SI KITU BILA PENZI LAKO -15
NYEMO CHILONGANI
SI KITU BILA PENZI LAKO-15
Maisha yalendelea kama kawaida kwa Hidifonce. Katika kipindi ambacho Maria alikuwa akisomea masomo ya kompyuta, alikuwa akiendelea kuwasiliana nae huku akifanya mchezo mchafu kama kawaida. Siku ziliendelea kukatika mpaka kufika kipindi ambacho Maria alitakiwa kwenda mkoani Kigoma kwa ajili ya kusomea ualimu.
Hidifonce aliendelea kumuahidi Maria ahadi mbalimbali ikiwa ile ya kuendelea kuwa nae mpaka mwisho wa maisha yake. Ni kweli moyo wake ulikuwa kwa Maria, mwaname ambaye alikuwa akimpenda kuliko yeyote hapa duniani.
Mawasiliano yao hayakukatika, kila siku waikuwa wakiendelea kuwasiliana kama kawaida. Kila mmoja alijisikia furaha kuwa karibu na mwenzake ingawa miili yao ilikuwa mbali sana. Halikuwa jambo rahisi hata mara moja kwa wawili hao kuwasiliana chini ya mara tano kwa siku, siku zote walikuwa wakiongea zaidi ya hapo.
Mara baada ya Hidifonce kuchukua kadi ya uwanachama wa chama cha siasa cha Republic, moja kwa moja wazee wakamtaka kugombea nafasi ya Udiwani katika uchaguzi ambao ulikuwa umebakiza miezi miwilikabla ya kufanyika.
Hidifonce hakukataa, alijua kwamba wazee hao walimchagua kwa kuwa tu alikuwa na elimu ya juu. Mishemishe ikaanza, siasa za hapa na pale zikaanza kufanyika. Wanachama wa chama cha Republic walikuwa wakikutana karibu kila wiki huku wakichukua nafsai hiyo kumfundisha Hidifonce mambo kadhaa.
Kutokana na kusoma sana somo la Uraia, Hidifonce hakupata tabu sana, akaanza kuelewa kwa haraka sana kile ambacho alitakiwa kukifanya wa wakati huo.
Siku ziliendelea kukatika mpaka katika kipindi ambacho kampeni zilipoanza. Wanachama wowote wakaonekana kumpa kampani Hidifonce ambaye kila alipokuwa akismama jukwaani na kuongea, hakukuwa na sababu ya kumyima nafasi hiyo ambayo alikuwa akiigombania.
Hidifonce alionekana kukaa kisiasa zaidi, alikuwa akiongea maneno mengi ya kufariji na kuahidi kuwapa nafasi kubwa wanawake ambao walionekana kuwa nyuma katika ngazi mbalimbali. Kila mkazi wa wilaya ya Kinondoni akaonekana kuvutiwa na maneno aliyokuwa akiongea Hidifonce katika mikutano mbalimbali ya kampeni.
Hidifonce akaonekana kuwakamata vilivyo wananchi wa wilaya ya Kinondoni kiasi ambacho mikutano yake ilikuwa ikijaza watu wengi kuliko mikutano ya vyama vingine vya upinzani. Kila mtu alikuwa akimkubali Hidifonce ambaye kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyoa ambavyoa alizidi kupata mvuto machoni mwa watu.
“Una mpenzi?” Mzee Khatibu alimuuliza Hidifonce ambaye kwa mbali alionekana kushtushwa na swali lile.
“Hapana”
“Una mtoto?”
“Hapana”
“Safi sana. Unajua kwa sasa hautakiwi kuwa na skendo hata mara moja. Najua wapinzani watakuwa wakifanya upelelezi wa chini chini kujua kama una mtoto au mpenzi. Cha msingi kuwa makini, hatuhitaji skendo kwani tayari unaonekana kushinda uchaguzi huu” Mzee Khatibu alimwambia Hidifonce.
Maswali yale yalionekana kumtia wasiwasi Hidifonce kiasi ambacho akaona kama angeendelea kumpiga simu Maria na kuongea nae, basi watu angefahamu kila kitu hali ambayo ingeanzisha skendo ambazo zingemfanya kushindwa katika uchaguzi.
Uamuzi ambao aliuona kufaa katika kipindi hicho ni kukata mawasiliano na Maria, laini ambayo alikuwa akiitumia zamani, akaitupa na kuitafuta laini nyingine. Hakutaka kabisa kuwasiliana na Maria, ila namba yake ya simu alikuwa ameiweka katika laini yake mpya pasipo kumpigia.
Siku ziliendelea kukatika na hatimae wiki tatu kubakia kabla ya uchaguzi kufanyika. Wazee wakamuita Hidifonce na kumuweka kikao. Kila kitu walikiona kuwa kinakwenda kama kilivyotakiwa. Tayari walijiona kutarajia kupata kile ambach walikuwa wakikitarajia kukipata.
“Kila kitu knakwenda sawa sasa ila kuna kitu ambacho ningependa sana kifanyike” Mzee Khatibu aliwaambia wazee wenzake waliokuwa katika kikao kile.
“Mgombea wetu anajitahidi sana kumvutia kila mtu, naona kwa sasa bora abadilishe jina lake. Asijiite tena Hidifonce, kwa heshima kubwa ajiite jina la ukoo la Mayemba” Mzee Khatibu aliwaambia.
Suala hilo likakubalika na kila mtu, Hidifonce hakulitumia jina hilo tena, kila mtu akaanza kumita Mayemba, jina la ukoo wake.
Siku ziliendelea kukatika zaidi na zaidi mpaka kufika kipindi ambacho siku mbili tu ndizo zilikuwa zimebakia kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika. Muda wote Mayemba alikuwa na wasiwasi kupita kawaida, hakuonekana kujiamini kabisa, lakini kila alipokuwa akiangalia jinsi alivyokuwa akikubalika, alijipa moyo wa kushinda nafasi hiyo ya Udiwani.
*****
Majaji walitumia dakika arobaini kuziangalia picha zile ambazo alikuwa amezichora Patrick, makubaliano tayari yalikuwa yamekwishawekwa kwamba picha zile zilikuwa ni za kuchorwa. Moja kwa moja wakaanza kurudi ukumbini ambapo bado minong’ono ilikuwa ikienedelea kusikika katika kila kona ukumbini pale.
Watu wakabaki kimya mara baada ya kuwaona majaji wale wakirudi ukumbini pale na kutulia vitini mwao. Majaji hawakuongea kitu chochote zaidi ya kuendelea kuziangalia picha za wachoraji wengine. Zoezi lile lilichukua takribani dakika arobaini na tano kumalizika.
Picha zote zikapelekwa kwa watu ambao walikuwa wakitumika kuziingiza katika mitandao ili watu waaanze kupiga kura. Wataalamu wa kompyuta walionekana kushangaa mara baada ya kuziona picha ambazo alizichora Patrick, picha zilikuwa zikionekana vizuri huku zikionekana kama zilikuwa zimepigwa picha kwa kutumia kamera.
Watu wakaanza kufungua mitandao katika simu zao na hatimae kuzikuta zile picha zikiwa zimekwishaingizwa, upigaji wa kura ukaanza mara moja. Si wau waliokuwepo ukumbini hapo ndio ambao walikuwa wakipiga kura, bali wananchi wote nchini Marekani walikuwa wakipiga kura.
Picha za washiriki wote zailikuwa zikionekana kuchorwa kwa ufasaha kabisa lakini picha za Patrick zilionekana kuwa tofauti na nyingine. Kura ziliendelea kupigwa huku watu wote waliokuwa ukumbini wakionekana kuwa bize na simu zao. Kura ziliendelea kupigwa zaidi na zaidi.
Baada ya nusu saa, muda wa kupigwa kura ukaisha. Watu wa mitambo wakakata upigaji wa kura. Kura zaidi ya milioni mia moja zilikuwa zimepigwa katika majimbo yote nchini Marekani pamoja na nchi nyingine za Amerika ya kati.
Kura zikagawanywa na kila mtu kuwa na kura zake, uhesabuji wa kura ukaanza mara moja kwa wataalamu wa kompyuta ambao walikuwa mahali hapo. Uhesabuji uliendelea kwa muda wa dakika chache kutokana na kompyuta zao kufanya kila kitu ambacho kilikuwa kikihitajika kufanywa.
Kura zikagawanywa na kila mtu kuwa na zake. Matokeo yakatumwa katika kompyuta ndogo ambazo walikuwa nazo majaji pale mbele ya ukumbi ule. Matokeo yalionekana kumshangaza kila mtu, historia ikaonekana kuvunjwa na rekodi ikaonekana kuwekwa.
Jaji mkuu, Mc Arson akasimama na kuanza kumwangalia kila mtu huku uso wake ukionekana kuwa na tabasamu pana. Akaanza kuongea mambo mengi hata kabla hajamtaja mshindi wa shindano hilo ambaye angejinyakulia kiasi cha dola milioni mbili ambazo ni zadi ya shilingi bilioni mbili za kitanzania na pia kwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya kushindana katika shindano kubwa la uchoraji duniani.
“Tumefanya kazi mchana na usiku kuandaa shindano hili. Tumempata mshindi ambaye nitakwenda kumtangaza mahali hapa, na ndiye ambaye atapata kiasi cha dola milioni mbili. Kuna kitu ambacho hapa pia ningependa kuwaambia.
“Umoja wa Mataifa umetoa nafasi kwa mshiriki ambaye atashinda katika shindano la dunia basi atakuwa balozi wa Umoja wa Mataifa ambaye atatembea sehemu mbalimbali kuangalia watoto wanaoteseka pamoja na wagonjwa mbalimbali.
“Katika shindano kubwa la dunia, mshindi atajipatia kiasi cha dola milioni thelathini na pia ataajiriwa katika kampuni kubwa ya Metropolian ambapo michoro yake itakuwa ikiuzwa kuanzia dola milioni moja kila mmoja,” Jaji mkuu Mc Arson aliwaambia watu ukumbini mule.
Kila mtu akaonekana kustaajabu, kiasi ambacho kilitangazwa kwa mtu ambaye angeshinda shidano hilo kilionekana kuwa kikubwa sana. Kila mtu akaanza kuomba Mungu kwamba mshindi wa shindano kubwa la Dunia basi angetoka nchini Marekani ili kwenda kupata sifa duniani kote.
Kila mmoja alijua kwamba nchi ya Marekani haikuwa na rekodi nzuri katika shindano hilo ambalo lilikwenda kufanyika nchini Marekani, hawakupata taji hilo kwa miaka mingi ya nyuma. Ni mwaka 1982 ndipo walipojinyakulia taji la mchoraji bora wa dunia, baada ya hapo, hawakunyakua tena mpaka muda huo.
Ingawa mara kwa mara walikuwa wakitoa wachoraji bora, lakini hawakuweza kuwa bora zaidi ya wale ambao walitoka katika mabara mengine. Kwa wakati huo walihitaji mtu bora ambaye angekwenda kuwawakilisha katika kinyang’anyiro kile na kupata heshima kubwa ambayo kila mtu alikuwa akiitamani.
Muda ulizidi kwenda huku kila mtu akiwa na hamu ya kumjua ni nani ambaye angekwenda kuwa mshidi katika kinyang’anyiro kile. Washiriki wote walikuwa wakitetemeka kwa hofu, kila mmoja alikuwa na wasiwasi huku akijuta kwa nini alichora michoro ile kwa sababu wote waliamini kwamba kama wangepewa nafasi nyingine zaidi, basi wangechora michoro mizuri zaidi.
“Our winner in this race is ....(Mshindi wetu katika kinyang’anyiro hiki ni.....)” Jaji mkuu alitangaza na kuanza kuinangalia kompyuta yake ndogo. Kila mtu ukumbini akabaki kimya akimsikiliza.
“A participant who is number 278, Patrick Innocent… (Mshiriki mwenye namba 278, Patrick Innocent...)” Jaji mkuu alitangaza.
Makofi ya shangwe yalisikika ukumbini hapo. Patrick akabebwa juu juu na wanafunzi wa shule ya Vanguard na kuanza kupelekwa mbele ya ukumbi ule. Watu waliokuwa na kamera wakaanza kumpiga picha Patrick ambaye wala hakupewa nafasi ya kukanyaga chini mpaka alipofikishwa mbele ya ukumbi ule.
Alisimama huku uso wake ukinyesha tabasamu pana, hakuonekana kuamini kama kweli alikuwa mshindi wa shindano lile. Patrick alikuwa ameweka historia na kutengeneza rekodi yake kwa kuwa mtu mweusi wa kwanza kwenda kuiwakilisha Marekani katika shindano kubwa la uchoraji wa dunia ambalo lilitarajiwa kufanyika nchini Ujerumani katika jiji la Hamburg.
Watu waliokuwa wakishughulika na mitambo, kwa haraka haraka wakaanza kumpiga picha Patrick na kuziweka katika mitambo. Kila aliyefungua Internet kwa wakati huo, aliziona picha zaidi ya hamsini za Patrick. Muda wote Patrick alikuwa akipunga mkono wake hewani na kutoa shukrani zake. Baada ya sekunde kadhaa, akakabidhiwa kipaza sauti.
“Hii imekuwa kama ndoto maishani mwangu, ndoto ambayo katika kipindi chote nilikuwa nikiiota. Namshukuru Mungu katika maisha yangu lakini vilevile ningependa kuwashukuru watu wote ambao wamenipigia kura kwa kuniona nastahili. Hakika nitaendelea kuwakumbuka maishani mwangu, naahidi kuwa sitowaangusha nchini Ujerumani” Patrick aliuambia umati ule.
Hivyo ndivyo shindano lilivyokwenda, kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa fedha za kitanzania kilikwenda kwa Patrick huku wale washiriki wengine waliopata nafasi za juu juu wakipokea zawadi kadharika. Magazeti yote nchni Marekani yalikuwa yamechapisha habari ya lile shindano huku picha za Patrick zikipamba kila kurasa ya mbele ya magazeti yale.
Patrick akaanza kupata umaarufu nchini Marekani, ushindi ambao alikuwa ameupata wa kuweka historia na kuvunja rekodi ndio ambao ulimfanya kujulikana zaidi. Hata wale ambao hawakuwa wakimfahamu Patrick wakataka kumuona kwa macho yao. Watu wengi wakawa wanamiminika katika shule ya vipaji ya Vanguard kwa lengo la kumuona Patrick ambaye kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kujulikana
Sherehe kubwa ya kumpongeza Patrick ikaandaliwa. Muda wote Vanessa alikuwa karibu na Patrick, kila picha ambayo alipigwa Patrick, Vanessa alikuwa pembeni yake. Ilikuwa ni furaha kwa kila mwanafunzi wa shule ya Vanguard siku hiyo.
Spika zaidi ya thelathini zilikuwa zimefungwa katika ufukwe wa Paradise uliokuwa katika jiji la Miami. Watu walisherehekea kupita kawaida, walikunywa mpaka kusaza. Muda mwingi Patrick hakuonekana kuwa na furaha kama ambavyo alitakiwa kuwa kitu ambacho kilimfanya Vanessa kuuliza mara kwa mara.
“Kwa nini kila siku uko hivyo Patrick. Unaonekana mnyonge, hauna furaha....kwa nini?” Vanessa alimuuliza Patrick.
“Nitakuwa vipi na furaha Vanessa? Nitakuwa vipi na furaha na wakati Victoria hayupo pamoja nami mahali hapa? Najua kwamba nina mafanikio kwa sasa lakini sitokuwa na furaha sana mpaka nitakapokuwa pamoja na Victoria” Patrick alimwambia Vanessa.
Kila siku Patrick alikuwa akimfikiria Victoria, aliyaona mafanikio aliyoyapata kuwa si kitu. Victoria ndiye ambaye alionekana kuwa kila kitu katika maisha yake. Hakutaka msichana yeyote awe katika maisha yake zaidi ya Victoria.
Alijua kwamba alikuwa na fedha nyingi na za kutosha ambazo angeweza kutumia atakavyo maishani mwake lakini pasipo kuwa na Victoria, fedha hizo hazikuonekana kuwa kitu maishani mwake. Kila siku alikuwa akimfikiria Victoria ambaye alikuwa nchini Tanzania akiishi katika maisha ambayo hakuyapenda kabisa.
Alijiona kuwa na uhitaji mkubwa wa kurudi nchini Tanzania ambako huko angekwenda mpaka katika kijiji alichokuwa akikaa Victoria na kisha kumchukua na kuondoka nae kuelekea nchini Marekani. Hakutaka Victoria aishi kwenye maisha ya tabu tena, aitaka msichana huyo aishi katika maisha ya kifahari kama yake.
Wiki nzima ilikatika. Washiriki ambao walitarajiwa kushiriki katika shindano kubwa la uchoraji lililoitwa BEST PICTURES OF THE YEAR COMPETITION walitakiwa kujiandaa kwa ajili ya shindano hilo ambalo lilitokea kupendwa kuangaliwa katika vituo vya televisheni kuliko kipindi chochote kile.
“Nitachora picha tatu muhimu sana” Patrick aliwaambia wanafunzi na walimu wa Vanguard katika kipindi ambacho wote walikusanyika ukumbini.
“Nitachora picha za matukio makubwa mawili duniani na tukio moja ambalo lilitokea katika maisha yangu” Patrick aliwaambia.
Kila mtu alikuwa na hamu ya kutaka kuziangalia picha hizo ambazo ziliahidiwa kuchorwa na Patrick. Wakajiandaa kuangalia picha hizo ambazo kila siku Patrck alikuwa akizisifia kuwa nzuri kuliko picha zozote zile alizochora kabla ya siku hiyo.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu mahali hapa.
Post a Comment