TCRA Yatishia Kuzifutia Leseni Kampuni za Simu
Mamlaka
ya Mawasiliano nchini (TCRA) imetishia kusitisha kwa muda au kufuta
kabisa leseni ya biashara kwa kampuni zote za mawasiliano nchini,
zitakazoshindwa kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE)
Hatua
hiyo ni kulingana na sheria mpya ya fedha ambayo imetoa ukomo wa hadi
Desemba 31 mwaka jana kampuni hizo ziwe zimejisajili katika soko hilo.
Akizungumza
na wanahabari jijini Dar es Salaam hii leo; Mkurugenzi Mkuu wa TCRA
Mhandisi James Kilaba amesema kwa sasa wanasubiri maelezo kutoka Mamlaka
ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kuhusu idadi ya kampuni za
mawasiliano zilizokidhi sifa za kusajiliwa katika soko la hisa kwa ajili
ya kuchukua hatua kwa zile zilizokaidi kutekeleza agizo hilo la
kisheria.
Mhandisi
Kilaba amesema TCRA imeikabidhi CMSA orodha ya kampuni zaidi ya 80 za
mawasiliano, orodha ambayo CMSA itaipitia kwa lengo la kuchuja na kupata
kampuni ambazo zinastahili kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es
Salaam.
Kauli
ya Mhandisi Kilaba imekuja huku taarifa kutoka soko la Hisa la Dar es
Salaam zikionesha kuwa ni kampuni tatu pekee ndizo zimejisajili katika
soko hilo, licha ya muda wa kufanya hivyo kufikia ukomo wake Jumamosi ya
Desemba 31 mwaka jana.
Post a Comment