Waziri Mkuu Aagiza Akiba Ya Mahindi Iliyopo Iendelee Kutunzwa
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea na kuagiza
akiba ya mahindi iliyopo iendelee kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.
Ametoa
agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na
baadhi ya watumishi wa NFRA Kanda ya Songea pamoja na viongozi na
watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kukagua akiba ya nafaka
iliyomo kwenye maghala ya kituo hicho.
Waziri
Mkuu alisema mabadiliko ya tabia nchi yamefanya mvua zichelewe kunyesha
katika mikoa mingi nchini ukiwemo mkoa wa Ruvuma ambao kwa kawaida
mwezi Januari mvua ya kutosha inakuwa imeshanyesha na huwa kuna baridi
nyingi.
“Angalieni
ninyi wenyewe hali ya joto iliyopo hivi sasa, kwa kawaida mvua
ingeshaanza kunyesha mwezi huu na mahindi yangekuwa yameanza kurefuka.
Lakini hadi leo (jana) naambiwa mvua imenyesha mara mbili tu na mahindi
yaliyopandwa yameanza kunyauka.”
“Kama
mvua haijanyesha hadi leo, ni lazima tuchukue tahadhari, na hata mvua
ikija hatujui itaendelea kunyesha hadi lini na kwa kiasi gani. RC, Ma-DC
na ma-DED toeni elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula.
Waambieni waachane na ngoma za unyago na sherehe za kipaimara ambazo
hutumia kiasi kikubwa cha chakula,” alisisitiza.
“Msiruhusu kutoa mahindi yaliyopo na kuyauza. Hizo tani 10,500 zilizopo ziendelee kuhifadhiwa hadi tutakapoamua vinginevyo,” alisisitiza.
Kwa
upande wake, Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Bw. Majuto Chabruma
alimweleza Waziri Mkuu kwamba msimu huu walipanga kununua tani 22,000 za
mahindi kutoka kwa wakulima lakini hadi kufikia Desemba 31, 2016,
wamefanikiwa kununua tani 10,335.3 zenye thamani ya sh. bilioni 5.28.
Alisema
kanda ya Songea ni miongoni mwa kanda saba zilizo chini ya NFRA ambayo
inahudumia mkoa wa Ruvuma. Alizitaja kanda nyingine zinazohudumia mikoa
yote nchini kuwa ni Arusha, Kipawa, Dodoma, Shinyanga, Makambako na
Sumbawanga.
“Kanda
ya Songea inayo maghala sita yenye uwezo wa kuhifadhi ytani 29,000 za
nafaka. Lakini hivi sasa kanda hii imeingizwa kwenye Mpango wa Kuongeza
Uwezo wa Hifadhi (NFRA Storage Expansion Project) na lengo la Wakala ni
kufikia uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 ifikapo mwaka 2020,” alisema.
“Kanda
ya Songea tumenunua viwanja viwili vyenye ukubwa wa mita za mraba
16,986 ambapo zitajengewa silos 12 zenye uwezo wa kuhifadhi tani 46,000
na maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 kila moja na hivyo
kuwa na ongezeko la tani 56,000 mradi huu utakapokamilika.”
Alisema
kukamilika kwa mradi huo, kutaiwezesha kanda ya Songea kuwa na uwezo wa
kuhifadhi tani 85,000 ndani ya maghala na vihenge kutoka tani 29,000 za
sasa.
Alipolizwa
ni kwa nini hawajaweza kutimiza tani zote walizojipangia kununua, Bw.
Chabruma alisema kuimarika kwa barabara za mkoa huo kumetoa changamoto
kwa wakala kwani wananchi walianza kuuza mahindi kabla ya msimu wa
ununuzi haujaanza (kawaida ni Julai mosi kila mwaka).
“Kuimarika
kwa barabara za mkoa kumesaidia kufungua biashara na mikoa ya jirani na
hivyo kuwawezesha wakulima wa Ruvuma kupata soko nje ya mkoa kabla NFRA
haijaingia sokoni na kuanza kununua nafaka kwa wakulima vijijini,” alifafanua.
Alisema
changamoto nyingine inayowakabili ni ubora hafifu wa nafaka kutoka kwa
wakulima ambao alisema ni tatizo tangu hatua za awali za uzalishaji wa
mazao ya chakula na biashara.
“Ubora
hafifu wa zao la mahindi ulionekana zaidi kwenye nafaka zilizooza,
punje zilizovunjika, wadudu hai, rangi mchanganyiko na takataka,” alisema.
Waziri
Mkuu leo anatembelea wilaya ya Songea na kukagua kituo cha kupoozea
umeme katika kijiji cha Mtepa, atakagua kituo cha afya cha Madaba ambako
pia atazungumza na watumishi wa ummakatia sekondari ya Madaba kabla
kuhutubia mkutano wa hadhara. Pia atakagua shamba la miti la TFS katika
kijiji cha Wino.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Post a Comment