ad

ad

Rais Magufuli Amtaka Muhongo Aachie Ngazi, Aivunja Bodi ya TMAA na Kumfuta Kazi Mkurugenzi Wake

IKULU, DAR ES SALAAM: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo Jumatano, Mei 24, 2017 wakati wa kupokea Ripoti ya Kamati Maalum ya Utafiti wa Mchanga (Makanika) uliomo kwenye makontena yaliyozuiliwa kwenye bandari tofauti hapa nchini, pamoja na hatua nyingine, amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ajitathmini kwa kina na ikiwezekana aachie ngazi mara moja kufuatia madudu yanayoendelea kwenye wizara yake ikiwemo upotevu wa madini.
 
Akipokea ripoti hiyo, Rais Magufuli pia amemfuta kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), na kuivunja bodi hiyo kwa upotevu wa madini huku akiitaka TAKUKURU na vyombo vya dola kuwachunguza na kuwachukulia hatua wafanyakazi wa bodi hiyo.
Aidha Rais Magufuli ameonesha kusikitishwa mno na ripoti hiyo ambayo imebainika kwamba kiwango kikubwa cha madini kinachotoroshwa nje ya nchi.
Ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinalinda madini yasitoroshwe na amepiga marufuku usafirishwaji wa mchanga huo nje ya nchi.

“Niwashukuru kamati kwa kazi nzuri na walioifanya kwa uwazi. Nafahamu ilikuwa kazi ngumu ikabidi tuwape ulinzi maalum”
“Tupo kwenye vita kubwa. Tunafahamu watu walipewa fedha na wahusika ili kupinga uchunguzi huu. Watanzania kwenye hili wote tushikamane. Ni kitu cha kuumiza sana na kutia aibu mno.
“Nilimfukuza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati sababu alipoulizwa uzito wa dhahabu alitoa jibu uongo, nikashindwa kujizuia.
“Kwenye Wizara hizi nilichagua wasomi wa kuziendesha, sasa naona wasomi wenzao wamewa-‘prove wrong.’
“Imeelezwa kuwa kampuni hizi zikichukua huu mchanga, sio wao wanaochenjua, bali na wao wanawauzia watu wengine.
“Wizara hizi zinaonyesha kuwa hazikununua smelter labda kwa kutokujua, makusudi au hawajui majukumu yao ya kazi.
“Hatuwezi kuvumilia mambo haya, kuanzia leo ninamfuta kazi Mkurugenzi wa Bodi ya TMAA, ninaivunja rasmi Bodi ya TMAA, ninavitaka vyombo vya uslama kwa kushirikiana na TAKUKURU, kuwachunguza na kuwachukulia hatua wafanyakazi wote kwa upotevu wa madini.”
“Ninamtaka Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ajitahmini kwa kina, ikiwezekana aachie ngazi haraka,” alisema Rais Magufuli na kumaliza mazungumzo.

No comments

Powered by Blogger.