ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-15

 
NYEMO CHILONGANI
Wazazi wakachanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka Melania kuanguka chini kama mzigo. Wakamsogelea, pale chini alipokuwa alikuwa kimya kabisa. Kila mmoja akashangaa, wakachukua simu na kuanza kuzungumza na mtu aliyekuwa upande wa pili ambaye aliwaambia kwamba kulikuwa na ajali mbaya ya gari ilikuwa imetokea na mtu aliyekuwa na simu hiyo alikuwa hoi.
Hawakutaka kuchelewa, wakamchukua Melania na kumpeleka nje ambapo wakampandisha ndani ya gari na kuanza kumpeleka hospitali. Njiani, walijaribu kumpa huduma ya kwanza lakini msichana huyo hakuweza kuzinduka.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika Hospitali ya Maria iliyokuwa Msasani, wakagawana, wengine wakaelekea katika Hospitali ya Palestina alipokuwa amelazwa Godson.
Walipofika na kuulizia mapokezi, wala halikuwa jambo gumu kumpata kwani tukio hilo lilitokea muda mchache uliopita na ilikuwa ajali mbaya. Wakaelekezwa katika wodi aliyokuwepo na kuambiwa kusubiri.
“Anaendeleaje?” aliuliza baba yake Godson.
“Bado hali yake si nzuri! Naomba mtuache kwanza,” alisema daktari kwa harakaharaka kama mtu aliyekuwa akiwahi kitu fulani.
Walikuwa wakijaribu kuyaokoa maisha ya Godson, alikuwa kwenye hali mbaya, kichwa chake kilichanika mpaka kuzifanya damu kuanza kutoka puani mwake. Watu walishangaa, mbali na kupasuka huko kichwa, bado mwili wake ulikuwa umechunika na kifuani alikuwa na kovu kubwa kwani alipotolewa dirishani, alitolewa nje kupitia kioo cha mbele na kifua chake kuwa kitu cha kwanza kilichofika kwenye barabara ya lami.
“Atapona?” aliendelea kuuliza baba yake huku machozi yakianza kumtoka.
Walisubiri mpaka baada ya saa mbili ambapo Bi Pamela na mama yake Godson walipofika mahali hapo ambapo wote kwa pamoja walikuwa wakilia tu. Hakukuwa na mtu aliyeruhusiwa kuingia ndani kwani hali aliyokuwa nayo Godson haikuwa nzuri hata kidogo.
Baada ya kukaa hapo kwa saa mbili, mlango ukafunguliwa na dakjtari mmoja aliyevalia koti kubwa kutoka huku uso wake ukionyesha kwamba kulikuwa na hali mbaya sana humo ndani alipotoka.
“We want to see him, how is he?” (tunahitaji kumuona, anaendelea?) aliuliza mama yake Godson huku akifuta machozi yake kwani kama kulia, alilia sana.
“Hali yake si nzuri, ni lazima tumuhamishe hospitali na kumpeleka Muhimbili,” alijibu daktari huyo, wakati anaongea, mlango ukafunguliwa, Godson alikuwa kimya juu ya machela, ikaanza kusukumwa kuelekea nje ambapo tayari gari la wagonjwa lilikuwa mahali hapo.
“Godson...Godson kijana wangu...” aliita mama yake Godson huku akilia kama mtoto, wakati akisema maneno hayo, tayari aliiwahi machela na kutaka kumuamsha kijana wake aliyekuwa kimya kabisa.
“Mama! Subiri tumuwahishe hospitali,” alisema daktari huku manesi wakimsogeza pembeni.
Safari ya kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikaanza, kila mmoja alikuwa na hofu kwamba hiyo ingekuwa nafasiu ya mwisho kwa Godson kwani kwa jinsi alivyokuwa ameumia, kwa jinsi mwili wake ulivyofungwa bandeji zilizokuwa zimelowanishwa damu, ilionyesha kabisa kwamba asingeweza kuinuka tena pale kitandani alipokuwa.
****
Moyo wa Nicholaus ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama kweli msichana Melania alimkomoa kwa kuzifuta picha zile katika simu yake na kwenye barua pepe yake. Alikasirika mno, moyo ulimuuma na kila wakati alipokuwa akilifikiria jina la msichana huyo, alihisi kuwa na moyo wa kutaka kulipiza kisa kwa kile alichokuwa amekimfanyia.
Siku za kwanza hakulala, aliumia, alitamani kuondoka Australia na kwenda Tanzania kwa ajili ya kumkomesha msichana huyo. Moyo wake ulibadilika, mapenzi aliyokuwa nayo kwa msichana huyo yakapotea na chuki kubwa kuutawala moyo wake.
Hakuonekana kuwa na raha, alikaa huku akionekana kuwa na mawazo tele, kwake, kwa kile kilichokuwa kimetokea kilionekana kuwa kama dharau hivyo ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba anamkomoa msichana huyo
Aliendelea kusoma nchini Australia na mwaka mmoja ulipomalizika, akarudi nchini Tanzania. Hakutaka kumtaarifu mtu yeyote, hakutaka kuwaambia wazazi wake kwani alirudi kwa ajili ya kufanya kazi ya kulipa kisasi tu kwa msichana Melania.
Akaanza kumfuatilia, akagundua kwamba msichana huyo alikuwa kwenye uhusiano na mwanaume mwingine, moyo wake ulimuuma, hakutaka kuona Melania akiwa kwenye uhusiano wowote ule, hivyo akapanga kummaliza mwanaume huyo.
Kitu cha kwanza kilikuwa ni kumfuatilia, alitaka kujua anapoishi, hilo halikuwa tatizo, akagundua kwamba jamaa huyo alikuwa akiishi Mbezi Beach hivyo kuhitaji msaada kutoka katika Kundi la Black Ninja lililokuwa na makazi Kinondoni kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo.
“Kitu cha kwanza tunahitaji kumjua huyo mtu,” alisema kiongozi wa kundi hilo aliyejiita Don King.
“Hakuna tatizo!”
Akawachukua vijana wa kundi hilo na kwenda nao mpaka Mbezi Beach ambapo wakaanza kumsubiria Godson nje ya nyumba yao, alipotoka ndani ya jumba hilo, vijana wawili wakamfuata, wakalisimamisha gari lake na kuanza kuzungumza naye.
“Hivi kwa mzee Mkude ni wapi?” aliuliza kijana mmoja, huyu alijiita Dracula.
“Mzee Mkude? Wala simfahamu mtu huyo,” alijibu Godson huku akionekana kutokuwa na hofu kabisa na watu hao.
“Humfahamu kweli? Mzee mmoja ana mbwa kumi, tumesikia anaishi huku,” alisema kijana mwingine aliyejiita Lizard.
“Wala simfahamu!”
“Basi sawa. tunashukuru!”
Hawakuoneekana kama watu wabaya, waliongea huku wakiwa na uhakika kwamba waliyekuwa wakiongea naye alikuwa Godson, mtu aliyekuwa akihitajika sana. Kazi yao kwa wiki nzima ilikuwa ni kumfuatilia, walitaka kuhakikisha wanafanikiwa kumuua kama walivyotakiwa kufanya.
Baada ya siku kadhaa kukatika, ndipo wakaandaa gari lao kubwa aina ya Lori, walikuwa na ratiba yake nzima, walijua kila siku alipokuwa akiamka, breki ya kwanza ilikuwa ni kwenda kazini na jioni alikuwa akielekea gym kabla ya kurudi nyumbani na baada ya hapo anakuwa na mizunguko kadhaa.
Walichokifanya, kwa kuwa alikuwa akifanya kazi katika Kampuni ya Amazon iliyokuwa katika jengo la Plaza, Ubungo, wakajua kwamba kila siku ilikuwa ni lazima kupitia Barabara ya Shekilango kwenda gym iliyokuwa Mwenge, hakutaka kupita Barabara ya Morogoro na kuunganisha Barabara ya Sam Nujoma kwa kuwa kulikuwa na foleni.
Walimfuatilia na siku hiyo ndipo walipojipanga. Wakaliweka lori lao maeneo ya Sinza Mori na wengine wakawa wanafuatilia kwa nyuma. Walipofika Palestina wakamwambia jamaa aliyekuwa na lori ajiandae na wale waliokuwa na Godson, mmoja akalipeleka gari lake aina ya coaster mbele ya gari la mwanaume huyo na mwingine akiwa nyuma, wakamuweka mtu kati, ili asione kile kilichokuwa kikija mbele na hata gari lililokuwa likija nyuma.
Godson hakujua kilichokuwa kikiendelea, hata gari lilipofika Sinza Makaburini, hakuweza kuliona lori lililokuwa likija kwa kasi kule mbele yake. Wakati lori lile likiwa limechochewa, kasi kubwa, alichokifanya dereva wa coster iliyokuwa mbele ni kukata kona kushoto, njia ya kuelekea katika Baa ya Honey Pot na kumwacha Godson peke.
Godson alishtukia kuliona lori likiwa mbele yake, alijitahidi kutaka kulikwepa lakini hakufanikiwa, liri lile lililokuwa kwenye mwendo wa kasi likalipiga gari lake, kishindo kikubwa kikasikika, watu wakashika vichwa, Godson akatolewa ndani ya gari, akapiga kichwa kwenye kioo cha mbele cha gari lake, kikavunjika, akatupwa nje na kujipigiza kwenye lami, hakujua kilichoendelea baada ya hapo, akabaki kimya kabisa, kila mtu akajua kwamba tayari jamaa alikufa hapohapo.
****
“Tell me the truth, Caspian, tell me the truth,” (niambie ukweli, Caspian niambie ukweli) alisikika msichana mmoja kwenye simu.
“What do you want me to tell you?” (unataka nikwambie nini?)
“Who is this Christine?” (huyu Christina ndiye nani?)
“I don’t know what you are talking about,” (sijui unazungumzia nini)
“I saw messages, you were chatting with her,” (nimeona meseji ulikuwa unachati naye)
“You are not serious,” (huna uhakika)
“I saw it! Let me show you,” (niliona! Acha nikuonyeshee meseji zote)
Ilikuwa kimbembe, kila kona watu walikuwa wakigombana, siri zilikuwa wazi, wale waliokuwa wakitumia mtandao wa Facebook, hakukuwa na amani tena. Meseji zao zote zilikuwa nje, hakukuwa na siri tena, watu walishindwa kuelewa ni kitu gani kilichokuwa kimetokea.
Wale waliofanya siri, siku hiyo kila kitu kilikuwa wazi kabisa. Hakukuwa na amani, meseji zote za kimapenzi zilikuwa nje. Mbali na meseji hizo, mpaka picha za watu walizotumiana zilionekana kwenye wall zao.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa na uwezo wa kuzifuta meseji wala picha hizo. Watu walilalamika mno, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea. Watumiaji wa mtandao huo wakachanganyikiwa, watu wakajua kwamba kulikuwa na mabosi waliokuwa wakilala na wafanyakazi wao, kulikuwa na wanaume waliokuwa wakilala na watoto wao, yaani kila siri ambayo ilikuwa katika mtandao wa kijamii wa Facebook, kipindi hicho ilikuwa wazi.
“Unalia nini?”
“Kumbe unatembea na rafiki yangu!”
“Hapana mpenzi! Nani kakudanganya?”
“Na mlitumiana picha za utupu!”
“Hapana! Nani kakwambia hayo?”
“Ingia Facebook!”
“Kuna nini kwani? Unanichanganya sana.”
“Nimesema ingia. Julian, sitaki unioe, sitaki tena ndoa, kumbe unatembea na rafiki yangu, tena si huyo tu, marafiki zangu wote umewatongoza, kwa nini? Kwa nini ulilala nao? Halafu leo unasema unataa kunioa? Kwa nini umeuumiza moyo wangu?” alilalamika msichana mwingine.
Hali iliendelea kuwa mbaya, kila kona kulikuwa na matatizo. Meseji zao za siri zilikuwa wazi, kila mmoja alikuwa na uwezo wa kuingia kwenye akaunti ya mtu yeyote na kufanya kitu chochote kile kikiwa ni kuangalia meseji zote ambazo waliwasiliana.
Wale waliokuwa kwenye mipango ya kuoana, hakukuwa na ndoa tena, siri zilivuja kwamba wanandoa waliotarajiwa kufunga ndoa, kumbe walikuwa na mahusiano ya kimapenzi na watu wengine.
Ilikuwa ni kilio dunia nzima, hakukuwa na usalama, kila siri ikawekwa wazi na hakuna aliyejua ni jambo gani lilikuwa limetokea.
Wakati hayo yakiendelea, ndani ya jengo la Kampuni ya Facebook watu walikuwa wamechanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka hali hiyo kutokea.
Kuingiliwa kwa mtandao wao na meseji kusomwa, watu wengi walijiua, ilikuwa ni aibu kubwa, wengine wakagundulika kwamba walikuwa wakifanya mapenzi ya jinsia moja, yaani kila kitu kilichokuwa siri kwenye Mtandao wa Facebook, kwa kipindi hicho kilikuwa wazi, na kila mtu akikiona zikiwemo meseji na picha mbalimbali za utupu walizokuwa wametumiana.

Je, nini kitaendelea?
Kwa nini siri za Mtandao wa Facebook zimevuja?
Je, Godson ataweza kupona?

No comments

Powered by Blogger.