Serikali Yafuta Posho Za Vitafunwa, Mazingira Magumu
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini
kuhakikisha fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya posho mbalimbali
zisizokuwa za kisheria zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Ametia
agizo hilo leo (Jumanne, Januari 3, 20017) wakati akizungumza na
watumishi wa Manispaa ya Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.
“Kuanzia
sasa marufuku Wakurugenzi kutoa posho zisizotambulika kisheria zikiwemo
za mazingira magumu, kujenga uwezo na vitafunwa katika halmashauri zenu
na badala yake fedha hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo,”
amesema.
Agizo
hilo litawezesha Jiji la Dar es Salaam kuokoa sh bilioni 130 zilizokuwa
zitumike na Halmashauri na Manispaa za jiji hilo, ambazo kwa sasa
zitaingizwa kwenye miradi na shughuli za maendeleo.
Aidha,
Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa mujibu
wa sheria na kuacha kutumia fedha kinyume cha utaratibu na
watakaobainika Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria.
“Katika
halmashauri zetu kila mtumishi anashiriki katika ukusanyaji wa mapato
hadi walinzi, lakini mwisho wa siku vitafunwa huliwa na wachache
wanaojiita wakubwa huku wengine wakisikilizia kwa nje. Jambo hili
haliwezekani,” amesisitiza.
Waziri
Mkuu amesisitiza kwamba Mkurugenzi yeyote atakayebainika kulipa posho
hizo baada ya siku ya leo atakuwa amejifukuzisha kazi.
Aidha,
ameagiza fedha zilizokuwa zikitolewa kwa madiwani kwa ajili ya
kuhamasisha maendeleo zisitolewe moja kwa moja kwa madiwani na badala
yake zipelekwe kwenye kata husika na zifuatiliwe matumizi yake.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amezionya halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa
kila fedha zinayopelekwa kwenye halmashauri hizo inatumika kama
ilivyokusudiwa na atakayebainika kutumia kinyume hatua kali
zitachukuliwa dhidi yake.
Pia
amewataka watumishi wote wa umma nchini kuwajibika ipasavyo na
kuhakikisha wanawatumikia vyema mwananchi ikiwa ni pamoja na kuepuka
vishawishi na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ufisadi.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu ametoa siku tatu kwa watumishi 10 wa halmashauri
hiyo ambao wamehamishiwa kutoka wilaya ya Temeke wawe wameripoti katika
Manispaa hiyo, vinginevyo watakuwa wamejifukuzisha kazi.
Awali
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bw. Hashim Mgandilwa wakati akiwasilisha
taarifa ya wilaya hiyo kwa Waziri Mkuu, alisema hadi sasa asilimia 98 ya
watumishi waliotakiwa kuhamia kwenye halmashauri hiyo wameripoti
isipokuwa 10 na hakuna taarifa zozote juu yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Post a Comment