Kauli ya Godbless Lema kuhusu wabunge CCM waliokwenda kumsalimia gerezani kuitwa wasaliti
Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameibuka na kueleza kushangazwa na kauli
ya Rais Dk. John Magufuli kwamba wabunge wa CCM waliotaka kwenda
kumwona gerezani walikuwa wasaliti.
Lema alisema anatarajia Spika wa Bunge, Job Ndugai, atatoa msimamo juu ya kauli ya kiongozi huyo wa nchi.
Kauli
hiyo ya Lema imekuja siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli,
kuripotiwa na chombo kimoja cha habari kwamba alishangazwa na hatua ya
baadhi ya wabunge wa CCM waliounda kamati ya kutaka kwenda kumtembelea
Lema gerezani.
Katika
mkutano wake na wabunge hao juzi uliofanyika Ikulu ndogo ya Chamwino
mkoani Dodoma, Rais Magufuli alisema amekuwa akielezwa kuwa kamati hiyo
ilikuwa imepanga safari za kutaka kwenda kumwona Lema alipokuwa gerezani
jambo ambalo alilifananisha ni sawa na usaliti kwa chama chake.
Katika
taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Lema alisema kitendo cha
wabunge hao kutaka kumtembelea si usaliti bali ni upendo ambao ni muhimu
kwa binadamu yeyote pale anapokuwa na matatizo.
Lema alikaa gerezani kwa muda wa miezi minne kwa kukosa dhamana kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
“Mheshimiwa
Rais Magufuli nakusalimu. Nimetoka gerezani hivi karibuni ambako
nilikuwa huko kwa zaidi ya miezi minne kwa kunyimwa masharti ya dhamana
kwa dhamana iliyokuwa wazi.
“Nimeona
kwenye vyombo vya habari leo kwamba wale wabunge waliokuwa wanataka
kunisalimia nilipokuwa magereza ni wasaliti wa chama cha CCM.
“Mheshimiwa
Rais wengi walinisalimia wakiwemo wachungaji, masheikh, wabunge na
viongozi mbalimbali, sidhani kama hatua hii ilikuwa ni usaliti isipokuwa
upendo ambao ni muhimu kwa binadamu yeyote pale anapokuwa na matatizo.
“Mheshimiwa
Rais nimeogopa sana kwa kauli hii, je Taifa linakwenda wapi? Hivi kweli
sisi wabunge ni maadui? Kama viongozi tutafikiri utengano ni moja ya
njia ya kuimarisha vyama vyetu, bila shaka tutakuwa tunalitendea Taifa
ubaya,” alisema Lema.
Mbunge huyo alisema dhambi hiyo ikikomaa ni wazi kwamba lugha za kidini, ukanda na ukabila hazitaacha kukomaa.
Alisema
ni muhimu sasa wakajenga utamaduni wa kuhimiza mshikamano wa kitaifa
bila kujali itikadi kama kweli wanapenda masikini na wanyonge.
“Nawaomba
wabunge wenzangu walionijali wakati niko gerezani wasijisikie vibaya
kwani walifanya jambo jema na muhimu kwa wakati muhimu sana katika
maisha yangu ninatarajia kuwa Spika wa Bunge atatoa neon juu ya kauli
hii ya Rais.
“Mheshimiwa
Rais wakati wa msiba wa Christina Lissu dada yake na Tundu Lissu,
nilikuona katika msiba ule wewe na mama yetu mke wako, je wewe ulikuwa
unasaliti chama chako?
“Meshimiwa
Rais neno la Mungu linasema wapendeni maadui zenu, waombeni wanaowadhi,
wabarikini wanaowaonea kwani kufanya hivi ni kuishi kwa thawabu za
Mwenyezi Mungu,”alisema Lema.
Mbunge
huyo alisema pamoja na hali hiyo ya kuzuiwa lakini aliwashukuru wabunge
wa CCM kwa kwenda kumjulia hali, akiwa nyumbani kwake baada ya kutoka
gerezani.
“Sina
la kusema katika hili kama Rais alikuwa anajua hawakuja kuniona
gerezani lakini niwashukuru wabunge wa CCM wote waliokuja kunijulia hali
nyumbani. Sisi kama nchi tunatakiwa kuwa na umoja badala ya kuanza
kubaguana kwa itikadi zetu za vyama.
“Mdogo
wangu wa kike amepata mchumba lakini familia ya huyo mchumba wake
inatokana na CCM je tuvunje vikao vya harusi kwa sababu ya tofauti ya
vyama?
“Jibu
ni hapana sisi ni Watanzania ni lazima tuishi kwa kupenda na kwa umoja
kama ambavyo utamaduni wetu unatutaka na si vinginevyo,” alisema.
Lema
alikamatwa Novemba 2, mwaka jana mjini Dodoma nje ya viwanja vya Bunge
na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Novemba 4 mwaka
jana akikabiliwa na kesi mbili namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya
Rais Dk. John Magufuli.
Katika
kesi ya kwanza ya jinai namba 440, anadaiwa kati ya Oktoba 22 mwaka
jana maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro, katika mkutano wa
hadhara alitoa maneno yenye kuleta tabaka miongoni mwa jamii kwa kutoa
matamshi yenye chuki, kuibua nia ovu kwa jamii.
Katika
kesi ya pili namba 441, alidaiwa kwamba, Oktoba 23, mwaka jana katika
mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa,
Lema alitoa maneno kuwa:
“Kiburi
cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu,
nimeota Mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshamchukua maisha yake,”.
Februari
27, mwaka huu, Mahakama ya Rufaa Tanzania ilifuta rufaa mbili za
Jamhuri dhidi ya Lema baada ya mawakili wa Serikali kuieleza mahakama
hiyo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hana nia ya kuendelea na rufaa,
hivyo kuiomba mahakama kuzifuta rufaa hizo zilizokuwa zinahusu dhamana
ya mbunge huyo.
Post a Comment