Kifo cha Denti Chuo Kikuu Chazua Utata! Ndugu wapigwa butwaa washindwa kuamini
DAR ES SALAAM: Kifo cha mwanachuo wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mkwawa kilichopo mkoani Iringa, Matrona Kileo (23), mkazi wa Sanya-Juu, Moshi mkoani Kilimanjaro, kimezua utata baada ya kuwepo madai kuwa amefariki dunia kwa kuchinjwa au kujichinja, kisa kikielezwa ni kukosa mkopo wa elimu ya juu.
Tukio hilo lilijiri hivi karibuni baada ya Matrona kudaiwa kutoweka kuanzia saa 4 asubuhi na kupatikana saa 9 alasiri akiwa amefariki dunia na mwili wake ukiwa umetupwa kwenye dampo (maarufu mtaa wa Wasomali), eneo la Bomang’ombe, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro. Baada ya kusimulia mkasa wa kusikitisha wa Matrona,Wikienda lilichimba undani wa kifo cha binti huyo kilichowashangaza ndugu, jamaa na marafiki na kugundua utata kuhusu mambo yafuatayo;
WAKATI ANAFARIKI DUNIA
Habari za kiuchunguzi kutoka kwa vyanzo vyetu vya kuaminika zilieleza kuwa, Matrona amekulia kwa shangazi zake huko SanyaJuu na huko ndiko alikokuwa akiishi siku zote. Ilifahamika kuwa, Matrona hakuwa anaishi na mama yake mzazi na hata wakati mauti inamfika alikuwa anaishi kimyakimya kwa rafiki yake.
KWA NINI RAFIKI YAKE?
Ilidaiwa kuwa, katika kuishi kwake, mwaka juzi Matrona alikutana na mwanamke mmoja kwenye uchaguzi mkuu ndipo wakaanzisha urafiki ingawa mwanamke huyo inasemekana ni mkubwa kiumri ukimlinganisha na marehemu.
MAISHA YA CHUONI
Ilielezwa kuwa, akiwa chuoni, Matrona alionekana kuwa na mawazo mengi lakini haikufahamika kama tatizo lilikuwa ni mkopo au la, lakini baada ya muda, alianza kulalamika kuumwa kichwa.
MAMA, RAFIKI WAMUENDEA IRINGA Ilidaiwa kuwa, baada ya kuumwa kwa muda mrefu, yule mwanamke ambaye anadaiwa kuwa ni rafiki yake, alifunga safari hadi chuoni kwa marehemu mkoani Iringa kwa kutumia gari binafsi akiwa na mama mzazi wa marehemu na kumchukua.
Marehemu Matrona Kileo
WIKI MBILI KWA RAFIKI YAKE
Iliendelea kusemekana kwamba, kilichoshangaza ni kwa nini mtu ukae na mtoto wa mtu kwa wiki mbili bila kutoa taarifa kwao hadi mauti inamkuta? Ilidaiwa kuwa, ukiangalia kutoka hapo Boma kwa huyo mama hadi Sanya-Juu ni muda wa dakika 45 au saa moja na nauli ni shilingi elfu moja tu lakini kwa nini asiende naye kwao kama aliweza kumfuata Iringa?
RAFIKI HAFAHAMIKI KWENYE FAMILIA
Iliendelea kudaiwa kuwa, rafiki huyo wa Matrona hakuwa anafahamika kwenye familia ya denti huyo.
MAUTI YAMKUTA WAKIJUA YUKO CHUO
Kwa mujibu wa chanzo hicho, familia ilishtushwa kuambiwa kuwa Matrona ameokotwa Boma-Ng’ombe akiwa amefariki dunia wakati wao walikuwa wanajua kuwa binti yao yupo chuoni Iringa.
MASHUHUDA: HAKUJICHINJA, KACHINJWA
Habari nyingine kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo zilieleza kuwa, kwa jinsi ambavyo mwili wa marehemu ulikutwa ni vigumu kuamini kuwa alikuwa amejichinja badala yake ilidaiwa alichinjwa kwa sababu mwili wake ulikuwa na majeraha ya visu, bisibisi na kuvunjwa goti moja. Baada ya kuona utata huo, Wikienda liliwasiliana na ndugu wa marehemu lakini simu yake iliita bila kupokelewa.
MKUU WA CHUO AFUNGUKA Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, Profesa Kiliani alipoulizwa juu ya tukio hilo alikuwa na haya ya kusema:
“Ni kweli kuna tukio la mwanafunzi wetu Matrona kufariki dunia, lakini mimi sina maelezo mengi zaidi, kama ni kweli ni mkopo au jambo lingine ndiyo limesababisha kifo chake. Kwa sasa liko chini ya vyombo vya dola, hao ndiyo wataweza kutupa majibu sahihi.”Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, ASP Wilbroad
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, ASP Wilbroad Mtafungwa alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo alisema yuko kwenye shughuli nyingine ya kijamii hivyo atafutwe siku ya pili yake. Marehemu Matrona alizikwa Februari 8, mwaka huu kwenye Makaburi ya Uru yaliyopo kijijini kwao, Sanya-Juu.
CHANZO: GABRIEL NG`OSHA| IJUMAA WIKIENDA
Post a Comment