SI KITU BILA PENZI LAKO -14
NYEMO CHILONGANI
SI KITU BILA PENZI LAKO-14
Mapenzi kati ya Hidifonce na Maria yalikuwa moto moto. Kila siku walikuwa pamoja na kufanya mambo tofauti tofauti yaliyokuwa yakihusu mahaba. Maria ndiye ambaye alionekana kuchanganyikiwa zaidi, kasi kubwa ya mapenzi ilikuwa imemkamata.
Darasani hakusoma kabisa kwani muda mwingi alikuwa akimfikiria Hidifonce hali iliyomplekea kutofanya vizuri katika masomo yake. Alipoingia kidato cha nne, bado akili yake ilikuwa ikifikiria mapenzi zaidi hali iliyompelekea kufeli mitihani yake ya mwisho.
Matokeo yale yalimfanya kutokuendelea na kisato cha tano, mchungaji Christopher na mkewe wakaamua kumuanzisha katika chuo kimoja ambako huko alikwenda kusomea kompyuta. Muda mwingi Maria bado alikuwa akiutumia kumfikiria Hidifonce, mapenzi bado yalikuwa yakiendelea kumchanganya.
Japokuwa bado alikuwa akisomea kozi ya kompyuta lakini bado Maria hakuonekana kutulia kabisa, bado mapenzi yalikuwa yakiendelea kumchanganya kila siku. Alichukua muda wa miezi miwili, kutokana na kuwa na alama zilizokuwa zikiridhisha, akapelekwa katika chuo cha uwalimu katika wilaya ya Kasuru Mkoani Kigoma.
Huko kidogo akaonekana kusoma, mawazo juu ya Hidifonce yalikuwa yakiendelea japokuwa hayakuwa kama kipindi ambacho alikuwa Dar es Salaam. Kila siku walikuwa wakiaidiana mambo mengi kuhusu maisha yao ya baadae, kila mmoja alitamani kuwa na mwenzake.
Hali ikaanza kubadilika, mabadiliko ya mwili yakaanza kumtia wasiwasi Maria. Muda mwingi alikuwa akijisikia kichefuchefu hali iliyompelekea kupenda sana kula vitu vichachu. Maria alijua ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea mwilini mwake, tayari akajijua kwamba alikuwa mjauzito.
Ingawa bado alikuwa akiendelea kuwa katika hali hiyo, alijitahidi sana kusoma kwani aliamini kama angefanikiwa basi mtoto wake ambaye alikuwa tumboni ni lazima angeishi maisha ambayo alitaka aishi. Taarifa za ujauzito wake akaamua kumpa Hidifonce ambaye akaonekana kushtuka kupita kiasi.
“Mbona umeshtuka sasa?” Maria alimuuliza Hidifonce simuni.
“Kulea. Unajua kuna kazi fulani nimeanza kuifanya, nimewaeleza ukweli kama sina mke wala mtoto” Hidifonce alimwambia Maria.
“Sasa unafikiri tutafanyaje mpenzi?”
“Nitaishi nawe ila kwanza acha nikamilishe hii kazi ambayo nimepewa”
“Kazi gani mpenzi?”
“Ya kawaida tu. Usijali. Nitakutaarifu” Hidifonce alimwambia Maria.
Huo ndio ukawa mwisho wa kuongea na Hidifonce mwaka huo. Kila alipokuwa akimpigia simu, hakuwa akipatikana. Jambo hilo lilionekana kumuumiza sana Maria lakini hakuonekana kujali kitu chochote kile. Bado akili yake akaiweka katika kusoma.
Baada ya miezi tisa, Maria akajifungua mtoto mzuri wa kike ambaye alimpa jina la Natalia. Natalia alionekana kuchukua kila kitu kutoka kwa mama yake. Sura yake iikuwa ikimvutia kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia. Uzuri wa Natalia ukawapelekea watu kuona kuwa mtoto huyo angekuja kutisha sana katika miaka ya baadae.
Alipomaliza masomo yake, akachaguliwa kufundisha katika shule ya msingi ya Kigoma. Kutokana na kuingiza fedha za kutosha kila mwisho wa mwezi, Maria akaanza kuyatengeza maisha yake na ya mwanae. Akapanga nyumba nzima maeneo ya Mji Mwema.
Nyumba ilikuwa kubwa lakini ni watu wawili tu ndio ambao walikuwa wakiishi humo. Kila siku Maria alijitahidi kumlea Natalia katika maisha ambayo mtoto alitakiwa kulelewa. Baada ya kuona kwamba kazi zilikuwa nyingi, akaamua kumuajiri msichana ambaye akaanza kumsaidia kazi pale nyumbani kwake.
Bosi wa shirika la Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa akiishi karibu na nyumba aliyopanga Maria akatokea kumpenda Maria. Kila siku bosi huyo, Jonas alikuwa akijitahidi kuwasiliana na Maria huku lengo lake kubwa likiwa ni kuweka mazoea makubwa ambayo yangepelekea kumtaka uhusiano.
Mara ya kwanza Maria alikuwa akiona usumbufu kupokea simu zaidi ya kumi na tano kutoka kwa Jonas lakini baadae akaonekana kuzoea, hakuona tena usumbufu wowote ule. Jonas alijitahidi kupiga hatua moja mpaka nyingine.
Hapo akaanza kumuomba Maria watoke chakula cha usiku ombi ambalo Maria wala hakukataa hata kidogo. Mara kwa mara walikuwa wakitoka mitoko ya kwenda hotelini lakini wala Jonas hakutamka kitu chochote kile, bado alikuwa akijipanga zaidi.
Kwanza alitaka kumsoma Maria, alitaka kujua mwanamke huyo alikwa akipendelea nini zaidi maishani mwake na vitu gani ambavyo hakuwa akivipendelea. Kumsoma Maria halikuwa jambo dogo, lilimchukua miezi miwili, akaonekana kujua mengi kutoka kwa Maria.
“Kwa nini mara kwa mara unaonekana mpweke?” Jonas alimuuliza Maria.
“Mawazo Jonas...”
“Mawazo ya nini tena? Au kazi unayoifanya hauitaki?” Jonas alimuuliza Maria.
Maria hakujibu chochote kile, alibaki kimya. Jonas hakutaka kuendelea kuuliza maswali zaidi, akaamua kuanzisha stori nyingine.
Bado Maria hakuwa sawa kiakili, kila siku alikuwa akimuwaza Hidifonce, moyo wake ulikuwa ukimuuma kupita kawaida mara baada ya kuona kwamba Hidifonce alikuwa amebadilisha namba ya simu. Muda mrefu uipita toka mara ya mwisho kuongea na Hidifonce, moyo wake haukuwa na furaha kabisa.
“Kuna kitu nataka kukwambia Maria” Jonas alimwambia Maria siku moja baada ya kutoka chakula cha usiku.
“Kitu gani?” Maria aliuliza.
“Kuna kazi nimekutafutia. Nimekutafutia kazi katika shirika la Umoja wa Mataifa” Jonas alimwambia.
Maria akaonekana kushtuka kupita kiasi. Hakuonekana kuamini kile ambacho alikuwa amekisikia kutoka kwa Jonas. Kufanya kazi katika shirika la Umoja wa Mataifa kulionekana kumchangaya kupita kiasi. Alilijua fika shirika hilo, lilikuwa moja ya mashirika makubwa duniani ambayo yalikuwa yamegawanyika katika vitengo vingi. Alimwangalia Jonas mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini.
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo Maria. Nimefanya hivyo kwa sababu ya kitu kimoja tu” Jonas alimwambia Maria.
“Kitu gani?”
Jonas hakutaka kujibu kwa haraka haraka, alibaki kimya kwa muda akimwangalia Maria. Uzuri wake ulionekana kumvutia kupita kawaida, akajisogeza kwa karibu zaidi. Akaupeleka mkono wake na kuushika mkono wa Maria.
“Nakupenda Maria. Mapenzi makubwa ambayo nimekuwa nayo juu yako ndiyo ambayo yamenifanya kkufanyia hivi. Nakupenda Maria, ninahitaji kuwa nawe, ninahitaji kukuoa na tuwe na familia yetu” Jonas alimwambia Maria.
Maria alibaki kimya. Maneno yae yaliirudisha akili yake nyuma kabisa, akaanza kumfikiria Hidifonce. Moyo wake ulikuwa kwa Hidifonce japokuwa kwa asilimia fulani Jonas alikuwa ameanza kuingia. Alimwangalia Jonas, picha ya Hidifonce ikawa ikijirudia mara kwa mara kichwani mwake.
“Haiwezekani Jonas” Maria alimwambia Jonas ambaye akashusha pumzi ndefu.
“Unasemaje?”
“Najua haukutegemea kulisikia hili Jonas”
“Tatizo nini Maria. Tatizo liko wapi kama nimamua kujitolea maisha yangu kwa ajili yako. Ninakupenda Maria. Ninajitahidi kufanya kila niwezapo kukufanya ufurahie maishani mwako” Jonas alimwambia Maria ambaye akaanza kulia.
“HIDIFONCE’ Lilikuwa jina ambalo lilikuwa lijirudia kichwani mwa Maria.
*****
Picha ile ambayo alikuwa ameichora Patrick ilibandikwa katika ubao wa shule. Kila mtu ambaye alikuwa akiiangalia picha ile, hakukuwa na yeyote ambay aliamini kama duniani kungekuwa na mtu ambaye alikuwa akijua kuchora namna ile.
Kila wakati Vanessa alikuwa mwenye furaha, jina lake nalo likaanza kusikika shuleni pale. Picha ile ikaonekana kuanza kumtambulisha shuleni hapo kwamba hata na yeye alikuwepo. Kila mtu akataka kumuona Patrick ambaye alikuwa ameichora picha ile ambayo baadhi ya wanafunzi wakaanza kuipiga picha kwa kutumia simu zao na kisha kuihifadhi.
Siku iliyofuata, Patrick alikuwa akiingia shuleni hapo. Kila mwanafunzi alikuwa akimwangalia kupita kiasi hali ambayo ilimfanya kusikia aibu. Patrick akapigwa na mshtuko mara baada ya kupita karibu na ubao wa shule na kuikuta picha ile ambayo alikuwa amemchora Vanessa.
Patrick alisimama kwa muda, wanafunzi wakaanza kujisogeza karibu nae ili kutaka kujua ni hali gani ambayo Patrick angeionyesha mahali hapo. Patrick akabaki akiiangalia, tabasamu likaanza kuonekana usoni mwake. Wanafunzi wote ambao walikuwa wamesimama karibu nae, nao wakajikuta wakitabasamu pamoja nae.
Patrick akaanza kupiga hatua kuelekea darasani. Wanafunzi wale wakaanza kumfuatilia, Patrick akaanza kuonekana binadamu asiye wa kawaida machoni mwao. Wala hakufika mbali, akajikuta akiitwa na mwalimu mmoja ambaye alikwenda nae mpaka ofisini.
Walimu zaidi ya thelathini walikuwa vitini mwao wametulia, katika kipindi ambacho Patrick alikuwa akiingia ofisini hapo, walimu wote wakanyamaza na kuanza kumwangalia Patrick. Picha ile bado ilikuwa ikijirudia rudia vichwani mwao. Patrick alionekana kuwa binadamu ambaye alikuwa na zaidi ya kipaji kile ambacho alikuwa nacho.
Walimu waliongea nae kwa muda wa dakika kadhaa, waliporidhika, wakamruhusu aelekee darasani. Vanessa ambaye alikuwa ametulia kitini, akainuka na kuanza kumfuata Patrick na kumkumbatia kwa furaha. Patrick hakuongea kitu chochote kile zaidi ya kutoa tabasamu pana.
Wanafunzi wenzake wa mule darasani wakaanza kumsogelea Patric ambaye alikuwa ametulia kitini huku akionekana kufikiria kitu. Kila mwanafunzi mahali hapo alitaka kuchorwa, kila mmoja akatoa karatasi na kuiweka mezani.
Patrick akabaki akishangaa, hakutarajia kama picha ile ambayo alikuwa ameichora ingewafanya wanafunzi kutaka kuchorwa. Hakuongea kitu chochote, alibaki kimya huku akiwaangalia wanafunzi wale.
“Mwacheni apumzike” Vanessa aliwaambia.
Hapo ndipo Patrick alipoanza kukionyesha kipaji chake. Alichora picha nyingi sana ambazo zilichukuliwa na kubandikwa ukutani. Habari za Patrick zikaanza kusambaza katika shule zote ambazo zilikuwa jijini Florida. Kila mtu ambaye alizisikia habari zile alitamani kufika shuleni hapo Vanguard kujionea mwenyewe.
Hakukuwa na mtu ambaye aliamini mara moja kama picha zile ambazo alikuwa akiziangalia ubaoni zilikuwa zimechorwa. Kila siku watu walikuwa wakibishana, wengine walikubali na kusema kwamba zile picha zilikuwa zimechorwa lakini watu wengine walipinga kwa nguvu zote.
Siku ziliendelea kukatika mpaka katika kipindi ambacho mashindano ya dunia ya uchoraji ambayo yalijulikana kama BEST PICTURES OF THE YEAR yalipotarajiwa kufanyika duniani kote. Miezi sita ndio ambayo ilikuwa imebakia kabla ya shindano hilo ambalo lilikuwa likiwasisimua watu kuanza.
Shindano hilo lilitakiwa kuchukua nafasi kuanzia ngazi ndogo mpaka kufikia hatua yenyewe kubwa. Lilitakiwa kuanza kishule ambako baada ya hapo, shule zote katika jiji moja lingemtoa mtu mmoja ambaye angeshindana na wachoraji kutoka katika katika majiji mengine.
Mtu ambaye angeibuka ambaye angeibuka mshindi, angekuwa mshindi wa jimbo zima ambapo baada ya hapo angeshindana na washindi wa majimbo mengine. Mshindi ambaye angepatikana hapo, moja kwa moja angeshindana na wachoraji wa bara zima ambapo mshindi wa hapo, angekuwa miongoni mwa washiriki sita ambapo kila mmoja angekuwa analiwakilisha bara alilotokea.
Safari ilionekana kuwa kubwa lakini kwa kila mwanafunzi ambaye alimfahamu Patrick, kazi ilioekana kuwa rahisi sana.
Ili kuepuka usumbufu ambao ungejitokeza, moja kwa moja Patrick akapitishwa na shule pasipo kufanya shindano lolote. Yeye ndiye ambaye alitakiwa kuiwakilisha shule ya Vanguard katika mashindano ya jiji ambayo yalitakiwa kufanyika baada ya wiki moja.
Patrick akaanza maandalizi ya kuchora, alikuwa akichora picha nyingi huku Vanessa akiwa mhakiki wa picha zake. Kila picha ambayo alikuwa akionyeshewa Vanessa, alibaki akiwa amechanganyikiwa tu. Kila picha ambayo alikuwa akiiangalia, ilionekana kumvutia kupita kiasi.
Siku ziliendelea kukatika mpaka kufika katika siku ya shindano lenyewe. Kila mtu alionekana kumhofia Patrick. Ni kweli walichora picha nyingi lakini kwa picha ambazo zilichrwa na Patrick na kubandikwa ukutani, zile tu zilionekana kuwaburuza vibaya.
Watu zaidi ya elfu ishirini walikuwa wamekusanyika katika ukumbi wa Matepolian ambao ulikuwa katika jiji la Jacksonville hapo hapo jimboni Florida. Umati huo ulikuwa umekusanyika mahali hapo kwa ajili ya kujua ni mtu gani ambaye alikuwa anakwenda kuliwakisha jimbo la Florida katika mashindano hayo ya kuchora.
Jina la Patrick lilikuwa likisikika katika kila kona ukumbini humo, picha zake ambazo alikuwa amezichora katika kipindi cha nyuma tayati zilionekana kupata umaarufu kupita kawaida.
Shindano likaanza mara moja, picha mbalimbali za washiriki mbalimbali zikaonyeshwa wazi, watu kitu ambacho walitakiwa kukifanya ni kutuma ujumbe mfupi wa picha za mtu ambaye alionekana kuwa na picha nzuri.
Hata kwa wale waliokuwa majumbani mwao hawakupata tabu kwani kituo cha runinga cha WPST ambacho kilikuwa na makao makuu katika jiji la Miami hapo hapo jimboni Florida kilikuwa kikirusha moja kwa moja kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea ukumbini hapo.
Ndani ya dakika kumi, zaidi ya kula milioni ishirini zilikuwa zimepigwa kwa kutumia simu pamoja na mtandao wa Internet. Mara baada ya muda wa kupiga kura kupita, kila kitu kikafungwa na moja kwa moja watu ambao walikuwa karibu na mashine ya kuhesabia kura kuanza kufanya kazi zao.
Patrick alionekana kukimbiza kupita kiasi, picha zilikuwa nzuri kuliko za mchoraji yeyote ambaye alishiriki katika kinyang;anyiro hicho. Patrick hakuonekana kuamini kile ambacho kilikuwa kimetangazwa na majaji. Wanafunzi wa Vanguard walikuwa wakirukaruka kwa furaha wakiyafurahia matokeo yale.
Kwa miaka mia moja na kumi tangu shule hiyo ianzishwe, hiyo ndio ilikuwa mara ya kwanza kwa shule hiyo kutoa mchoraji bora, kila mwaka walikuwa wasindikizaji tu.
Sherehe kubwa ya kumpongeza Patrick ikaandaliwa katika ufukwe wa Miami. Watu walisherehekea kupita kiasi huku muda wote Vanessa akiwa karibu na Patrick. Kila mtu alikuwa akitaka kupiga picha na Patrick ambaye alianza kuwa maarufu kwa wakati huo.
“Mbona unaonekana kutokuwa na raha Patrick?” Vanessa alimuuliza Patrick.
“Sijisikii kuwa na furaha Vanessa”
“Kwa nini?”
“Victoria. Moyo wangu unamkumbuka sana Victoria”
“Hata kama Patrick. Furahia tu, tutakwenda pamoja kumchukua huko alipo na kumleta hapa”
“Inaniuma sana. Naishi maisha mazuri na wakati yeye anaishi katika maisha ya tabu...inaniuma sana” patrick alimwambia Vanessa.
“Najua ni jinsi gani unampenda Victoria. Usijali, utakuwa pamoja nae karibuni” Vanessa alimwambia Patrick.
Patrick akaonekana kufarijika kupita kiasi, maneno aliyoongea Vanessa yalionekana kumpa nguvu. Tabasamu pana likaanza kuonekana usoni mwake. Kila siku alikuwa akimuona Vanessa kuwa karibu nae kuliko mtu yeyote shuleni. Akayapeleka macho yake usoni mwa Vanessa, Patrick alibaki akitabasamu tu.
Mwezi ukapita, shindano bado lilikuwa likiendelea, hatua hii ilikuwa ni kuwashindanisha washindi wote ambao walikuwa mabingwa katika majimbo yao. Washindi kutoka New York, Washington na sehemu nyingine nchini Marekani wakakusanyika katika ukumbi wa Staples Center uliokuwa katika jimbo la Los Angelel.
Majaji wakubwa watano wa kimataifa walikuwa wamejiandaa vilivyo kwa ajili ya kufanya kazi ya kumchagua mchoraji bora ambaye angeiwakilisha nchi ya Marekani katika mashindano ya dunia ambayo yalitazamiwa kufanyika baada ya mwezi mmoja nchi Ujerumani.
Mpaka linabakia saa moja kabla ya shindano kuanza, tayari ukumbi mzima ulikuwa umekwishajaa na watazamaji zaidi ya elfu ishirini walikuwa wamekusanyia huku watu wengine wakikosa nafasi na kuamua kubaki nje wakifuatilia katika televisheni kubwa zilizokuwa zimewekwa ukutani.
Mara baada ya kila kitu kukamilika, moja kwa moja picha zikaanza kuletwa kwa majaji ambao walitakiwa kuziunganisha katika mashine iitwayo Projector ambayo ilitumika kupiga katika kitambaa kikubwa cheupe na kuifanya picha ile ionekane kwa ukubwa.
Vile vile wataalamu ambao walikuwa wamesomea mambo mengi kuhusiana na mitandao walikuwa mahali hapo. Kazi yao kubwa ilikuwa ni kuzipiga picha picha zile na kisha kuziingiza mtandaoni. Kazi hiyo ilitakiwa kufanyika kwa haraka sana na ndio maana walikuwa wamewaita wataalamu wa mitandao ambao waliwaamini kuwa wangefanya kazi hiyo kwa haraka sana.
Majaj wakaanza kuzipitia picha moja baada ya nyingine. Watazamaji wote walikuwa wameziandaa simu zao kwa ajili ya kupiga kura mara tu wangeruhusiwa kufanya hivyo hata kabla ya muda kuisha. Majaji wakaonekana kuziangalia picha zote kwa makini.
Wanafunzi wa shule ya Vanguard walikuwa wamekaa katika sehemu moja pamoja na Patrick ambaye alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi mwingi. Kama kawaida yake, Vanessa alikuwa pembeni yake akimfariji na kumtia moyo kwamba angeibuka mshindi katika kinyang’anyiro hicho.
Majaji bado walikuwa wakiendelea kuziangalia picha za mshirika mmoja mmoja. Walipofika katika picha za Patrick, majaji wote wakasimama na kwenda katika chumba kimoja ambacho kilikuwa na viti pamoja na meza kwa ajili ya kufanyia mikutano midogo midogo.
Kila mtu akabaki akishangaa, hawakujua sababu ambayo iliwapelekea majaji wale kuondoka ukumbini na kwenda katika chumba cha faragha. Minong’ono ikaanza kusika kutoka ukumbini pale.
Majaji walikuwa wamekaa katika viti ndani ya ukumbi ule mdogo huku picha za Patick zikiwa mezani. Picha zile ndizo ambazo ziliwafanya kukusanyika katika chumba kile, zilionekana kuwachanganya kabisa. Kila mmoja alikuwa akizichukua picha zile na kuziangalia.
“Mnazionaje picha hizi jamani?” Jaji mmoja aliuliza.
“Mimi mwenyewe zinanichanganya. Hivi zimechorwa au zimepigwa picha na kamera?” Jaji mwingine aliuliza.
“Mmmh! Hapana. Hakuna mtu anayeweza kuchora namna hii. Hizi zitakuwa zimepigwa picha na kamera” Majaji waliendelea kuziangalia picha zile.
Je, nini kitaendelea?
Post a Comment