ad

ad

Mtatiro: CUF Hatushughulishwi na Matamko ya Watu Waliochanganyikiwa, Ashauri Lipumba Apelekwe Mirembe



Baada ya Baraza Kuu la Uongozi Taifa la Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kwa Mwenyekiti wa CUF Taifa, anayetambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Ibrahim Lipumba juzi Jumanne kutangaza kummvua, Maalim Seif nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Chama hicho na nafasi hiyo kukaimiwa na Bi. Magdalena Hamis Sakaya hatimaye Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro ameibuka na kutoa ufafanuzi kuhusu Katibu Mkuu wa CUF.

Akiandika ufafanuzi huo kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mtatiro amesema ndani ya CUF hawashughulishwi na matamko ya watu waliochanganyikiwa na kushauri Profesa Lipumba apelekwe Mirembe huku akitoa angalizo kuwa huko njiani wanaompeleka wanaweza pia kupigwa mabomu na akaondolewa mikonononi mwao na kurudishwa Buguruni.

Usome ujumbe wa Mtatiro hapa;

"KUHUSU KATIBU MKUU WA CUF...

Katibu Mkuu wa CUF anachaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa. Maalim Seif alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu mwaka 2014 sambamba na Lipumba (Uenyekiti) na Juma Duni Haji (Umakamu Mkiti).

"Mwaka 2015 Lipumba alijiuzulu na mwaka 2016 Mkutano Mkuu wa Taifa ulithibitisha na kukubali kujiuzulu kwake kwa asilimia 70 ya kura za wajumbe wa Bara na Zanzibar (Mkutano Mkuu ilihitimisha UENYEKITI wa Lipumba). Juma Duni Haji alijiunga CHADEMA kwa maelekezo ya Baraza Kuu la CUF, kwa hiyo nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti iko wazi kama ilivyo wazi ile aliyowahi kuishikilia Lipumba, ya Uenyekiti.

"Hata kama Lipumba angelikuwa mwenyekiti Halali wa CUF (kwamba anatambuliwa na chama na vikao vyake) basi asingelikuwa na mamlaka ya kuteua Katibu Mkuu mpya.
Kwa hiyo, sisi ndani ya CUF hatushughulishwi na matamko ya watu waliochanganyikiwa, nawashauri mpelekeni MIREMBE lakini huko njiani mnaweza kupigwa mabomu na akaondolewa mikonononi mwenu na kurudishwa Buguruni.

"Hivi sasa serikali na vyombo vyake hawalali, lengo lao ni kuhakikisha kuwa Lipumba anafanya kile walichomtuma, kile alichojaribu kukifanya mwaka 2015 lakini CUF ikabaki kuwa moja, imara na iliyojipatia ushindi mkubwa kihistoria." ameandika Mtatiro

Tujikumbushe

Profesa Lipumba alitangaza kumvua Ukatibu Mkuu Maalim Seif akidai Baraza Kuu la Uongozi Taifa la Chama cha Wananchi (CUF) limefikia uamuzi huo kutokana na sababu mbalimbali ambapo mojawapo ni Maalim Seif kutofika ofisini na kutohudhuria kwenye vikao vya chama vinavyotambulia kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.  Jambo hilo limeonekana kuzidi kuchochea mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho.

No comments

Powered by Blogger.