Umoja wa Mataifa waingilia kati sakata la kupotea kwa Ben Saanane
Sakata
la kupotea kwa mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema, Ben Saanane
limechukua sura nyingine baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kusema upo
tayari kutuma watu nchini kwa ajili ya uchunguzi.
Saanane,
ambaye pia ni msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba 18 mwaka jana na hadi
sasa haijaeleweka kuwa alitekwa au kuuawa, ingawa Chadema imehusisha
kutoweka kwake na taarifa ambayo Saanane aliitoa kwenye mitandao ya
kijamii kuhusu utata wa elimu ya baadhi ya viongozi.
Siku
chache baada ya kupotea kwa Saanane, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu
Lissu aliitaka Serikali kueleza kama inamshikilia kada huyo au ifanye
uchunguzi wa kina kuhusu kupotea kwake.
Sanjari
na hilo, Lissu aliitaka Serikali kufuatilia ujumbe wa vitisho ambao
Saanane aliwahi kutumiwa kwenye simu yake ya mkononi na mtu ambaye bado
hajafahamika.
Akisisitiza
msimamo wa chama chake, Lissu alizitaka mamlaka zote husika na usalama
wa raia ziseme hali halisi inayozingira sintofahamu ya mahali alipo,
ikiwa yuko ndani ya nchi au nje, au hata kama amefariki na kuzikwa kwa
kutotambuliwa.
Wakati
utata huo ukiendelea, ofisi ya kamishna mkuu wa haki za binadamu
duniani ya UN yenye makao yake makuu jijini Geneva, Uswisi, imesema iko
tayari kutuma timu ya uchunguzi.
Uamuzi
huo ulifikiwa katika mkutano uliotishwa na ofisi hiyo, Kanda ya Afrika
uliohusisha nchi za Sudan, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Ethiopia,
Djibouti na Tanzania.
Jana,
mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen
Kijo- Bisimba alisema suala hilo liliibuka baada ya wajumbe wa mkutano
huo kutaka kujua undani wa sakata hilo, lakini hakukuwa na taarifa za
kina.
“Wajumbe
walionyesha kuguswa na suala la mtu kupotea katika mazingira ya utata
na kutaka tuelezee kwa undani ilivyokuwa. Hatukuwa na taarifa za kina
hivyo wakasema wako tayari kulifanyia kazi endapo tutatuma urgent
alert,” taarifa ya dharura.
“Taarifa
tutakayotuma ndiyo itakayowawezesha wao kutuma timu ya uchunguzi ije
hapa baada ya hapo watajua ni kitu gani waseme kwa Serikali.”
Dk
Bisimba alieleza kuwa bado taarifa hiyo haijaandikwa kutokana na
kuwasubiri ndugu wa Saanane ambao wanatakiwa kutoa maelezo kwa kina.
“Tuliwaambia
ndugu zake waje tupate maelezo yatakayotuwezesha kuandika hiyo urgent
alert, lakini bado hawajaja. Watakapofika tutaandika na kuituma ili
uchunguzi ufanyike.”
Alipotafutwa
kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa suala hilo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai(DCI), Kamishna Robert Boaz alisema: “Nitafute Jumatatu
kwa sasa nipo kwenye kikao.”
Post a Comment