TCRA Yazipiga Pini Michuzi TV, Ayo TV na Global TV, Yaandaa Kanuni kwa TV Mtandao
Na Sultani Kipingo, Globu ya Jamii
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezitaka Michuzi TV, AYO TV na Global TV kusitisha huduma zao za TV mtandaoni hadi hapo kanuni za usajili rasmi ambazo mamlaka hiyo imesema inaandaa kwa huduma hizo zitapokuwa tayari.
Barua hiyo, iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu Mhandisi James Kilaba tarehe 30 January mwaka huu, imevitaka vyombo hivyo ambavyo vinapendwa sana nchini na nje ya nchi kuacha mara moja kutoa huduma za TV mtandaoni.
“Kwa mujibu wa section 13 (1) of the electronic and postal communications Act Cap 306, sheria za Tanzania zinahitaji watoa huduma zozote za aina hiyo wanahitaji leseni kutoka mamlaka ya mawasiliano”, imesema barua hiyo.
Wamiliki wa mitandao hiyo – Millard Ayo, Ankal Issa Michuzi na Abdallah Mrisho – wameeleza kushtushwa kwao kwa agizo hilo la ghafla, tena wakati hata kanuni zenyewe hazijawekwa.
“Gloval TV ipo tayari hata leo kukamilisha taratibu za usajili – kama zingekuwepo – na kwa sababu bado kukamilika tunaomba kupewa muda zaidi wa kuendelea kutoa huduma hii ya bure tukiwa chini ya uangalizi wakati tunasubiria kanuni hizo mpya,” alisema Abdallah Mrisho, Meneja Mkuu wa Global Publishers.
Ankal Michuzi na Millard Ayo waliunga mkono kauli hiyo na kwa pamoja watatu hao wameomba kuonana na mkurugenzi wa TCRA ili kuwasilisha maombi rasmi ya kuruhisiwa kuendelea kutoa huduma hiyo kwa muda wakati kanuni zikisubiriwa.
Bahati mbaya Mhandisi Kilaba alikuwa safari na swala hilo limepangwa kushughuliwa ataporejea wiki ijayo.
“Ukizingatia kwamba tumekuwa tunatoa huduma hii kwa muda mrefu na haijulikani kanuni zitakuwa tayari lini tunaomba TCRA iangalie namna ya kufanya ili wananchi wanaotutegemea sana kwa taarifa mbalimbali wasikose huduma hii”, alisema Ankal. Hata hivyo vituo hivyo vitatu vinaendelea kuhudumu nje ya mwenendo wa TV mtandao, ambapo kwa sasa vitaendelea kuhudumu kwa kutumia majina ya blog zao.
Ayo TV, Michuzi TV na Global TV, ambazo zinaongoza kwa mbali kwa kutazamwa na watu wengi nchini na nje ya nchi, ni TV mtandao pekee zilizoitikia mwito wa TCRA, kati ya vituo mtandao takriban 51vinavyosadikika vinatoa huduma za TV mtandao nchini.
Ankal Issa Michuzi wa Michuzi TV, Millard Ayo na Askofu wa Ayo TV na Abdallah Mrisho wa Global TV wakitoka makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano walikoitwa kuchukua barua zao zinazowazuia kuendelea kutoa huduma za TV mtandao hadi hapo kanuni za usajili na leseni utapokamilika.
Post a Comment