuwa yakifanyika kila mwaka.
Kiwewe kiliwashika mara baada ya kuziona picha za Patrick ambazo zilikuwa zimempa ushindi. Kila muingereza hakuamini kama kuna mtu ambaye angeweza kuchora picha nzuri namna zile. Hakukuwa na mtu ambaye aliamini kama kweli picha zile zilikuwa zimechorwa kwa mkono wa mtu.
Waingereza wakazichukua picha zile na kuziweka katika kompyuta zao kwa ajili ya kuzichunguza kama kweli zilikuwa zimechorwa kwa mkoo wa mtu. Ingawa walitamani sana Benard achukue ubigwa ule kwa mara tatu mfululizo na kuweka rekodi lakini kwa jinsi picha za Patrick zilivyokuwa zikionekana, zilionekana kuwatia wasiwasi kupita kawaida.
Kila Muingereza alikuwa akizikubali kimoyo moyo picha zile ambazo kila aliyeziona duniani hakuamini kama zilikuwa zimechorwa kwa mkono wa mtu. Mioyo yao ilijikuta ikitamka kuwa Patrick alikuwa juu hata zaidi ya Benard wao ambaye walikuwa wakimwamini sana.
“Ulijisikiaje mara baada ya kutangazwa mshindi?” Bwana Larry King aliuliza.
“Nilijisikia furaha sana. Unajua kuweka rekodi na kuvunja historia ni kitu kizuri ambacho kila mtu anatamani kukifanya” Patrick alijibu.
“Kama unavyojua kwamba huko unapokwenda kuna wachoraji wengi wazuri, umejiandaa vipi kukabiliana nao?” Bwana Larry King aliuliza.
“Nimejiandaa vizuri. Ila katika hili ningependa kuwaambia watu kwamba picha ambazo nitazichora zitakuwa katika ubora ambao hakukuwa na mtu atakayetarajia” Patrick alisema.
Maneno yake hayo ndio ambayo yaliwafanya watu wote kuwa na hamu ya kutaka kuziangalia picha hizo ambazo alikuwa akizizungumzia. Hawakujua zingekuwa na ubora kiasi gani. Walijua kwamba alizichora picha nyingi nzuri ambazo zilikuwa na ubora wa juu, sasa walitaka kuziona picha hizo ambazo zilikuwa na ubora zaidi ya zile.
Uongozi wa nchini Marekani ambao ulikuwa ukijihusisha na idara ile ya uchoraji ikaandaa watu wawili ambao walitakiwa kwenda pamoja na Patrick nchini Ujerumani. Mtu ambaye walimteua alikuwa mwalimu wake, Simon Marth pamoja msichana Vanessa ambaye Patrick alitaka kwenda nae katika sehemu yoyote alipokuwa.
Harakati za safari zikaanza huku Patrick akitumia muda wa masaa sita kuchora picha katika maktaba ya nyumbani kwa mchungaji Smith. Alikaa chumbani mule kwa masaa hayo ambako baada ya hapo, picha zile zilikuwa zimekamilika.
Aliziangalia kwa makini, akajikuta akitingisha kichwa chake juu na chini kuonyesha ni kwa jinsi gani hata yeye mwenyewe alizikubali. Akatoka chumbani mule na kwenda kumuita mchungaji Smith pamoja na mkewe, Bi Rachel na kisha kuwaonyeshea picha zile tatu ambazo alikuwa amezichora.
Kila mmoja alikuwa amezikubali na kumpa ushindi Patick katika kinyanganyiro hicho. Picha zile ambazo zilikuwa zimebeba matukio matatu makubwa zilionekana kuwa kali zaidi kuliko zile ambazo alikuwa amezichora katika shindano lile lililopita.
“Huyu ni mwanamke wa Kihindi ambaye ameshikwa na uchungu wa kujifungua. Picha hii nimeichora kama ukumbusho wa kumkumbuka mwanamke yule wa Kihindi ambaye alijifungulia hotelini nchini India na kufariki dunia” Patrick alimwambia mchungaji Smith ambaye aliiangalia vizuri picha ile, hakuonekana kuamini kama picha ile ilikuwa imechorwa.
“Hii ni picha ya pili. Ni picha ambayo niliichora nilipokuwa nimesoma kitabu cha Vetnam. Huyu unayemuona ni askari wa Kimarekani ambaye anaonekana amejeruhiwa vibaya katika vita hivyo. Pembeni unayemuona ni mkewe ambaye alikwenda hospitalini kumuona pamoja na mtoto wake mpendwa” Patrick aliwaambia huku akiwakabidhi zile picha.
“Hii ya tatu.....” Patrick akaanza kuiangalia picha ile kwa makini. Uso wake ukabadilika, hali ya huzuni ikaanza kuonekana usoni mwake. Ghafla tabasamu likaanza kuonekana.
“Huyu ndiye msichana ambaye ninampenda sana maishani mwangu. Hapa ni katika hatua yangu ya mwisho ya kumuacha porini. Huyu ni mimi na huyu ni yeye tuko kichakani usiku. Hii mianga ya tochi ambayo mnaiona ni ya watu ambao walikuwa wakitukimbiza. Hapa ndipo ambapo nilimpa ahadi ya kumrudia kijijini na kumchukua kabla ya kumuoa. Huyu ndiye Victoria nimpendae” Patrick aliwaambia.
Mchungaji Smith akaichukua picha ile na kuanza kuiangalia. Hakuamini kama Patrick angeweza kuchora picha ambayo ilikuwa na ubora kama ule. Aliweza kujichora mwenyewe pasipo kujikosea hata sehemu moja. Msichana ambaye alikuwa akijulikana kuwa kama Victoria alikuwa akionekana vizuri, uzuri ambao alikuwa akiuzungumzia Patrick ulikuwa ukionekana vizuri sana.
“Hii ni nzuri sana. Nimeipenda sana” Mchungaji Smith alimwambia Patrick.
Tayari siku ambayo alikuwa akitakiwa kuelekea nchini Ujerumani ikawadia. Watu zaidi ya elfu moja walikuwa katika uwanja wa ndege wakimuaga Patrick ambaye akaingizwa katika ndege ya kukodi na kuelekea nchini Ujerumani akiwa pamoja na Simon na Vanessa ambaye muda wote alikuwa pembeni ya Patrick.
“Najua tunakwenda kuchukua ubingwa....tutarudi Marekani na ubingwa” Mwalimu Simon alimwambia Patrick.

Je, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.